SHERH YA MISINGI MITATU

Kitabu hiki kinazunguzi misingi mitatu ya Tawhidi


SHARH YA
MISINGI MITATU

Imaam Muhammad Bin ‘Abdil-Wahhaab

شرح الأصول الثلاثة
لشيخ الإسلام محمد بن عبد الوهاب

 

Mfasiri wa matn:
Ummu Iyyaad
Kimepitiwa na:
Muhammad Baawazir Sa’iyd Baawazir
Mfasiri wa Sharh:
Abu Bakr Khatwiyb al-Atrush


Dibaji ya mfasiri    2
Historia Fupi Ya Imaam Muhammad bin 'Abdil-Wahhaab    4
Historia Fupi Ya Shaykh Swaalih al-Fawzaan    10
MASUALA MANNE JUU YETU KUYAJUA
1.    Suala la kwanza    16
2.    Suala la pili    19
3.    Suala la tatu    20
4.    Suala la nne    20
MASUALA MATATU WAJIBU KUJIFUNZA
1.    Suala la kwanza    24
2.    Suala la pili    30
3.    Suala la tatu    32
MISINGI MITATU WAJIBU KUIJUA
1.    Msingi wa kwanza    45
2.    Msingi wa pili    69
3.    Msingi wa tatu    106






Dibaji ya mfasiri

Bismillaahi Rahmaani Rahiym. Himidi zote ni Zake Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) Aliyepwekeka katika Uungu Wake, Uola Wake na Majina na Sifa Zake. Ninashuhudia ya kwamba hapana mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah na Mtume Muhammad ni mja Wake na Mtume Wake. Amma ba´ad:
Huu ni ufafanuzi (Sharh) wa Kitabu al-Usuwl ath-Thalaathah cha Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah). Sharh imefanywa na Shaykh al-´Allaamah Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan (Hafidhwahu Allaah).
Napenda kuwajulisha ndugu zangu wapendwa (Allaah Awahifadhi). Lengo langu khaswa haikuwa kufasiri Sharh hii ya Shaykh, bali lengo langu ilikuwa ni kujinufaisha mwenyewe kielimu.  Na kwa sababu hii ndio maana Sharh yenyewe nimeifasiri kwa mukhtasar tu na si yote. Hivyo nikawa nimeonelea yale madogo niliyoyasoma na kustafidi faida isiishie kwangu mwenyewe.
Kama alivyosema Mtume (´alayhis-Salaam):
“Hatoamini mmoja wenu mpaka ampendelee ndugu yake yale anayojipendea nafsi yake mwenyewe.”
Kwa ajili hii, sikupenda ninufaike mwenyewe bali nilipenda vile vile faida hii waipate ndugu zangu Waislamu. Na ninamuomba Allaah (Ta´ala) Atujaalie sote tuwe ni katika waumini wa kweli wanaopendeana na kutakiana kheri. Kwani mapenzi sampuli hii pekee ndio yatayonufaisha Aakhirah. Pia namuomba Allaah (Ta´ala) Ajaalie kazi hii tuwe tumeifanya kwa kutafuta Uso Wake Mtukufu Pekee. Na Ajaalie iweze kunufaisha Waislamu wote kwa jumla.
Swalah na salaam zimwendee Mtume wetu Muhammad, na ahli zake na Maswahabah zake.
Historia Fupi Ya Imaam Muhammad bin 'Abdil-Wahhaab

Asili yake

Jina lake ni Abul-Husayn Muhammad bin ‘Abdil-Wahhaab bin Sulyamaan bin ‘Aliy Musharrif Al-Wuhaybiy. Kabila lake ni Bani Tamiym. Amezaliwa mwaka 1115 H (1704 M) katika mji ya ‘Uyaynah kijiji cha Yamaamah ndani ya Najd, kaskazini Magharibi ya mji wa Riyadhw, Saudi Arabia. Ametoka katika familia ya Wanavyuoni kwani baba yake ‘Abdul-Wahhaab alikuwa ni Mwanachuoni maarufu wa Najd na Qaadhiy wa mji huo.
 
 
Elimu Yake

Alijifunza kusoma Qur-aan alipokuwa na umri mdogo na akaihifadhi akiwa chini ya umri wa miaka kumi. Na Allaah (سبحانه وتعالى) Alimjaalia kuwa na uhodari na akili nzuri, wepesi wa kufahamu na kumaizi jambo au somo. Alipendezewa mno kusoma kazi za Shaykhul-Islaam Ibn Taymiyyah na mwanafunzi wake Ibnul-Qayyim (رحمهما الله).

Alifanya bidii kwenye masomo yake na kuendelea kujifunza chini ya usimamizi wa baba yake. Akajifunza elimu ya Dini chini ya Wanavyuoni walioko mjini mwake wakiwemo baba yake na ‘ami yake. Alisafiri kutoka kwenda Madiynah kusoma chini ya Wanavyuoni wakubwa wa huko wakiwemo; Shaykh ‘Abdullaah bin Ibraahiym bin Ash-Shamariyyi, na Mwanachuoni maarufu wa India Shaykh Muhammad Hayaat Al-Sindi.Alikwenda Makkah pia na alitekeleza Hajj. Hatimaye akaelekea Baswrah (Kaskazini Iraq)  kutafuta elimu zaidi akasoma chini ya Wanavyuoni wa huko akawa maarufu kwa mijadala baina yake na Wanavyuoni.

Harakaat Na Mitihani
Watu wa Najd walikuwa katika shirki na bid’ah (uzushi). Walikuwa wakiabudu miungu mingi na kuabudu makaburi, miti, mawe, mapango, majini na mashaytwaan, waja wema waliojulikana kama ni mawalii. Uchawi na unajimu (utabiri wa nyota) ulisambaa pia. Hakuna aliyekataza ‘Ibaadah potofu hizo kwani watu walikuwa katika kuchuma manufaa na starehe za dunia zaidi na wakakhofia kuyapoteza hayo. Hivyo Shaykh akaona umuhimu mkubwa uliohitajika kuwarudisha watu katika msimamo wa Qur-aan na Sunnah.  Akaanza kuwalingania watu katika Tawhiyd - kumpwekesha Allaah (سبحانه وتعالى) bila ya kumshirikisha na lolote katika ‘Ibaadah. Akaazimia kujitumikisha peke yake kwa uvumilivu katika konde. Akajua hakuna lolote kitachofaulu kufanyika ila Jihaad katika Njia ya Allaah.
 Shaykh alikumbana na mitihani, misukosuko, na vitisho,  lakini alikuwa ameshategemea hali hiyo kumfikia na alikuwa tayari kukabaliana nayo kwani alitambua kuwa hilo ni jambo lisiloepukika kwa kila mlinganiaji kwani ndio  hali waliyokutana nayo Mitume wote, na Salafus-Swaalih (waja wema waliotangulia).
 Miongoni mwa mitihani aliyokumbana nayo ni kutokana na Wanavyuoni wadhaifu wasiokuwa na hoja ambao walimpinga na kumfanya akabiliane na misukosuko, vitisho na kukasirikiwa. Pia alikabiliana na misukosuko na mateso chini ya mikono ya madhalimu wa Huraymilaa. Na alipowashawishi watawala kuwahukumu wadhalimu kwa Shari’ah ya Kiislamu, ilisababisha baadhi ya watu kuyaweka maisha yake hatiani lakini Allaah (سبحانه وتعالى) Alimnusuru.
 Aliamua kurudi kwao ‘Uyaynah, ambako kipindi hicho kulikuwa chini ya utawala wa mtoto wa Mfalme ‘Uthmaan bin Muhammad bin Mu’ammar, ambaye alimpokea Shaykh kwa ukarimu na kumuahidi kumuunga mkono na kumsaidia kuwaita watu katika Uislam. Akaendelea kufundisha na kutoa da’wah hatimaye akashawishika kidhati na kwa vitendo kuondoa dini ya miungu mingi pale alipoona baadhi ya watu ni wagumu kurudi katika Uislamu. Aliweza kumshawishi gavana wa mji huo kulivunja zege lililojengewa juu ya kaburi la Zayd bin Al-Khattwaab ambaye alikuwa ni kaka wa ‘Umar bin Al-Khattwaab (رضي الله عنهما). Akavunjavunja mangome mengineyo, mapango, miti n.k. Akaamrisha Shari’ah ya Kiislamu itekelezwe kama kumpiga mawe hadi afe mwanamke aliyekiri kuwa amefanya zinaa. Shaykh aliendelea na harakati zake za vitendo na kauli ambazo zilimfanya azidi kuwa maarufu. Hatimaye akawa jaji (Qaadhiy) wa mji wa ‘Uyaynah. Lakini hakuweza kuendelea hapo kwani Mfalme alishawishiwa na viongozi wa miji ya jirani amuue Shaykh kwa vile hawakupendezewa na da’wah yake. Ikabidi afukuzwe katika mji huo.
Akakaribishwa mji wa ad-Dir’iyyah ambao ulikuwa ni jirani yake. Huko akakaribishwa ingawa kwanza alitiliwa shaka. Alifikia kwa mja mwema aliyempokea ila alimkhofia kutokukubaliwa na mtoto wa Mfalme Muhammad bin Sa’uud.  Habari zikamfikia kwanza mke wa Ibn Sa’uud ambaye alikuwa mkarimu na mwenye taqwa. Akamfahamisha mumewe kwa kumwambia, “Hii ni bahati kubwa umeletewa kutoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى) mtu ambaye anawaita watu katika Uislamu, anawaita katika Qur-aan na Sunnah za Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم). Bahati iliyoje? Mkimbilie haraka na umuunge mkono wala usimpinge au kumkataza kwa hayo”. Muhammad Ibn Sa’uud akakubali ushauri wa mkewe na akaenda kwa Shaykh na akafanya mkataba naye kwamba asiondoke nchini hapo. Ndipo Shaykh akaweka makazi yake hapo na kuendelea na da’wah. Aakaendelea na harakati za da’awah hapo Dar’iyyah. Akaheshimika na kupendwa mno na akaungwa mkono na watu.  Da’wah yake iliwaathiri na kuwapendezea mno watu. Ikaenea katika nchi za Kiislamu na nyinginezo. Wakimiminika watu na Wanavyuoni kufika hapo Dar’iyyah kujifunza kwake.
 Kama ijulikanavyo kila jema halikosi mitihani. Wakatokeza wapinzani na waliokuwa na chuki naye. Kulikuweko waliompinga da’wah yake ya kuondosha shirki na bid’ah na kuwaita watu katika Tawhiyd. Na wengineo waliompinga kabisa ni kwa sababu ya kuhofu kufukuzwa katika nafasi au vyeo vyao vya kazi. Kwa hiyo wengine walimpinga kwa ajili ya Dini, na wengine walimpinga kisiasa. Wapinzani wake walimzushia ya kumzushia walifika hadi kudai kwamba Shaykh alikuwa ni mfuasi wa Khawaarij. Na mara nyingine wakimlaumu bure bila ya dalili na nje ya upeo wa elimu zao. Hivyo yakaweko malumbano na majibishano yaliyoendelea katika mijadala kadhaa. Shaykh aliwaandikia kuwajibu madai yao, na wao walimrudishia majibu na yeye akawa akiwathibitishia ufahamu wao mbya wa shari’ah na Dini kwa ujumla kwa dalili. Ndipo wingi wa maswali na majibu yakawajumuisha watu na wakazidi kuongezeka. Baadhi ya mijadala hiyo iliandikwa na kuchapishwa katika vitabu.
 
Athari Ya D’awah Yake
Da’wah yake ya takriban miaka 50 imedhihirika na kuleta athari kubwa kwanza kwa Waislamu wa zama hizo. Watu waliacha kuabudu makaburi, miti, mawe, majini, waliacha utabiri wa nyota na kila aina ya shirki. Imewatoa pia watu katika ujinga wa kufuata mila za mababu bila ya dalili. Maamrisho ya mema na makatazo ya maovu yakalinganiwa katika Misikiti. Na hapo msimamo wa Qur-aan na Sunnah ukahuishwa na shirki na bid’ah zikapotoka. Amani na utulivu ukawafunika watu kila mahali. Na mpaka sasa da’wah yake imekuwa na umuhimu mkubwa katika jamii ya Kiislamu. Vijana khasa kutoka nchi za Magharibi na zaidi wale wanaosilimu wamekuwa na hamasa na shauku kubwa ya kujifunza Dini iliyo sahihi na si ile iliyochanganywa na shirki na bid’ah. Kwa hiyo, mafundisho ya msimamo wake wa Ahlus-Sunnah wal-Jama’ah ambao pia ndio mwendo wa Safafus-Swaalih yamekuwa kiupamble katika lengo la kutafuta elimu kwa Waislamu watakao na wapendao haki.
 
Kazi Zake
Ameandika vitabu vingi vya mafunzo mbali mbali lakini alitilia mkazo zaidi katika somo la Tawhiyd na ‘Aqiydah. Na alitumia hikma ya kuandika vitabu vidogo vidogo lakini vilivyokusanya nukta muhimu kabisa. Vilikuwa ni mukhtasari wa maudhui aliyotaka kuidhihirisha. Na vitabu hivyo vimekuja kufafanuliwa kwa kushereheshwa na Ma’ulamaa kadhaa na vimekuwa vina umuhimu mno katika vyuo vya Kiislamu vinavyofuata mwendo wa Ahlus-Sunnah wal-Jama’ah.
 Vifuatavyo ni baadhi ya vitabu vyake maarufu. Vinne vya mwanzo ni ambavyo mashuhuri zaidi kwa umuhimu wa maudhui zake. Na vinginevyo vimekusanywa na kujumishwa katika ‘Maj’muu’at Mu-allafaatil-Imaam Muhammad bin ‘Abdil-Wahhaab.
1. Kitaabut-Tawhiyd - kitabu hiki kimekuwa mashuhuri mno na kimeenea sana na somo lake limekuwa ni lenye kutoa mafunzo muhimu kuhusu kumpwekesha Allaah na kuepukana na shirki.
2. Al-Uswuul Ath-Thalaathah – kitabu kitoacho mafunzo kuhusu asili au misingi ya Uislamu.
3. Al-Qawaaid Al-Arba’h - kinatoa mafunzo ya kanuni za ufahamu wa shirki kwa ujumla.
4. Kashf Ash-Shubuhaat - kinakanusha hoja zinazojulikana na watetezi wa shirki na bid’ah.
5. Mukhtaswar Al-Inswaaf was-Sharh Al-Kabiyr
6. Mukhtaswar Zaad Al-Ma’aad
7.  Mukhtaswar As-Siyrah
8. Mukhtaswar al-Fat-h
9. Masaail Al-Jaahiliyyah
10. Adaab Al-Mashiy ilaa as-Swalaah
 
Wanafunzi Wake
Alikuwa na wanafunzi wengi mno. Miongoni mwao ni watoto na wajukuu wake ambao waliendeleza kazi yake ya da’wah na Jihaad katika njia ya Allaah, walifungua vyuo karibu na kwao wakifunza watu masomo ya Dini. Kati ya watoto wake ni Husayn, ‘Aliy, ‘Abdullaah na Ibraahiym. Na kati ya wajukuu wake ni ‘Aliy bin Husayn, na pia ‘Abdur-Rahmaan bin Hasan aliyeandika kitabu cha ‘Fat-h Al-Majiyd Sharh Kitaab At-Tawhiyd. Wanafunzi wake wengineo ni ‘Abdul-‘Aziyz bin Muhammad bin Sa’uud, Hamad bin Naaswir bin Mau’ammar na ‘Abdul-‘Aziyz bin ‘Abdillaah bin Husayn.
 
Familia Yake
Alikuwa na watoto sita; Husayn, ‘Abdullaah, Hasan, ‘Aliy, Ibraahiym, ‘Abdul-‘Aziyz. Shaykh anatokana na kizazi kinachojulikana kwa ‘Aal-Shaykh’ ambacho kimetoa Wanavyuoni kadhaa akiwemo Shaykh Muhammad bin Ibraahiym Aal-Shaykh aliyekuwa Mufti mkuu  wa awali  Saudi Arabia na Shaykh ‘Abdul-‘Aziyz Aal-Shaykh  ambaye ni Mufti mkuu wa sasa.
 
Kifo Chake
Alifariki mwaka 1206 H (1792 M) akiwa na umri wa miaka 91. Rehma za Allaah ziwe juu yake na Allaah Amruzuku Pepo ya Firdaws. Aamiyn.

 
Historia Fupi Ya Shaykh Swaalih al-Fawzaan

Jina Lake Na Kuzaliwa Kwake:
 
Jina lake ni Swaalih bin Fawzaan bin 'Abdillaah al-Fawzaan na kazaliwa 1354 (1933) H.
 
 
Malezi Yake Na Masomo:
 
Baba yake alifariki wakati bado yu mdogo, kwa hivyo alikulia katika familia ya baba yake na kujifunza Qur-aan na kusoma na kuandika na Wanachuoni katika mji wake. Ndipo akaanza kusoma katika Madrasah ya serikali katika mji wake  mwaka 1379 H. Baadaye aliendelea na masomo yake katika Madrasah ya Buraydah katika mwaka wa 1371 H. Kisha akasoma katika kituo cha kujifunza Buraydah kilichoanza kati ya 1373 H hadi 1377 H. Kisha akaendelea na masomo yake katika fani ya Shari´ah Riyaadh na akahitimu mwaka 1381 H.
 
Baada ya hapo akaendelea kusoma shahada ya pili kisha ya tatu ya udaktari katika Fiqh.
 
 
Waalimu Wake:
 
1) Shaykh 'Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz, Muftiy wa Saudi Arabia aliotangulia. Shaykh Ibn Baaz alikuwa na uaminifu sana na Shaykh al-Fawzaan na alikuwa akimpa vitabu mbalimbali avipitie na kutaka rai yake.
 
2) Shaykh 'Abdullaah bin Humayd, mkuu wa mahakama ya juu kabisa katika Baraza la Saudi Arabia huko nyuma. Alikuwa akihudhuria katika darsa zake nyingi alipokuwa akisoma Buraydah.
 
3) Shaykh Muhammad Amiyn ash-Shanqiytwiy, mfasiri bingwa wa Qur-aan wa zama zetu.
 
4) Shaykh 'Abdur-Razzaaq al-'Afifiy Mwanachuoni kutoka Misri aliyekuwa katika Baraza la Kudumu la Kutoa Fatwa (al-Lajdan ad-Daaimah) Saudi Arabia chini ya Muftiy wa wakati huo, Imaam Ibn Baaz.
 
 
Kazi Zake:
 
1) Alikuwa mwalimu katika Madrasah ya Buraydah na Riyaadh, baada ya hapo akaajiriwa kama mwalimu katika kitivo cha Shari´ah.
 
2) Alikuwa Mudiyr wa Chuo kikuu cha U-Qaadhiy Riyaadh mwaka 1396 H.
 
3) Amekuwa mjumbe wa baraza la Ma’ulamaa wakubwa katika mwaka 1407 H Saudi Arabia.
 
4) Amekuwa mjumbe wa baraza la Fatwa Saudi Arabia katika mwaka wa 1411 H.
 
5) Ni mjumbe wa baraza la Fatwa Makkah la Raabitwat-ul-´Aalam Al-Islaamiy.
 
6) Ni Imaam, mwalimu na Khatwiyb wa Ijumaa katika msikiti wa Amiyr Mutw'ib bin 'Abdil-´Aziyz, huko Riyaadh.
 
7) Anajibu maswali katika kipindi cha Radio cha ‘Nuwr 'Alaa Ad-Darb’ katika kituo cha Saudi cha Redio.
 
8) Alikuwa mshauri na msimamizi katika mitihani mingi ya kitaaluma katika ngazi za shahada ya pili na udaktari.
 
 
Vitabu Vyake:
 
Shaykh ameandika vitabu vingi na wanafunzi wake huwa wanaandika mihadhara yake ya sauti. Miongoni mwa vitabu hivyo ni:
 
1) I'aanat-ul-Mustafiyd Sharh Kitaab at-Tawhiyd. Maelezo ya kina ya Kitaab-ut-Tawhiyd, mijalada miwili.
 
2) al-Mulakhasw-ul-Fiqhi. Kitabu kifupi na maarufu cha Fiqh kinachofundishwa duniani kote.
 
3) at-Tahqiyqaat al-Mardiyyah fiyl-Mabaahith al-Fardiyyah fiyl-Mawaariyth. Moja ya vitabu maarufu katika Shari´ah ya Kiislamu cha Miyraath katika zama hizi kinachofundishwa katika Chuo kikuu cha Kiislamu.
 
 
 
 








 













 

Misingi mitatu 

Msingi ni kitu ambacho mtu hujengea juu yake kitu kingine. Na kaita kuwa ni misingi kwa kuwa kunajengewa juu yake mambo mengine ya Dini. Dini yote inajengewa juu ya mambo haya matatu: Mtu kumjua Mola Wako, Mtume Wako na Dini Yako. Haya ndio mambo ya Dini matatu kwa ujumla na ufafanuzi (maelezo) yake yatakuja huko mbele katika maneno ya Shaykh.

Bismillaahi Rahmaani Rahiym

Kaanza Risaalah hii kwa Bismillaahi Rahmaani Rahmiym, kwa kufuata Kitabu cha Allaah. Na Bismillaah hii inaanza kwa kila Suurah ila tu Suurah at-Tawbah. Hali kadhalika Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akianza kuandika Bismillaah anapoandika barua zake; kuwaandikia wafalme, raisi na watu wengine akiwalingania katika Uislamu. Ni jambo lioneshalo ya kwamba kuanza kwa Bismillaah ni Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kama jinsi Sulayman (´alayhis-Salaam) alivyoanza barua yake aliyomtumia Malkia.
Hivyo kuanza kwa Bismillaah ni jambo muhimu katika kila jambo la muhimu na kila Risaalah na kitabu. Na wale wasioanza Risaalah zao kwa Bismillaah, wameacha Sunnah. Na pengine vitabu vyao hivi vikawa havina baraka na faida kwa kuacha Sunnah. Maana yake ni kwamba naomba kinga, au naanza kwa jina la Allaah.

Tambua

Neno hili linaonesha dalili ya umuhimu wa mada. Na hii ni amri. Maana yake ni kwamba jifunze yanayokuja. Elimu ni kule kujua kitu kama jinsi kilivyo kwa sasa, ama kujua kitu kwa kinyume na jinsi kilivyo kwa sasa, hili huitwa ujinga.

Allaah Akurehemu

Hii ni Du´aa. Shaykh anawaombea wanafunzi Allaah (Ta´ala) Awarehemu. Huu ni usulubu mzuri mwalimu kwa mwanafunzi wake ili aweze kupokea na kuzingatia. Mwalimu anapaswa kuanza kwa maneno mazuri na ya kuvutia. Ama mwalimu akianza kwa maneno mazito, hili litawakimbiza anaowalingania. Aanze kwa Du´aa, maneno laini na mazuri. Ama mkaidi na mjeuri, hawa wana ulinganio mwingine. Anasema (Jalla wa ´Alaa):
وَلَا تُجَادِلُوا أَهْلَ الْكِتَابِ إِلَّا بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ إِلَّا الَّذِينَ ظَلَمُوا مِنْهُمْ
“Na wala msijadiliane na Ahlal-Kitaabi isipokuwa kwa yale ambayo ni mazuri zaidi; isipokuwa wale waliodhulumu miongoni mwao.” (29:46)
Hawa hawalinganiwi kwa njia iliokuwa nzuri. Na Akasema kuhusiana na wanafiki:
يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ جَاهِدِ الْكُفَّارَ وَالْمُنَافِقِينَ وَاغْلُظْ عَلَيْهِمْ
“Ee Nabii! Pambana jihaad na makafiri na wanafiki na kuwa mshupavu kwao.” (66:09)
Na Akasema (Jalla wa ´Alaa) kwao:
وَقُل لَّهُمْ فِي أَنفُسِهِمْ قَوْلًا بَلِيغًا 
“Na uwaambie maneno yatakayowaathiri na kuingia katika nafsi zao.” (04:63)
Watu sampuli hii wana ulinganio mwingine wakulingana na wao. Ama mwanafunzi analinganiwa vizuri kwa usulubu mzuri kwa kuwa anataka haki.

ni wajibu wetu

-    La wajibu ni lile ambalo analipwa kwalo yule mwenye kulifanya, na anaadhibiwa kwalo yule mwenye kuliacha.
-    Mustahaba  ni lile ambalo anapewa thawabu kwalo yule mwenye kulifanya, na haadhibiwi yule mwenye kuliacha.
-    Mubaahah  ni lile lisilokuwa na thawabu katika kulifanya wala adhabu kwa kuliacha.
Kauli yake ni wajibu, ni kuonesha ya kwamba sio katika mustahaba wala mubaahah. Na tukiliacha ni kuonesha kuwa ni adhabu kwetu.

kujua mas-alah manne:

Yameitwa masuala kwa kuwa ni wajibu kuyauliza.


Suala la kwanza: Elimu:
Nayo ni elimu ya kumjua Allaah, na elimu ya kumjua Mtume Wake (صلي الله عليه وسلم) na elimu ya kuijua Dini ya Kiislamu kwa dalili.

1.    Suala la kwanza
Makusudio ya elimu hapa ni ya Kishari´ah. Haya ni masuala ambayo ni wajibu kwa kila Muislamu, mwanaume, mwanamke, mtu aliye huru, mtumwa, tajiri, masikini, maliki n.k. Kila Muislamu ni wajibu kujifunza mambo haya manne. Na hili ndio huitwa waajib-ul-´Aiyn. Kama Swalah na mengineyo.  Kwa kuwa elimu imegawanyika sehemu mbili:
-    Elimu ya kwanza ni ile ambayo ni wajibu kwa kila mtu kuijua na hapewi udhuru yeyote kwa kutoyajua, nayo ni yale ambayo haisimami Dini isipokuwa kwayo. Kama nguzo tano za Uislamu, haya haijuzu kwa Muislamu kutoyajua. Ni lazima ajifunze nayo. Ajifunze maana ya Shahaadah  ambayo ni ´Aqiydah; nguzo, sharti, Sunnah za Swalah kwa kina kabisa na sio kuswali tu na wewe hujui nguzo za Swalah. Vipi Muislamu atafanya ´amali naye hajui kitendo hichi anachokifanya, vipi ataswali naye hajui Ahkaam za Swalah? Ni lazima ajifunze Ahkaam za Swalah na yanayobatilisha Swalah, Ahkaam za Zakaah, Swawm na Hajj na ´Umrah. Haya mtu hapewi udhuru kwa kutoyajua.

-    Ama elimu ya pili ni yenye kuzidi hapo katika Ahkaam za Kishari´ah ambazo Ummah kwa ujumla inazihitaji. Kama Ahkaam za biashara, matangamano, wasia, mirathi na mengineyo. Sio wajibu kwa watu wote kuyajua haya. Wakiyajua wanachuoni yatosheleza kwa wengine. Na akikosekana kabisa katika Ummah anaejua mambo haya, Ummah wote unapata dhambi. Tofauti na fungu la kwanza.
Kabla ya kwenda mbali, tujue kuwa elimu ambayo hapa ni wajibu kwa Ummah kuijua ni ya Kishari´ah ambayo imekuja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ama elimu ya dunia, kama sanaa, uinjenia na kadhalika elimu hizi ni mubaahah kujifunza nazo. Na inaweza kuwa wajibu ikiwa Ummah itazihitajia, (katika hali hiyo itakuwa ni) wajibu kwa yule atakayeweza. Lakini sio makusudio katika Qur-aan na Sunnah na (elimu) ambayo Allaah Kawasifu walioibeba na ambayo kasema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):
”Ma´ulamaa ni warithi wa Mitume (´alayhimus-Swalaat was-Salaam).”
Makusudio ni elimu ya Kishari´ah. Ama hizi elimu zingine za kidunia ni elimu mubaahah. Asiyezijua hana dhambi juu yake, na yule mwenye kujifunza imeruhusiwa kwake. Na ukinufaika Ummah kupitia elimu yake hiyo basi atakuwa ni mwenye kupata thawabu na ujira. Na  lau mtu atakufa na hakijifunza elimu hii  hatochukuliwa (adhibiwa) siku ya Qiyaamah.
Lakini atakayefariki naye hajui elimu ya Kishari´ah na khaswa elimu za dharurah, ataulizwa siku ya Qiyaamah kwa nini hakujifunza na kwa nini hakuuliza. Atapowekwa ndani ya kaburi maswali matatu akaweza kuyajibu huyu ataokoka, na atapoulizwa wapi umeyajua haya? Atasema nilisoma Kitabu cha Allaah na nikajifunza. Ama yule ambaye aliyapa mgongo atapoulizwa ndani ya kaburi lake, atasema ”Aah, aah, sijui! Niliwasikia watu wakisema na mimi nikasema.” Huyu atajaziwa ndani ya kaburi lake moto na atawekwa kwenye shimo miongoni mwa mashimo ya Motoni. Huyu ni kwa kuwa hakusoma na wala hakushikamana na wanachuoni.
Elimu ni kumjua Allaah, Mtume Wake na Dini ya Uislamu kwa dalili. Hii ndio elimu ya Shari´ah inayotakikana kwetu. Kumjua Allaah kwa Majina na Sifa Zake, kujua haki Zake juu yetu ambayo ni ´Ibaadah pasina Shirki. Hili ndio jambo la kwanza kwa mja kulijua. Na vipi utamjua Mola Wako - hilo linakuja huko mbele. Atamjua kwa Aayaat (Ishara) Zake na viumbe Vyake. Aayaat (Ishara) Zake kawniyyah (za utendaji kazi Wake) na Qur-aaniyyah (za Kishari´ah zilizomo ndani ya Qur-aan).
Kumjua Mtume Wake, kwa kuwa yeye ndiye mfikishaji kutoka kwa Allaah. Na yeye ndiye waasitwah mkati na kati baina yetu sisi na Allaah katika kufikisha Risalaah. Lazima ujue ni nani; nasaba yake, mji wake, aliyokuja nayo, alianza vipi Wahyi, alifanyaje Da´wah, tangu alipoanza mpaka Madiynah. Ajue Siyrah yake. Haiwezekani kwa Muislamu akawa hamjui Mtume wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ni Muhammad bin ´Abdillaah, bin ´Abdil-Muttwalib, bin Haashim, bin al-Manaaf mpaka mwisho wa nasabu yake ambayo inaenda mpaka kuishia kwa Ibraahiym (´alayhis-Swalaat was-Salaam). Mtu ajue aliishi vipi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kabla ya utume, na baada ya utume. Vipi Wahyi ulimjia kutoka kwa Allaah na alifanya nini baada ya utume wake. Muislamu haimstahiki akawa hamjui (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Vipi utamfuata mtu na wewe humjui? Hili haliingia akilini.
Na kujua Dini ya Uislamu ambayo ni Dini ya Allaah (Jalla wa ´Alaa) ambayo Kawaamrisha kwayo waja Wake na ambayo Amekuamrisha kuijua. Ni lazima uijue Dini hii kwa dalili na si kwa kufuata kichwa mchunga tu. Kwa dalili kutoka katika Qur-aan na Sunnah. Elimu ni ile ambayo Kasema Allaah, kasema Mtume Wake na Maswahabah.
Ama kauli za wanachuoni ni zenye kusherehesha na kuweka wazi tu Maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) na maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Na kunaweza kuwa katika baadhi yake makosa au kupatia. Ama dalili sio maneno ya wanachuoni, bali ni Aayah za Qur-aan na Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Uislamu ndio Dini ya Mitume wote (´alayhimus-Swalaat was-Salaam). Kila mwenye kufuata Dini ya Mtume miongoni mwa Mitume waliotangulia (katika wakati wa Risaalah ya Mtume yule) basi huyo ni Muislamu. Ni mtu aliyejisalimisha na kunyenyekea kwa Allaah (´Azza wa Jalla). Huu ni Uislamu kwa maana ya jumla, kujisalimisha kwa Allaah kwa kumpwekesha na kumuelekea kwa utiifu na kujitakasa na Shirki. Ama Uislamu kwa maana maalum, ni ambayo Allaah Kamtuma nayo Mtume Wake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa kuwa baada ya kutumwa Mtume akaja na Uislamu, ni kumfuata (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).
Haya ndio mas-alah ya kwanza na dio msingi na ´Aqiydah. Mtu huanza kwa ´Aqiydah katika kufunza na Da´wah.

Suala la pili:  Kuifanyia kazi.


2.    Suala la pili
Yaani kuifanyia kazi elimu. Haitoshi kwa Muislamu kusoma na kujua tu. Bali ni lazima kuifanyia kazi elimu yake. Elimu bila ya ´amali ni hoja dhidi ya mwenye nayo. Ama mwenye kujua bila ya kufanyia kazi elimu yake, huyu kaghadhibikiwa. Kwa kuwa kaijua haki na akaiacha kwa ujuzi. Na mshairi anasema:
“Na msomi kwa elimu yake ambayo hakuifanyia kazi, ataadhibiwa kabla ya muabudu sanamu.”
Hili limesemwa katika Hadiyth ya kwamba mtu wa kwanza atakayeadhibiwa siku ya Qiyaamah ni mwanachuoni ambaye hakuifanyia kazi elimu yake. Huyu ndiye katika watu wa kwanza watakaowekwa Motoni siku ya Qiyaamah. ´Amali ndio matunda ya elimu. Elimu bila ya ´amali ni kama mti usiokuwa na matunda. Kama ambavyo mtu kufanya ´amali pasina elimu ni kujichosha bure tu. Anasema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):
“Akatakayefanya ´amali isiyokuwa humo na amri yetu atarudishiwa mwenyewe.”
Na Allaah (Ta´ala) Kawaita watu hawa kuwa ni wapotofu.
Aina ya kwanza ya watu ni wale wenye elimu na hawakuifanyia kazi wameghadhibikiwa. Na aina ya pili ni wale wenye kufanya ´amali bila ya elimu, wamepotea. Na ndio maana kila tunaposwali tunaomba:
اهْدِنَا الصِّرَاطَ الْمُسْتَقِيمَ
“Tuongoze katika njia iliyonyooka.” (01:06)

Suala la tatu: Kuilingania.

3.    Suala la tatu
Haitoshi mtu kujifunza, akafanya ´amali mwenyewe na wala halinganii katika Dini ya Allaah. Ni lazima afanye hivyo ili awe ameinufaisha nafsi yake mwenyewe kwanza kisha amenufaisha wengine. Kwa kuwa elimu hii ni amaanah. Ni wajibu kuwafikishia wengine, kuwabainishia na kuwalingania watu katika kheri.
 وَإِذْ أَخَذَ اللَّـهُ مِيثَاقَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ لَتُبَيِّنُنَّهُ لِلنَّاسِ وَلَا تَكْتُمُونَهُ
“Na (taja ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) Alipochukua Allaah fungamano la wale ambao wamepewa Kitabu (Allaah Akawaambia): “Bila shaka mtakibainisha kwa watu na wala hamtokificha”.” (03:187)
قُلْ هَـٰذِهِ سَبِيلِي أَدْعُو إِلَى اللَّـهِ ۚ عَلَىٰ بَصِيرَةٍ أَنَا وَمَنِ اتَّبَعَنِيۖ وَسُبْحَانَ اللَّـهِ وَمَا أَنَا مِنَ الْمُشْرِكِينَ
”Sema: “Hii ndio njia yangu nalingania kwa Allaah, juu ya baswiyrah (ujuzi, umaizi)  mimi na anayenifuata. Na Subhaana Allaah (Ametakasika Allaah), nami si miongoni mwa washirikina”.” (12:108)
Hii ndio njia ya Mitume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wafuasi wao: elimu, ´amali na Da´wah katika Dini ya Allaah. Ama yule ambaye atakuwa na elimu na asiitoe, atalazimishwa kuitoa siku ya Qiyaamah kwa Moto kama ilivyokuja katika Hadiyth.

Suala la nne: Kusubiri (kuvumilia) maudhi yatakayopatikana ndani yake.

4.    Suala la nne
Ni jambo linalojulikana ya kwamba mwenye kulingania watu na kuwaamrisha mema na kuwakataza maovu atasibiwa na maudhi kutoka kwa watu. Kwa kuwa watu wengi hawataki kheri, bali wanataka mambo ya shahawa na ya haramu na matamanio. Akijitokeza mtu mwenye kuwalingania kwa Allaah na kuwarudisha kwa shahawa zao, lazima asibiwa na yakusibiwa kwa kauli na vitendo. Hivyo ni wajibu kuwa na subira juu ya maudhi na aendelee na Da´wah katika njia ya Allaah. Na viigizo vyake ni Mitume (´alayhimus-Swalaat was-Salaam), na wa mwisho wao (Mitume) alikuwa ni Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Alipatwa na nini kutoka kwa watu kwa kauli na vitendo, aliambiwa ni mchawi, muongo, mwendawazimu wakasena na kusema. Mambo ambayo Ameyasema Allaah (Jalla  wa ´Alaa) katika Qur-aan. Akapigwa mawe, kuwekewa utumbotumbo alipokuwa amesujudu kwenye Ka´abah, wakamtishia kumuua. Yote haya yalimfika katika Da´wah ya Allaah, lakini alikuwa ni mwenye kusubiri ilihali naye ndio mbora wa viumbe.
Hivyo ni lazima kwa yule mwenye kusimama na Da´wah hii avumilie kwa maudhi kwa kiasi cha Imani yake. Asubiri maadamu yuko katika haki. Yeye yuko katika Njia ya Allaah (´Azza wa Jalla), na maudhi yanayomfika yeye anapata thawabu.

Na dalili ni kauli Yake Ta´ala:
وَالْعَصْرِ إِنَّ الْإِنسَانَ لَفِي خُسْرٍ إِلَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَتَوَاصَوْا بِالْحَقِّ وَتَوَاصَوْا بِالصَّبْرِ

”Naapa kwa Al-‘Aswr (zama). Hakika bin-Aadam bila shaka yumo katika khasara. Isipokuwa wale walioamini na wakatenda mema na wakausiana kwa ya haki na wakausiana kwa subira.” (103:1-03)


Mambo haya manne asemayo Shaykh yana dalili? Dalili ni:
 Jambo la kwanza ni elimu kwa kuwa Imani haiwi ila kwa elimu, nayo ndio kumjua Allaah (Ta´ala), Mtume Wake na Dini ya Uislamu. Kuifanyia kazi. Kuilingania. Kuwa na subira.
Allaah Kaapa kwa (zama za) ´Aswr, Allaah Anaapa kwa Atakacho katika viumbe Vyake. Na Haapi ila kwa kitu kilicho na umuhimu na ni Aayah (Ishara) katika Aayaat (Ishara) za Allaah. Ama viumbe hawaapi isipokuwa kwa Allaah. Haijuzu kwetu kuapa kwa asiyekuwa Allaah. Anasema Mtume:
“Atakayeapa kwa asiyekuwa Allaah, amekufuru au ameshiriki.”
“Mwenye kutaka kuapa, aape kwa Allaah au anyamaze.”
Binaadamu wote wako katika khasara na kuangamia isipokuwa ambao wamesifika kwa sifa hizi nne; elimu, ´amali, Da´wah na subira.


Imaam Ash-Shaafi'iyy  alisema:  “Lau kama Allaah Asingeliteremsha hoja kwa viumbe Vyake isipokuwa Surah hii, basi ingeliwatosheleza”

Shaafi´iy ni unasibisho wa babu yake. Na ni katika Ahl-ul-Bayt Quraysh, alizaliwa katika mwaka wa 150 H. Anasema:
“Lau Allaah Asingeliteremsha hoja kwa viumve Vyake ila Suurah hii basi ingeliwatosheleza.”
Kwa kuwa Allaah Kabainisha sababu za mafanikio. Sababu za mafanikio ni mtu asifike kwa sifa hizi nne.  Allaah Angelisema mimi nimewabainishia sababu za kuokoka katika Suurah hii fupi. Ama Qur-aan yote ni ufafanuzi wa mambo haya manne. Lazima Suurah hii imebainisha sababu za kuokoka kwa njia ya jumla na hoja imewasimamia viumbe. Na nususi zingine katika Qur-aan ni zenye kufafanua na kubainisha mas-alah haya manne. Si kwamba Suurah hii ingeliwatosheleza lau kama wasingelitumiwa zingine, hapana. Bali ingelikuwa ni hoja tosha kwao. Hakuna yeyote angesema kuwa mimi sikujua sababu za kuokoka ilihali naye anasoma Suurah hii.


Na Al-Bukhaariy  amesema katika Baabul-´Ilm qablal-qawli wal-´amal: “Mlango wa elimu kabla ya kauli na ´amali”.
Na dalili ni kauli Yake Ta´ala:
فَاعْلَمْ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا اللَّـهُ وَاسْتَغْفِرْ لِذَنبِكَ
“Basi elewa kwamba laa ilaaha illa-Allaah (Hapana Anayastahiki kuabudiwa kwa haki  ila Allaah), na omba maghfirah kwa dhambi zako.” (47:19)
Akaanza kwa elimu kwanza kabla ya kauli na ´amali (kitendo).


Kwa kuwa kauli na ´amali havinufaishi isipokuwa ikiwa vimejengeka juu ya elimu. Ama kauli na ´amali vilivyojengeka juu ya ujinga havimnufaishi mwenye navyo bali inakuwa ni upotofu kwake siku ya Qiyaamah. Lazima mtu atangulize kwanza elimu kisha afuatishe kwa ´amali na kauli. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):
فَاعْلَمْ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا اللَّـهُ وَاسْتَغْفِرْ لِذَنبِكَ
“Basi elewa kwamba laa ilaaha illa-Allaah (Hapana Anayastahiki kuabudiwa kwa haki  ila Allaah), na omba maghfirah kwa dhambi zako.” (47:19)
“Basi elewa...” hii ni elimu. “Na omba maghfirah kwa dhambi zako” hii ni ´amali. Allaah Kaanza elimu kabla ya kauli na ´amali. Lazima kwanza mtu atangulize elimu kisha afanyie kazi alivyojifunza.


Tambua Allaah Akurehemu, kwamba ni wajibu kwa kila Muislamu mwanamme na Muislamu mwanamke, kujifunza mas-alah haya matatu (yafuatayo) na kuyafanyia kazi:


Ni wajibu kwetu, hii inaonesha ya kwamba jambo hili si kwamba limependekezwa bali ni lazima kutoka kwa Allaah. Na si kwamba ni Shaykh ndio katulazimisha, bali Allaah (´Azza wa Jalla) katika Aliyoteremsha katika Kitabu na Sunnah. Kujifunza maana yake ni kuchukua elimu kutoka kwa wanachuoni, kuhifadhi na kufahamu. Huku ndio kusoma sahihi. Kujifunza mambo matatu ndio maana hii tulioitaja. Kwa kuwa mas-alah haya matatu ndio asli ya Dini, na mengine yanajengeka juu yake.


(Suala) La kwanza:  Kwamba Allaah  Ametuumba, na Anaturuzuku, na Hakutuacha bure bali Ametutumia Mitume. Basi atakayemtii ataingia Peponi, na atakayemuasi ataingia motoni. Na dalili ni kauli Yake Ta´ala:
إِنَّا أَرْسَلْنَا إِلَيْكُمْ رَسُولًا شَاهِدًا عَلَيْكُمْ كَمَا أَرْسَلْنَا إِلَىٰ فِرْعَوْنَ رَسُولًا فَعَصَىٰ فِرْعَوْنُ الرَّسُولَ فَأَخَذْنَاهُ أَخْذًا وَبِيلًا
 
”Hakika Sisi Tumekutumieni Mtume (awe) shahidi juu yenu, kama Tulivyotuma kwa Fir’awn Mtume.  (Lakini) Fir’awn alimuasi (huyo) Mtume, Tukamkamata mkamato wa kuangamiza.” (73:15-16)


1.    Suala la kwanza
هَلْ أَتَىٰ عَلَى الْإِنسَانِ حِينٌ مِّنَ الدَّهْرِ لَمْ يَكُن شَيْئًا مَّذْكُورًا
“Je, haukumpitia bin-Aadam wakati katika dahari, hakuwa kitu kinachotajwa?” (76:01)
Kakuumba na wala hukuwa kitu. Mtu kabla ya kuumbwa alikuwa si kitu. Na Akaturuzuku, kwa kuwa sisi tunahitajia riziki mbali mbali, sawa za kutoka ardhini na mbinguni. Ili tuweze kuishi na za tusaidie katika kumuabudu Allaah (´Azza wa Jalla). Allaah Katuumba na Kuturuzuku kwa hekima.
أَفَحَسِبْتُمْ أَنَّمَا خَلَقْنَاكُمْ عَبَثًا وَأَنَّكُمْ إِلَيْنَا لَا تُرْجَعُونَ
 
“Je, mlidhania kwamba Sisi Tulikuumbeni bila kusudio (kwa burudani na mchezo tu?); na kwamba nyinyi Kwetu hamtorejeshwa?” (23:115)

وَمَا خَلَقْنَا السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا لَاعِبِينَ
”Na Hatukuumba mbingu na ardhi na yaliyoko baina yake kwa mchezo.” (44:38)
Allaah Alipotuumba na Akaturuzuku mambo haya ni kwa hekima kubwa, nayo ni ili tumuabudu (Subhaanahu wa Ta´ala). Na Hakutuumba kama minyama ambayo iko kwa maslahi ya waja kisha unakufa na kutoweka, na haukukalifishwa, wala kuamrishwa na kukatazwa. Bali Katuumba ili tumuabudu:
وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ
 
”Na Sikuumba majini na watu wa isipokuwa waniabudu.” (51:56)
Hakutuumba kwa ajili ya maisha haya ya duniani tu tueshi humo, tule, tunywe, tuvae n.k. na hakuna baada yake kitu, hapana. Maisha haya ni sehemu ya kupanda kwa ajili ya Aakhirah, kwa matendo mema. Kisha tutakufa, kisha tutafufuliwa, kisha tutahesabiwa na kulipwa kwa ´amali zetu. Haya ndio makusudio ya binaadamu na majini.
Dalili ya hilo ni nyingi zinazotolea dalili kufa, kufufuliwa, kuhesabiwa, kufanyiwa hesabu na kadhalika. Na akili inatolea dalili hilo pia, ya kwamba hailingani kwa Hekima ya Allaah (Ta´ala) Kuumba Uumbaji huu wa ajabu na Kumuwekea ulimwengu huu binaadamu kisha Akawaacha wakafariki na kwenda bila ya natija. Hili ni jambo lisilowezekana. Lazima kuonekana natija ya ´amali hizi katika Nyumba ya Aakhirah. Na kwa ajili hii, kunaweza kupatikana katika watu ambao wanatumia maisha yao yote katika kumuabudu Allaah na kumtii, na mtu huyo yuko katika ufukara, haja, na pengine akawa ni mwenye kudhulumiwa, kughadhibikiwa, kuonewa na wala hapati kitu kutokana na ´amali anazofanya katika dunia hii. Akafariki naye hakupata chochote katika malipo ya matendo yake katika dunia hii.
Na upande mwingine ikawa kinyume chake, kuko katika watu ambao ni makafiri Mulhiduun waovu, wanafanya watakacho katika maisha haya, wanastarehe, wanaipa nafsi kila watakacho, wanafanya Aliyoharamisha Allaah, anawadhulumu watu, kuwaonea, kula mali yao, anaua bila ya haki, anaiba na kufanya ujabari kisha anafariki bila ya kupatwa na kitu katika adhabu. Yaani anakufa katika hali ambayo hakupatwa na kitu katika adhabu, je kweli inalingana kwa Uadilifu na Hekima ya Allaah kumuacha mtu mwema huyu bila ya malipo na Akamuacha kafiri huyu bila ya kumlipa? Hapana. Hili halilingani na Uadilifu na Hekima Yake (Subhaanahu wa Ta´ala). Na kwa ajili hiyo ndio maana kafanya Nyumba nyingine ikawa ni ya malipo. Mwema alipwe kwa wema wake na muovu alipwe kwa maovu yake. Kudhihiri matunda ya ´amali. Dunia ni nyumba ya ´amali ima kheri au shari, ama Aakhirah ni Nyumba ya malipo ima Pepo au Moto. Hivyo Hakutuacha bure kama wanavyodhani Malaahidah, ad-Dahriyyuun. Wakasema:
مَا هِيَ إِلَّا حَيَاتُنَا الدُّنْيَا نَمُوتُ وَنَحْيَا وَمَا يُهْلِكُنَا إِلَّا الدَّهْرُ
“Haya sisi chochote isipokuwa ni maisha yetu dunia, tunakufa na tunahuika, na hakuna cha kutuangamiza isipokuwa dahari.” (45:24)

Hivi ndivyo walivyosema Malaahidah ambao hawaamini kufufuliwa. Allaah Akawakatalia:
أَفَنَجْعَلُ الْمُسْلِمِينَ كَالْمُجْرِمِينَ مَا لَكُمْ كَيْفَ تَحْكُمُونَ
“Je, Tuwajaalie Waislamu kama wakhalifu? Mna nini! Vipi mnahukumu?.” (38:35-36)
أَمْ حَسِبَ الَّذِينَ اجْتَرَحُوا السَّيِّئَاتِ أَن نَّجْعَلَهُمْ كَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ سَوَاءً مَّحْيَاهُمْ وَمَمَاتُهُمْ ۚ سَاءَ مَا يَحْكُمُونَ
”Je, wanadhania wale waliochuma maovu kwamba Tuwafanye (wawe) sawa na wale walioamini na wakatenda mema (na pia) sawasawa uhai wao na kufa kwao? Uovu ulioje wanaouhukumu.” (45:21)

أَمْ نَجْعَلُ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ كَالْمُفْسِدِينَ فِي الْأَرْضِ أَمْ نَجْعَلُ الْمُتَّقِينَ كَالْفُجَّارِ
”Je, Tuwajaalie wale walioamini (Tawhiyd ya Allaah) na wakatenda mema (walingane sawasawa) kama mafisadi (wanaomshirikisha Allaah na kutenda maovu) katika ardhi? Au Tuwajaalie wenye taqwa kama (sawa) na waovu?” (38:28)
Hili haliwezekani na halitokuwepo kamwe. Ni dalili ioneshayo ya kwamba kuna kufufuliwa baada ya kufa. Na kwamba kuna kulipwa baada ya kufa kwa ´amali zetu katika dunia hii. Allaah Katuumba ili kumuabudu na Katuamrisha kumpwekesha na kumtii. Kisha Hakutuacha kumuabudu kwa hatamanio yetu, mtazamo wetu au kwa kumfuata kichwa mchunga fulani katika watu, kufanya ´Ibaadah kwa ada zetu au ada za watu. Katutumia Mitume wanaotubainishia vipi kumuabudu Allaah, kwa kuwa ´Ibaadah ni Tawqiyfiyyah. Haijuzu kumuabudu Allaah kwa kitu ambacho Hakikuwekwa.
Kazi ya Mitume (´alayhis-Swalaat was-Salaam) ni kuwabainishia watu vipi kumuabudu na kuwakataza Shirki, kufuru na maasi. Haya ndio mambo ya muhimu kwa Mitume (´alayhimus-Swalaat was-Salaam). Bid´ah na ukhurafi vinarudishwa. ´Ibaadah haikubaliwi isipokuwa kwa Shari´ah aliyokuja nayo Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kafikisha ubainisho wa wazi, kafikisha amaanah na Risaalah kwa Ummah na kabainisha na kuweka wazi na kutuacha katika njia iliyokuwa nyeupe kabisa usiku wake ni sawa na mchana wake. Hatopotea isipokuwa mpotevu.
Katutumia Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Atakayemtii kwa aliyoamrisha ataingia Peponi. Na atakayemuasi kwa aliyokataza ataingia Motoni.
مَّن يُطِعِ الرَّسُولَ فَقَدْ أَطَاعَ اللَّـهَ
“Atakayemtii Mtume basi kwa yakini amemtii Allaah.” (04:80)
وَإِن تُطِيعُوهُ تَهْتَدُوا
“Na mkimtii Mtume wa Allaah mtaongoka.” (24:54)
وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ
“Na mtiini Mtume ili mpate kurehemewa.” (24:56)
Anasema Mtume:
“Kila mtu ataingia Peponi ila mwenye kukataa. Akaulizwa: “Ni nani atakayekataa?” Akasema: “Atakayenitii ataingia Peponi, na atakayeniasi atakuwa amekataa”.”
"Hatosikia yeyote kuhusu mimi si myahudi wala mnaswara kisha asiniamini isipokuwa ataingia Motoni."
Hii ndio tofauti baina ya Muislamu na kafiri.
إِنَّا أَرْسَلْنَا إِلَيْكُمْ رَسُولًا شَاهِدًا عَلَيْكُمْ كَمَا أَرْسَلْنَا إِلَىٰ فِرْعَوْنَ رَسُولًا
 
”Hakika Sisi Tumekutumieni Mtume (awe) shahidi juu yenu, kama Tulivyotuma kwa Fir’awn Mtume.” (73:15)
Mtu hatokuwa na hoja siku ya Qiyaamah kwamba sikujiwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), hapana. Na Ummah huu unatolea ushahidi siku ya Qiyaamah ya kwamba Mitume (´alayhimus-Swalaat was-Salaam) walifikisha ujumbe wa Allaah, kutokana na watakayokutana katika Kitabu cha Allaah. Yote haya waliyajua kupitia katika Kitabu cha Allaah.
لَّا يَأْتِيهِ الْبَاطِلُ مِن بَيْنِ يَدَيْهِ وَلَا مِنْ خَلْفِهِ ۖ تَنزِيلٌ مِّنْ حَكِيمٍ حَمِيدٍ

”Haitokifikia ubatili mbele yake, na wala nyuma yake; ni Uteremsho kutoka kwa Hakiymin-Hamiyd (Mwenye hikmah wa yote daima - Mwenye kustahiki kuhimidiwa).” (41:42)
Hakuna mtu ana hoja siku ya Qiyaamah kusema hakufikiwa na kitu, hakujiwa na muonyaji n.k. Hata makafiri watakubali.
قَالُوا بَلَىٰ قَدْ جَاءَنَا نَذِيرٌ فَكَذَّبْنَا وَقُلْنَا مَا نَزَّلَ اللَّـهُ مِن شَيْءٍ إِنْ أَنتُمْ إِلَّا فِي ضَلَالٍ كَبِيرٍ وَقَالُوا لَوْ كُنَّا نَسْمَعُ أَوْ نَعْقِلُ مَا كُنَّا فِي أَصْحَابِ السَّعِيرِ

”Watasema: Ndio! Kwa yakini alitujia mwonyaji, tukakadhibisha, na tukasema (kuwaambiwa waonyaji): “Allaah Hakuteremsha kitu chochote; nyinyi si chochote isipokuwa mumo katika upotofu mkubwa. Na watasema: “Lau tungelikuwa tunasikilia (na kusikiliza) au tunatia akilini, tusingelikuwa miongoni mwa wakaazi wa Moto uwakao (kwa nguvu)”.” (67:09-10)

Wanawakadhibisha na kuwaambia Mitume (´alayhimus-Salaam) kuwa wako katika upotofu mkubwa. Allaah Atukinge. Watu wa Fir´awn walipewa adhabu tatu kubwa kwa kumuasi Muusa (´alayhis-Salaam); kwanza waliteswa mateso makubwa, kisha ndani ya kaburi wanaadhibiwa kwa kuoneshwa Moto asubuhi na usiku, na siku ya Qiyaamah ikifika watapewa adhabu kali.
Hali kadhalika kwa yule atakayemuasi Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) adhabu yake itakuwa kama ya Fir´awn na huenda ikawa kubwa zaidi, kwa kuwa Mtume Muhammad ndio Mtume bora (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Atakayemuasi adhabu yake itakuwa kali. Hali kadhalika maadui wa Mitume hii ndio adhabu na hii ndio njia yao. Katika Aayah hii kuna kukumbushwa na Allaah kututumia Mitume (´alayhimus-Salaam).

La pili: Kwamba Allaah Haridhii kushirikishwa na  yeyote katika waja Wake, ikiwa ni Malaika aliye karibu (Naye), wala Nabii aliyetumwa.


2.    Suala la pili
Suala hili linahusiana na suala la kwanza, kwa kuwa linahusiana na wajibu wa kumuabudu Allaah na wajibu wa kumfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Na hii ndio maana ya Shahaadah. ´Ibaadah ikichanganyika na Shirki itakuwa haina faida na wala hainufaishi, lazima iwe kwa ajili ya Allaah Pekee. Atakayemuabudu Allaah na akamuabudu mwengine badala yake (´Ibaadah yake) ni batili, kuwa kwake ni kama kutokuwepo kwake. ´Ibaadah haitofaa ila kwa Ikhaalasw  na Tawhiyd. Ikichanganyika na Shirki inabatilika. Kama Alivyosema Allaah:
وَلَقَدْ أُوحِيَ إِلَيْكَ وَإِلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكَ لَئِنْ أَشْرَكْتَ لَيَحْبَطَنَّ عَمَلُكَ وَلَتَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ بَلِ اللَّـهَ فَاعْبُدْ وَكُن مِّنَ الشَّاكِرِينَ
”Kwa yakini umeletewa Wahy na kwa wale walio kabla yako (kwamba): “Ukifanya shirki (kumshirikisha Allaah) bila shaka zitaporomoka ‘amali zako (zote), na bila shaka utakuwa miongoni mwa waliokhasirika. Bali Allaah (Pekee) mwabudu, na uwe miongoni mwa wenye kushukuru.” (39:65-66)
وَلَوْ أَشْرَكُوا لَحَبِطَ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ
“Na lau wangemshirikisha bila shaka ingewaharibikia yale waliyokuwa wakitenda.” (06:88)
´Ibaadah haiwi ´Ibaadah ila pamoja na Tawhiyd, kama jinsi Swalah haiitwi Swalah ila pamoja na Twahara. Shirki ikichanganyika katika ´Ibaadah inaiharibu, kama jinsi Swalah ambayo imechanganyika na moja katika mambo ambayo yanavunja Wudhuu inaharibika.
Kumuamini Allaah hakutoshi isipokuwa pamoja na kukufuru at-Twaaghuut.  Washirikina wanamwamini Allaah ila wanamshirikisha kwa kutokufuru Twaaghuut. Allaah Haridhii hilo.
Hawa watu ambao wanaswali, wanashahidilia laa ilaaha illa Allaah wa Anna Muhammad Rasuulu Allaah, wanafunga, wanahiji, lakini wanaomba makaburi na wanamuomba Hasan, Husayn, Badawiy, fulani na fulani, wanawachinjia maiti, watu hawa ´Ibaadah zao ni batili kwa kuwa wanamshirikisha Allaah (´Azza wa Jalla). Wanaiharibu ´Ibaadah yao kwa Shirki. ´Amali zao ni batili mpaka wampwekeshe Allaah (´Azza wa Jalla) na wamtakasie ´Ibaadah na waache ´Ibaadah badala yake. Ni wajibu kutanabahi kwa hili. Allaah Haridhii kushirikishwa katika ´Ibaadah yake na yeyote; sawa iwe ni sanamu, mti, jiwe, kaburi, jini, mtu, aliyehai, maiti n.k. Kwa kuwa kuko wanaosema mimi namchukua (na kumuabudu) mtu aliye mwema na mchaji Allaah na sichukui masanamu, nawachukua kama waombezi wangu kwa kuwa ni watu wema na ni mawalii wa Allaah (Ta´ala). Si Malaika aliyekaribu wala Nabii aliyetumwa. Allaah Haridhii hili. Hii ni Radd kwa wale wanaodai ya kwamba wao wanawachukua watu wema na mawalii kuwa ni waombezi wao kwa Allaah na kwamba wanawakurubisha kwa Allaah. Ni kama walivvosema Ahl-ul-Jaahiliyyah.


Na dalili ni kauli Yake Ta´ala:
وَأَنَّ الْمَسَاجِدَ لِلَّـهِ فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا
 
”Na kwamba Misikiti ni (kwa ajili) ya Allaah, basi msiombe (msimuabudu) yeyote pamoja na Allaah.” (72:18)

Msikiti ni Nyumba ya Allaah. Haijuzu kuomba humo badala ya Allaah. Na Misikiti haijuzu kuijenga kwenye makaburi. Kwa kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kamlaani mwenye kufanya hivyo na kusema kuwa hichi ni kitendo cha mayahudi na manaswara katika uhai wake wa mwisho alipokuwa katika kukata roho (´alayhis-Salaam).
“ahadaa (yeyote)”, hapa inamjumuisha kila yule anayeombwa badala ya Allaah. Dalili hii inatolea dalili ya kwamba ´Ibaadah haifai isipokuwa pamoja na Tawhiyd. Na ikiingiwa ndani yake na Shirki haimfai kitu mwenye nayo na badala yake ni maangamivu.
Na Aayah hii inatolea  dalili ya kwamba Misikiti ni wajibu ijengwe kwa nia nzuri ya Khaaliswan, makusudio isiwe Riyaa, Sum´aa, Athaar Islaamiyyah kama inavyosemwa. Makusudio Msikiti uwe umejengwa kwa ajili ya Allaah na kwa makusudio mazuri, isiwe makusudio ya haramu. Mali iwe ya halali na iwe kwa nia nzuri. Kwa kuwa kujenga Misikiti ni ´Ibaadah.


La Tatu: Kwamba Atakayemtii Mtume, na Akampwekesha Allaah, haijuzu kwake kufanya urafiki na ushirikiano na yule anayempinga Allaah na Mtume Wake hata ikiwa ni jamaa wa karibu.


3.    Suala la tatu
Haya ni masuala ya Tawhiyd al-Walaa´ wal-Baraa´. Katika haki za Tawhiyd ni al-Walaa´ wal-Baraa´. Kuwapenda mawalii wa Allaah na kuwachukia maadui wa Allaah. al-Muwaalaat na al-Walaa´ ina maana moja, al-Walaa´ kunakusudiwa kuwapenda moyoni, kuwanusuru na kuwasaidia. Muislamu awapende mawalii wa Allaah na awanusuru. Na mambo yao Waislamu na matatizo yao Waislamu yawe baina yao wao kwa wao, na yasiwe baina ya Muislamu na kafiri. Haijuzu kwa yule mwenye kumpwekesha Allaah na kumtii Mtume kumpenda anayempinga Allaah. Kupingana ni Allaah kuwa upande huu na mtu huyo upande mwingine. Huku ndio kumpinga Allaah. Hata ikiwa ni jamaa wa karibu kabisa kinasabu, ikiwa ndugu yako ni adui wa Allaah na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Wake, ni wajibu kwako kumkata na kumsusa. Na atakayekuwa ni walii wa Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni wajibu kwako kumpenda na kumsaidia hata akiwa ni mtu aliye mbali na wewe kinasabu, sawa awe mweusi, mweupe, mwarabu, asiyekuwa mwarabu, awe katika mji wako, asiwe katika mji wako n.k. Waislamu ni ndugu wao kwa wao.


لَّا تَجِدُ قَوْمًا يُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ يُوَادُّونَ مَنْ حَادَّ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَلَوْ كَانُوا آبَاءَهُمْ أَوْ أَبْنَاءَهُمْ أَوْ إِخْوَانَهُمْ أَوْ عَشِيرَتَهُمْ ۚ أُولَـٰئِكَ كَتَبَ فِي قُلُوبِهِمُ الْإِيمَانَ وَأَيَّدَهُم بِرُوحٍ مِّنْهُ ۖوَيُدْخِلُهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا ۚ رَضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ ۚ أُولَـٰئِكَ حِزْبُ اللَّـهِ ۚ أَلَا إِنَّ حِزْبَ اللَّـهِ هُمُ الْمُفْلِحُونَ
 
”Hutokuta (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) watu wanaomuamini Allaah na Siku ya Mwisho (kuwa) wanawapenda wale wanaopinzana na Allaah na Mtume Wake, japo wakiwa (ni) baba zao, au watoto wao, au ndugu zao, au jamaa zao. Hao (Allaah) Amewaandikia katika nyoyo zao iymaan, na Akawatia nguvu kwa Roho kutoka Kwake, na Atawaingiza (kwenye) mabustani yapitayo chini yake mito wadumu milele humo. Allaah Ameridhika nao, nao wameridhika Naye. Hao ndio kundi la Allaah. Tanabahi! Hakika kundi la Allaah ndio lenye kufaulu.” (58:22)

Hapa ananadiwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ni jambo lisilowezekana kwa muumini kumpenda yule anayempinga Allaah na Mtume Wake. Akimpenda atakuwa sio muumini hata kama anadai hilo. Anasema Ibnul-Qayyim (Rahimahu Allaah):
“Unawapenda maadui wa Kipenzi (Mtume) na unadai kumpenda, yako wapi madai yako?”
Hili ni jambo haliwezekani kamwe kwa yule anayewapenda makafiri kusema kuwa anampenda Allaah na Mtume Wake. Kamwe.
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَتَّخِذُوا عَدُوِّي وَعَدُوَّكُمْ أَوْلِيَاءَ تُلْقُونَ إِلَيْهِم بِالْمَوَدَّةِ
“Enyi mlioamini! Msimchukue adui Wangu na adui wenu (kuwa) marafiki wandani mkiwapelekea (siri za mikakati) kwa mapenzi.” (60:01)
قَدْ كَانَتْ لَكُمْ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ فِي إِبْرَاهِيمَ وَالَّذِينَ مَعَهُ إِذْ قَالُوا لِقَوْمِهِمْ إِنَّا بُرَآءُ مِنكُمْ وَمِمَّا تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ كَفَرْنَا بِكُمْ وَبَدَا بَيْنَنَا وَبَيْنَكُمُ الْعَدَاوَةُ وَالْبَغْضَاءُ أَبَدًا حَتَّىٰ تُؤْمِنُوا بِاللَّـهِ وَحْدَهُ
“Kwa yakini mna kigezo kizuri kwa Ibraahiym na wale walio pamoja naye, walipowaambia watu wao: “Hakika sisi tumejitenga nanyi na yale (yote) mnayoyaabudu badala ya Allaah, tunakukanusheni, na umedhihirika baina yetu na baina yenu uadui na bughudha ya daima mpaka mumuamini Allaah Pekee”.” (60:04)
وَمَا كَانَ اسْتِغْفَارُ إِبْرَاهِيمَ لِأَبِيهِ إِلَّا عَن مَّوْعِدَةٍ وَعَدَهَا إِيَّاهُ فَلَمَّا تَبَيَّنَ لَهُ أَنَّهُ عَدُوٌّ لِّلَّـهِ تَبَرَّأَ مِنْهُ ۚ إِنَّ إِبْرَاهِيمَ لَأَوَّاهٌ حَلِيمٌ
”Na haikuwa Ibraahiym kumuombea maghfirah baba yake isipokuwa kwa sababu ya miadi aliyofanya naye. Lakini ilipombainikia kwamba yeye (huyo baba yake) ni adui wa Allaah, alijiepusha naye. Hakika Ibraahiym niawwaah (mwenye huruma mno) na mvumilivu.” (09:114)
Hii ndio Mila (Dini) ya Ibraahiym. Alijiweka mbali na baba yake ambaye ni jamaa aliye karibu zaidi kwake. Ilipombainikia kwake ya kwamba ni adui wa Allaah. Ni dalili ya kwamba mapenzi kuwapenda makafiri yanapingana na kumuamini Allaah na siku ya Mwisho.
Lakini ikiwa kuwapenda kwao kuna kuwasaidia madhehebu yao pia na kufuru yao, hili linamtoa mtu katika Muislamu. Ama ikiwa mtu hawasaidii kwa kufuru yao na anaamini wamo katika upotofu lakini akawa anawapenda pamoja na kuchukia yale waliyomo, huyu anachukuliwa kuwa ana Imani pungufu na Ufaasiq. Muradi ya “wanaopingana” hapa ni kufuru. Kaanza na wale watu walio karibu. “jamaa zao” ni kabila. Maadamu ni maadui wa Allaah Ajiweke nao mbali.
Aayah hii imeteremka kwa Abu ´Ubayd bin Jarraah (Radhiya Allaahu ´anhu) alipomuua baba yake katika vita vya Badr, kwa kuwa baba yake alikuwa katika kufuru na alikuwa anataka kumuua mtoto wake Abu ´Ubayd. Abu ´Ubayd akawa amemuua baba yake kwa kuwa ni adui wa Allaah. Tendo la yeye kuwa baba yake halikumzuia kumuua. Watu sampuli hii ndio kundi la Allaah, ama makafiri ni kundi na wasaidizi wa Shaytwaan.
Lakini hili haina maana sisi [Waislamu] tuwakate makafiri hata katika mambo kama ya biashara na manufaa ya kidunia. Jambo la kwanza pamoja na kuwachukia na kuwabughudhi ni wajibu kwetu kuwalingania katika Dini ya Allaah. Hatuwaachi na kusema ni maadui wa Allaah. Hapana. Ni lazima tuwalinganie huenda Allaah Akawaongoza. Ikiwa hawatokubali ni wajibu kwetu kupigana nao vita na Jihaad, ima wainge katika Uislamu ima watoe Jizyah ikiwa ni mayahudi, manaswara ilihali ni wenye kunyenyekea hukumu ya Kiislamu. Hawaachwi kwa waliyomo. Mbali na watu hawa (Ahl-ul-Kitaab) wengine ni ima waingie katika Uislamu au wauawe.
Na hakuna neno kuelekea amani kwa makafiri kukiwa na haja ya kufanya hivyo, ikiwa Muislamu hawezi kuwapiga vita na kunakhofiwa kwa Waislamu kupatwa na shari yao, hakuna neno kufanya hivyo mpaka pale Waislamu watapokuwa na uwezo wa kuwapiga vita. Au ikiwa wao wataelekea kwa amani.
وَإِن جَنَحُوا لِلسَّلْمِ فَاجْنَحْ لَهَا وَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ
“Na kama (maadui) wakielemea kwenye amani (usalama), basi (nawe pia) elemea; na tawakali kwa Allaah.” (08:61)
Wataelekewa kwa amani lakini hili haliwi daima, bali inakuwa kwa muda maalum mpaka hapo atapopatikana Imaam wa Waislamu.
Jambo la tatu hakuna neno kulipiza wema ikiwa mmoja wao (katika makafiri) atawatendea Ihsaan Waislamu. Hakuna neno na wao kulipizwa wema. Anasema Allaah:
لَّا يَنْهَاكُمُ اللَّـهُ عَنِ الَّذِينَ لَمْ يُقَاتِلُوكُمْ فِي الدِّينِ وَلَمْ يُخْرِجُوكُم مِّن دِيَارِكُمْ أَن تَبَرُّوهُمْ وَتُقْسِطُوا إِلَيْهِمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُقْسِطِينَ
 
”Allaah Hakukatazeni kuwafanyia wema na uadilifu wale wasiokupigeni vita katika Dini, na wala hawakukutoeni kutoka majumbani mwenu. Hakika Allaah Anapenda wafanyao uadilifu.” (60:08)
Jambo la nne, ni wajibu kwa mtoto ambaye ana baba kafiri kumtendea wema baba yake. Lakini asimtii katika kufuru.
وَوَصَّيْنَا الْإِنسَانَ بِوَالِدَيْهِ حَمَلَتْهُ أُمُّهُ وَهْنًا عَلَىٰ وَهْنٍ وَفِصَالُهُ فِي عَامَيْنِ أَنِ اشْكُرْ لِي وَلِوَالِدَيْكَ إِلَيَّ الْمَصِيرُ وَإِن جَاهَدَاكَ عَلَىٰ أَن تُشْرِكَ بِي مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ فَلَا تُطِعْهُمَا ۖ وَصَاحِبْهُمَا فِي الدُّنْيَا مَعْرُوفًا ۖ وَاتَّبِعْ سَبِيلَ مَنْ أَنَابَ إِلَيَّ
 
”Na Tumemuusia bin-Aadam (kuwafanyia wema) wazazi wake wawili. Mama yake ameibeba mimba yake (akimzidishia) udhaifu juu ya udhaifu, na (kumnyonyesha na) kuacha kwake ziwa katika miaka mwili; ya kwamba, Unishukuru Mimi, na wazazi wako; Kwangu ndio marejeo ya mwisho. Lakini (wazazi wako) wakikufanyia juhudi kwamba unishirikishe na yale usiyokuwa na elimu nayo, basi usiwatii. (Lakini) Suhubiana nao kwa wema duniani, na fuata njia ya anayerudi (kutubia) Kwangu.” (31:14-15)
Baba ana haki zake hata kama ni kafiri. Lakini usimpende. Mtendee tu haki zake kwa kumfanyia wema kama baba huku ukimchukia.
Jambo la tano, mlango wa kushirikiana nao katika biashara na kuchukua mambo ya manufaa kutoka kwao kwa thamani, hakuna neno kubadilishana mambo ya manufaa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akitaamiliana na makafiri na mayahudi. Huku sio kuwapenda bali ni kubadilishana mambo ya manufaa. Ni wajibu kujua mambo haya na kujua ya kwamba hayaingii katika kuwapenda na hayakukatazwa.
Hali kadhalika kuchukua deni kwao, Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alichukua deni kwa myahudi. Na alikufa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ilihali ana deni kwa myahudi. Hakuna neno kwa hili kwa kuwa haya ni mambo ya kidunia na mambo ya manufaa, na wala si dalili kwamba ni kuwapenda au kujenga nao urafiki. Kwa kuwa baadhi ya watu wana ufahamu wao wa kimakosa pindi wanaposikia baadhi ya Aayah zinazozungumzia kuwafanya makafiri maadui na kuwachukia wanaweza kufahamu ya kwamba haifai kuamiliana nao na kuwakata kabisa, hapana. Hili lina masharti na Ahkaam zake.


Tambua, Allaah Akuongoze katika utiifu Wake, kwamba  al-Hanifiyyah (kuelemea Dini ya haki na kujiepusha na dini potofu)  ni Dini ya Ibraahiym. Umwabudu Allaah Pekee ukimtakasia Dini Yake, na kwa hilo Allaah Amewaamrisha watu wote, na Amewaumba kwa sababu hiyo. Kama Anavyosema Ta´ala:
وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ
 
”Na Sikuumba majini na watu wa isipokuwa waniabudu.” (51:58)

Hapa ni kana kwamba anaanza Risaalah ya tatu, kwa kuwa tumeshatangulia kusoma Risaalah mbili: ya kwanza ni masuala manne yaliyomo katika Suurat-ul-´Aswr, ya pili ni masuala matatu, Risaalah ya tatu ndio hii na Risaalah ya nne ni misingi mitatu.
Uongofu ndio Dini ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), na upotofu ndio Dini ya Abu Jahl na mfano wao. Hii ni neema kubwa Allaah Akikuongoza katika utiifu Wake, na utiifu ni kufanya yale ambayo Allaah Kakuamrisha na kujiepushe na yale ambayo kakukataza. Mtu anafanya haya kwa kuogopa adhabu ya Allaah na kutaraji malipo kutoka kwake.
al-Haniyfiyyah mi Mila Khaalisw kwa Allaah. Hanaaf ni kuelemea na kukengeuka kutoka katika Shirki. Hii ndio maana yake kilugha. Na Ibraahiym alikuwa Haniyfah Muislamu, yaani akielemea kutoka katika Shirki na kumtakasia ´Ibaadah Allaah  (´Azza wa Jalla). Hii ni katika sifa za Ibraahiym (´alayhis-Swalaat was-Salaam).
ثُمَّ أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ أَنِ اتَّبِعْ مِلَّةَ إِبْرَاهِيمَ حَنِيفًا
“Kisha Tukakuletea Wahy (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kwamba fuata Dini ya Ibraahim haniyfaa  (aliyejiengua na dini potofu akaelemea Dini ya haki).” (16:123)
 مَا كَانَ إِبْرَاهِيمُ يَهُودِيًّا وَلَا نَصْرَانِيًّا وَلَـٰكِن كَانَ حَنِيفًا مُّسْلِمًا
”Hakuwa Ibraahiym Yahudi wala Naswara; lakini alikuwa haniyfaa, (aliyejiengua na dini potofu akaelemea Dini ya haki); Muislamu.” (03:67)

قُلْ إِنَّنِي هَدَانِي رَبِّي إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ دِينًا قِيَمًا مِّلَّةَ إِبْرَاهِيمَ حَنِيفًا ۚ وَمَا كَانَ مِنَ الْمُشْرِكِينَ
”Sema: (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): “Hakika mimi, Amenihidi Mola wangu katika njia iliyonyooka, Dini iliyosimama thabiti, Mila ya Ibraahiym Haniyfaa (aliyejiengua na dini potofu akaelemea Dini ya haki) na na hakuwa miongoni mwa washirikina.” (06:161)
Hizi ni Sifa za Ibraahiym ya kwamba alikuwa Haniyfah na ndio ilikuwa Mila yake isiyokuwa ndani yake Shirki. Na Kaamrishwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kufuata Mila hii.
ثُمَّ أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ أَنِ اتَّبِعْ مِلَّةَ إِبْرَاهِيمَ حَنِيفًا
“Kisha Tukakuletea Wahy (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kwamba fuata Dini ya Ibraahim haniyfaa  (aliyejiengua na dini potofu akaelemea Dini ya haki).” (16:123)
Na tumeamrishwa sisi pia kufuata Mila hii ya Ibraahiym (´alayhis-Salaam):
هُوَ اجْتَبَاكُمْ وَمَا جَعَلَ عَلَيْكُمْ فِي الدِّينِ مِنْ حَرَجٍ ۚ مِّلَّةَ أَبِيكُمْ إِبْرَاهِيمَ ۚ هُوَ سَمَّاكُمُ الْمُسْلِمِينَ
 
”Yeye Ndiye Amekuteueni (kuwa Ummah bora kabisa), na Hakukufanyieni ugumu wowote (ule) katika Dini. Dini ya baba yenu Ibraahiym. Yeye (Allaah) Ndiye Aliyekuiteni Waislamu.” (22:78)
Hili ndilo tumeloamrishwa, ndio Dini ya Mitume (´alayhimus-Swalaat was-Salaam) wote. Mila hii imenasibishwa kwake (Ibraahiym) kwa kuwa Ibraahiym (´alayhis-Salaam) ndio Mtume bora baada ya Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), na ndio baba wa Mitume (´alayhimus-Salaam), na kutokana pia na kazi maalum aliyoifanya katika kulingania katika Tawhiyd na kukataza Shirki, hii Mila ndio maana ikawa imenasibishwa kwake. Mitume wote waliokuja baada yake ni katika kizazi chake. Nayo ni Mila ya Tawhiyd na kumtakasia ´Ibaadah Allaah. Na Mila hii ya Ibraahiym ni lazima kwa Waislamu wote waijue, haitoshi kujinasibisha nayo (Uislamu) bila ya kuijua, na bila ya kujua yanayoivunja, Shari´ah ya Kiislamu na Ahkaam zake. Ni lazima mtu aijue ili aweze kuifuata na asiulizwe akasema hajui. Mila ya Ibraahiym ni ipi? Ni kumuabudu Allaah na kumtakasia Yeye Dini. Hii ndio Mila ya Ibraahiym. Mtu ajumuishe mambo haya mawili. Kwa kuwa yule atakayemuabudu Allaah pasina kumtakasia ´Ibaadah, ´Ibaadah yake haitokuwa sahihi. Kama kuomba, kuchinja kwa asiyekuwa Allaah n.k.
Watu wengi wanaojinasibisha na Uislamu leo wanatumbukia katika Shirki kubwa; wanaomba asiyekuwa Allaah, ´Ibaadah ya makaburi, kuyachinjia, kuyawekea nadhiri, kutabarruk kwayo, kuwachinjia maiti na mengineyo, ilihali na wao wanasema ni Waislamu. Watu hawa hawajui Mila ya Ibraahiym aliyokuwemo Mtume Muhammad. Hawajui. Au wameijua na wakaenda kinyume nayo kwa ujuzi na hili ndio baya zaidi. Hivyo Mila ya Ibraahiym haikubaliani na Shirki, na atakayeichanganya ´amali yake na Shirki huyo hayuko katika Mila ya Ibraahiym hata kama anajinasibisha kwayo na kudai ya kwamba ni Muislamu. Hili ndio linalotakikana kuijua Mila ya Ibraahiym, kushikamana nayo na kuifanyia kazi. Kusiwe katika ´Ibaadah yako Shirki kubwa wala  ndogo. Hii ndio Mila ya Ibraahiym (´alayhis-Salaam).


Na maana ya  ((waniabudu Mimi)) ni: Wanipwekeshe. Na jambo kuu kabisa Aloamrisha Allaah ni At-Tawhiyd ambayo ni: Kumpwekesha Allaah katika ´Ibaadah. Na jambo kuu kabisa Alokataza ni shirki, ambayo ni: kumwabudu mwengine (au chochote kingine) pamoja Naye. Na dalili ni kauli Yake Ta´ala:
وَاعْبُدُوا اللَّـهَ وَلَا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا
”Na mwabuduni Allaah na wala msimshirikishe na chochote.” (04:36)


Sio kila mwenye kumuabudu Allaah anakuwa ni mwenye kumtakasia Yeye Dini. Bali miongoni mwao (Waislamu) wako wanaochanganya Dini na Shirki. Huu hazingatiwi ya kwamba yumo katika Dini ya Ibraahiym, al-Haniyfiyyah. Bali huyu yuko katika Mila (Dini) ya Shirki. Na kwa hilo Allaah Kawaamrisha hilo watu wote na Kawaumba kwa hilo.
وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ
 
”Na Sikuumba majini na watu wa isipokuwa waniabudu.” (51:56)

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اعْبُدُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُمْ وَالَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ
”Enyi watu! Mwabuduni Mola wenu Ambae Amekuumbeni na wale wa kabla yenu mpate kuwa na taqwa.” (02:21)
Huu ni wito kwa watu wote na ndio lengo la Allaah Kuwaumba ili wamuabudu. Binaadamu na majini. Majini wapo ila hatuwaoni, hata hivyo wapo na wao wamekalifishwa kwa ´Ibaadah. Mwenye kupinga kuwepo kwa majini huyo ni kafiri, kwa kuwa anamkadhibisha Allaah, Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Ijmaa´ ya Waislamu. Allaah Kawaumba majini na binaadamu kwa leongo moja nalo ni ili wamuabudu tu, na Allaah Hana haja nao bali binaadamu wao ndio wenye haja naye. Aayah hii ni dalili ya kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) Hakuwaumba viumbe bure tu hivi hivi, bali Kawaumba kwa lengo maalum. Hakuwaumba ili wale, wanye, walale n.k. Hapana.
Na maana ya “liyaabudun (waniabudu)” yaani wanipwekeshe Mimi na ´Ibaadah. Hivyo ´Ibaadah na Tawhiyd maana yake ni moja. Na hii ni Radd kwa wale wenye kufasiri Tawhiyd ya kwamba maana yake ni kukiri ya kwamba Allaah ndiye Muumba, Mwenye Kuruzuku, Mwenye kuendesha mambo, mwenye kuhuisha na kufisha, hii sio Tawhiyd ambayo viumbe wameumbwa kwa ajili yake. Bali wameumbwa ili wamuabudu, kwa ajili ya Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah. Kwani hata Ibliys hakuipinga Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah, alisema: “Mola Wangu”.  Haikupinga yeyote. Hivyo maana ya Tawhiyd ni ´Ibaadah. Kubwa Aliloamrisha Allaah ni ´Ibaadah, na kubwa Alilokataza ni Shirki. Dalili ni kauli ya Allaah:
وَاعْبُدُوا اللَّـهَ وَلَا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا ۖ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا وَبِذِي الْقُرْبَىٰ وَالْيَتَامَىٰ وَالْمَسَاكِينِ وَالْجَارِ ذِي الْقُرْبَىٰ وَالْجَارِ الْجُنُبِ وَالصَّاحِبِ بِالْجَنبِ وَابْنِ السَّبِيلِ وَمَا مَلَكَتْ أَيْمَانُكُمْ
”Na mwabuduni Allaah na wala msimshirikishe na chochote. Na wafanyieni ihsaan wazazi wawili na jamaa wa karibu, na mayatima, na masikini na majirani wa karibu na majirani walio mbali, na rafiki wa ubavuni na msafiri na wale iliyowamiliki mikono yenu ya kulia.” (04:36)
Hii inaitwa Aayah ya haki kumi. Na haki ya kwanza Aliyoanza nayo kabisa ni ya Allaah, kisha ndio akafuatisha haki za wengine. Ikiwa ndio kitu cha kwanza Alichoanza kwacho Allaah, basi ni wajibu kuanza kwacho katika kufunza. Mtu aanze kwa kujifunza ´Aqiydah kabla ya kitu kingine chochote, baada ya kujifunza mtu awabainishie wengine. Na leo kuna madai ya watu kuipuuza ´Aqiydah, kuna watu wamepewa mtihani huu wa kuipuuza ´Aqiydah. Tawhiyd ni ipi? Je, ni kuamini ya kwamba Allaah ndio Muumba, Mwenye Kuruzuku, Kuhuisha na Kufisha? Hapana. Tawhiyd ni kumpwekesha Allaah kwa kumtakasia Allaah ´Ibaadah. Hakuna mtu mwenye akili duniani anaamini ya kwamba kuna mwenye kuumba mbinguni na ardhini asiyekuwa Allaah. Hakuna mtu hata mmoja duniani – wakiwemo makafiri na Malaahidah – ya kwamba kuna mtu yeyote, binaadamu kwenye ardhi anayetamka, kunywa, kutembea aliyemuumba binaadamu.
وَلَئِن سَأَلْتَهُم مَّنْ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ لَيَقُولُنَّ اللَّـهُ
 
”Na ukiwauliza: “Ni nani aliyeumba mbingu na ardhi?” bila shaka watasema: “Allaah”.” (31:25)
أَمْ خُلِقُوا مِنْ غَيْرِ شَيْءٍ أَمْ هُمُ الْخَالِقُونَ أَمْ خَلَقُوا السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ ۚ بَل لَّا يُوقِنُونَ
 
”Au wameumbwa pasipo na kitu chochote, au wao (wenyewe) ndio waumbaji? Au wameumba mbingu na ardhi? Bali hawana yakini.” (52:35-36)
Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah hii ni ya kimaumbile na ipo akilini. Lakini haitoshi. Tanabahi hili.
Na kubwa Alilokataza Allaah ni Shirki. Kwa kuwa kuna watu ambao wanaamini ya kwamba kuna kubwa zaidi ya Shirki. Wanasema Ribaa na Zinaa ndio haramu iliyokubwa. Na ndio maana utawaona ni wenye kutilia nguvu katika kukataza Ribaa, Zinaa, tabia mbaya lakini hawalipi umuhimu suala la kukataza Shirki ilihali wanaona watu wametumbukia ndani yake. Huu ni ujinga mkubwa wa kutoifahamu Shari´ah ya Allaah. Kubwa kuliko Ribaa, Zinaa, kunywa pombe, kuiba, kula mali za watu kwa dhuluma, kamari na mengine yote ni Shirki. Dalili  ni Kauli ya Allaah:
قُلْ تَعَالَوْا أَتْلُ مَا حَرَّمَ رَبُّكُمْ عَلَيْكُمْ ۖ أَلَّا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًاۖ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا ۖ وَلَا تَقْتُلُوا أَوْلَادَكُم مِّنْ إِمْلَاقٍ ۖنَّحْنُ نَرْزُقُكُمْ وَإِيَّاهُمْ ۖ وَلَا تَقْرَبُوا الْفَوَاحِشَ مَا ظَهَرَ مِنْهَا وَمَا بَطَنَ ۖ وَلَا تَقْتُلُوا النَّفْسَ الَّتِي حَرَّمَ اللَّـهُ إِلَّا بِالْحَقِّ ۚذَٰلِكُمْ وَصَّاكُم بِهِ لَعَلَّكُمْ تَعْقِلُونَ وَلَا تَقْرَبُوا مَالَ الْيَتِيمِ إِلَّا بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ حَتَّىٰ يَبْلُغَ أَشُدَّهُۖ وَأَوْفُوا الْكَيْلَ وَالْمِيزَانَ بِالْقِسْطِ ۖ لَا نُكَلِّفُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا ۖ وَإِذَا قُلْتُمْ فَاعْدِلُوا وَلَوْ كَانَ ذَا قُرْبَىٰ ۖ وَبِعَهْدِ اللَّـهِ أَوْفُوا ۚ ذَٰلِكُمْ وَصَّاكُم بِهِ لَعَلَّكُمْ تَذَكَّرُونَ
"Sema: “Njooni nikusomeeni yale Aliyoyaharamisha Mola wenu kwenu. Kwamba: Msimshirikishe na chochote, na muwafanyie wema wazazi wawili, na wala msiwaue watoto wenu kutokana na umasikini. Sisi Tunakuruzukuni pamoja nao. Na wala msikaribiefawaahish (machafu; zinaa, liwati n.k.) yaliyo dhahiri na yaliyo siri. Na wala msiue nafsi ambayo Ameiharamisha Allaah (kuiua) isipokuwa kwa haki. Hivyo ndivyo Alivyokuusieni (Allaah) kwayo mpate kutia akilini. “Na wala msiikaribie mali ya yatima (kuila) isipokuwa kwa njia bora (ya kumtengenezea hicho chake) mpaka afikie kubalege. Na timizeni kipimo na mizani kwa uadilifu. Hatukalifishi nafsi isipokuwa kwa wasaa wake. Na mnaposema (katika kushuhudia) basi semeni kwa uadilifu japokuwa ni jamaa wa karibu. Na timizeni Ahadi ya Allaah.  Hivyo ndivyo Alivyokuusieni (Allaah) kwayo mpate kukumbuka (na kuwaidhika).” (06:151-152)

لَّا تَجْعَلْ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ فَتَقْعُدَ مَذْمُومًا مَّخْذُولًا
”(Ee bin-Aadam!) Usifanye pamoja na Allaah ilaaha(mungu) mwengine, ukaja kushutumiwa na mwenye kutupiliwa mbali (Motoni).” (17:22)
Aayah hii (ya Suurat-ul-An´aam) inaitwa wasia kumi. Na jambo la kwanza Aliloanza nalo Allaah ni Kutomshirikisha. Na katika Suurat-ul-Israa katika makatazo Kaanza kwa Kukataza Shirki na Kamalizia kwa kukataza Shirki. Ni dalili ya kwamba hilo ndilo kubwa Alilokataza Allaah (Ta´ala). Na katika Hadiyth Swahiyh:
“Ni dhambi ipi kubwa? Akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Ni kumfanyia Allaah mshirika Naye Ndiye Kakuumba... “
Kaanza kwa kusema kuwa ni Shirki ndio dhambi ya kwanza kubwa.
“Jiepusheni na madhambi saba yenye kuangamiza.” Wakasema: “Ewe Mtume wa Allaah! Ni yapi hayo?” Akasema: “Ni kumshirikisha Allaah, uchawi, kuiua nafsi ambayo Allaah Kaiharamisha kuuliwa isipokuwa kwa haki, kula Ribaa, kula mali ya mayatima, kukimbia siku ya vita na kuwazulia uongo wa kuzini wanawake wa Kiislamu waliohifadhika.”
Kaanza pia kwa Shirki. Ni dalili ioneshayo ya kwamba Shirki ndio dhambi ya kwanza kubwa. Na mshirikina hatoingia Peponi.
إِنَّهُ مَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ حَرَّمَ اللَّـهُ عَلَيْهِ الْجَنَّةَ وَمَأْوَاهُ النَّارُ ۖ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنصَارٍ
”(Kwani) Hakika mwenye kumshirikisha Allaah bila shaka Allaah Atamharamishia Jannah, na makazi yake yatakuwa ni Motoni. Na madhalimu hawatopata mwenye kunusuru yeyote.” (05:72)
Mshirikina Allaah Hatomsamehe.
إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ
“Hakika Allaah Haghufuri kushirikishwa; lakini Anaghufuria yasiyokuwa hayo kwa Amtakae.” (04:48)
Mshirikina kuharamishiwa Pepo na Allaah Kutomsamehe mshirikina. Ni dalili ioneshayo ya kwamba Shirki ndio dhambi kubwa. Ama madhambi mengine yote chini ya Shirki yako chini ya matakwa ya Allaah. Muumini bila kujali wingi wa madhambi yake yuko katika matakwa ya Allaah. Akitaka Mwenyewe Atamsamehe na Akitaka Atamuadhibu.
Ikiwa Shirki ndio dhambi kubwa, hivyo ni wajibu kwa wanachuoni na wanafunzi kuikataza na kuitahadharisha. Wasinyamaze kukataza Shirki. Na ni wajibu kuwapiga Jihaad washirikina kukiwa uwezo wa kufanya hivyo. Kama jinsi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alivyowapiga Jihaad.
فَاقْتُلُوا الْمُشْرِكِينَ حَيْثُ وَجَدتُّمُوهُمْ 
“Basi waueni washirikina popote muwakutapo.” (09:05)
Ni wajibu kuwapiga vita washirikina na kubainisha ni nini Shirki ili watu waweza kujiepusha nayo. Hili ndio la wajibu. Ama kunyamazia Shirki na kuwaacha watu katika ´Ibaadah badala ya Allaah ilihali wanadai ni Waislamu na wala hakuna yeyote anayekataza wala kutahadharisha. Hili ni jambo la khatari sana. Kuna watu wanaokataza Ribaa, Zinaa, kuwa na tabia mbaya, haya mambo ni haramu lakini si kama Shirki. Na kwa nini Shirki isikatazwe na kuichukulia sahali na kuwaacha watu kutumbukia humo? Je, huu ndio Uislamu? Hivyo, ni wajibu kuanza kwa kukataza Shirki.
Na ni nini Shirki? Ni kuomba kwa asiyekuwa (badala ya) Allaah. Atakayefanya ´Ibaadah kumfanyia asiyekuwa Allaah hii ndio Shirki. Unapaswa kujua maana ya Tawhiyd na Shirki. Kwa kuwa katika watu wako ambao wanaifasiri Shirki kinyume na tasfiri yake [sahihi] kama jinsi wako ambao wanafasiri Tawhiyd kinyume na maana yake. Kuna watu wanaosema Shirki ni al-Haakimiyyah, ndio ni Shirki ya utiifu. Ni aina miongoni mwa Shirki. Lakini kuna ambayo ni kubwa kuliko hii nayo ni ´Ibaadah badala ya Allaah; kwa kuchinja kuweka nadhiri, twawafu, kuomba msaada na kadhalika. Haya ni makubwa. Ni wajibu kutahadharisha Shirki ya kila sampuli. Na kuko wanaosema Shirki ni kuipenda dunia na mali, kuipenda mali sio Shirki kwa kuwa haya ni mapenzi ya kimaumbile, watu wanahitajia mali na wanaipenda. Allaah Kawakataza tu (na kuwakemea) wale wanaoitanguliza mali kabla ya Allaah. Hawa wanaosema hivi ima ni wajinga hawakusoma Tawhiyd au ni wadanganyifu.


Basi utakapoulizwa: “Nini Uswuul ath-Thalaathah (misingi mitatu) ambayo binaadamu anawajibika kuitambua?”. Sema: “Mja kumjua Mola wake, na Dini yake, na Nabii wake (صلي الله عليه وسلم).
Msingi Wa Kwanza: Kumjua Mola Mlezi.


1.    Msingi wa kwanza

Hivi sasa tunaingia katika Risaalah ya nne. Mtu kumjua Mola Wake, Dini Yake na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Shaykh kaanza kwa misingi hii mitatu kwa kuwa ndio msingi na ndio maswali matatu anayoulizwa mja kwenye kaburi lake. Atapowekwa ndani ya kaburi lake na akafukiwa na mchanga na watu wake wakaenda anajiwa na Malaika wawili kwenye kaburi lake, anarudishiwa uhai wake tena, al-Hayyaat al-Barzakhiyyah.  Wanamuuliza “ni nani Mola Wako, Dini yako na Mtume Wako?” Muumini atasema Mola Wangu ni Allaah, Uislamu ndio Dini yangu na Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndio Mtume wangu. Ataulizwa umejuaje? Atasema nimesoma Kitabu cha Allaah nikawa nimejua. Atanadi Mwenye kunadi na Kusema: “Kasema kweli mja Wangu”, mfungulieni mlango wa Peponi aanze kuneemeshwa humo. Atasema: “Ewe Mola wangu simamisha (lete) Qiyaamah” ili aweze kurejea kwa ahli zake na mali yake.
Ama mtu muovu, aliyeishi kwenye Ribaa, aliyeishi kwenye shaka na kutokuwa na yakini – hata kama atadai Uislamu – ikiwa alikuwa na mashaka katika Dini ya Allaah, atapoambiwa: “Ni nani Mola Wako, Dini na Mtume Wako? Atasema: “Aah, Aah sijui. Nilisikia watu wakisema nami nikawa nasema tu.” Yaani alikuwa mfuata kichwa mchunga tu huyu. Hakuwa muumini, bali alikuwa akisema hivi kwa njia ya Taqliyd. Huyu ni mnafiki ambaye alikuwa akidhihirisha Uislamu na kuficha unafiki. Atapigwa chuma cha moto minyama itasikia mlio wake, na lau binaadamu na majini wangelisikia wangelizima na kufa. Kisha atafunguliwa mlango wa Motoni aone mahali pake alipoandaliwa. Halafu atasema: “Ee Mola Wangu usisimamishe (usilete) Qiyaamah.”
Ikiwa mas-alah haya yana umuhimu kama huu, basi ni wajibu kwetu kujifunza nayo na kuyaamini. Na haitoshi tu kuyasoma, bali tujifunze nayo, tuyaamini na kuyafanyia kazi. Huenda Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) Akatuthibitisha wakati tutapoulizwa maswali. Hii misingi mitatu ina umuhimu mkubwa, na ndio maana Shaykh kayaweka wazi na kuyabainisha katika kitabu hichi.
Alipobainisha Shaykh misingi mitatu kwa ujumla, sasa anataka kuibainisha kwa ufafanuzi (msingi) mmoja baada ya mwingine kwa dalili zake katika Kitabu na Sunnah, Aayaat Ishara za Allaah ulimwengu na dalili za kiakili.


Basi utakapoulizwa: “Nani Mola wako?”. Sema: “Mola wangu ni Allaah Aliyenilea (kwa kuniruzuku, kuniendeshea mambo yote, kunisimamia kwa kila nilolihitaji) na Aliyewalea walimwengu wote kwa Neema Zake. Naye Ndiye Ninayemwabudu, na sina mwengine ninayemwabudu. Na dalili ni kauli Yake Ta´ala:
 الْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ
”Alhamduli-LLaah (Sifa njema zote ni za Allaah)  Mola wa  walimwengu.” (01:02)


Mola ni Yule Anayewalea waja Wake kwa neema na riziki. Anawalea baada ya Kuwaumba. Anawalea kwa Kuwapa riziki hata ndani ya matumbo ya mama zao, kuwapulizia pumzi mpaka anapotoka. Kisha baada ya kutoka Allaah Anamlea kwa neema ya afya, maziwa ya mama yake mpaka anapofikia kuweza kula chakula. Kisha Anaendelea kumlea kidogo kidogo mpaka anapobaleghe. Baada ya hapo Anamlea mpaka anapofikisha miaka arubaini. Huyu ndiye Mola. Kila kilichoko juu ya ardhi katika bari na bahari kinaneemeka kwa neema za Allaah.
وَمَا مِن دَابَّةٍ فِي الْأَرْضِ إِلَّا عَلَى اللَّـهِ رِزْقُهَا وَيَعْلَمُ مُسْتَقَرَّهَا وَمُسْتَوْدَعَهَا
”Na hakuna kiumbe chochote kitembeacho katika ardhi isipokuwa riziki yake iko kwa Allaah; na (Allaah) Anajua mahali pa kustakiri (pa kutulia na kukaa milele) na pa bohari (pa kuwekwa muda mdogo).” (11:06)
Huyu ndiye Mola. Ama wengine badala ya Allaah Hawamiliki katika riziki chochote. Bali wao wenyewe wanaruzukiwa. Na Yeye Mola Mwenye uwezo huu Yeye Ndiye Mwenye kustahiki kuabudiwa.
Kisha Shaykh akasema haitoshi kukiri Rubuubiyyah peke yake, bali ni lazima umjue pia kwa Kumuabudu na kumtakasia ´Ibaadah. Na hii ndio tofauti ya mpwekeshaji na mshirikina. Mpwekeshaji anakiri Rubuubiyyah na Kuabudiwa Kwake. Na mshirikina anakiri Rubuubiyyah lakini anamshirikisha katika ´Ibaadah Yake. Anaabudu badala ya Allaah, miti, mawe, mawalii, watu wema na makaburi. Na ndio maana akawa mshirika na kukiri kwake Rubuubiyyah hakukumuingiza katika Uislamu. Hii ndio maana “Naye Ndiye ninayemwabudu”, yaani Anayestahiki kuabudiwa. “Sina mwengine ninayemwabudu”, sawa Malaika, Mitume, watu wema, miti, mawe na kadhalila. Huku ndio kukiri Tawhiyd.


“Na kila kitu (watu, majini, Malaika n.k.)  kisichokuwa Allaah, ni walimwengu  (kimeumbwa)  nami ni mmojawapo wa waliwengu (walioumbwa).”


Hakuna mtu hata mmoja awezae kusema mimi ni Mola asiyekuwa Allaah. Hili haliwezekani kamwe. Hii ni dalili ya Rubuubiyyah ya Allaah. Na Akisha Yeye Ndiye Mola wa walimwengu, basi Yeye Ndiye Mwenye kustahiki ´Ibaadah. Na ndio maana baada ya Kusema:
الْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ
”Alhamduli-LLaah (Sifa njema zote ni za Allaah)  Mola wa  walimwengu. (01:02)
 Akafuatisha kwa Kusema:
 إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ
”Wewe Pekee tunakuabudu na Wewe Pekee tunakuomba msaada.” (01:05)
Yaani hatumuabudu yeyote asiyekuwa Wewe. Hatuna mwengine zaidi Yako. Hii ndio maana ya laa ilaaha illa Allaah.


Basi utakapoulizwa:  “Umemjuaje Mola wako?”. Sema: “Kutokana na Ishara Zake na Alivyoviumba. Na miongoni mwaIshara Zake ni: Usiku, mchana, jua, mwezi. Na miongoni mwa Alivyoviumba ni mbingu saba na ardhi saba, na kila kilichokuwemo ndani yake na baina yake”. Na dalili ni kauli  Yake Ta´ala:
وَمِنْ آيَاتِهِ اللَّيْلُ وَالنَّهَارُ وَالشَّمْسُ وَالْقَمَرُ ۚ لَا تَسْجُدُوا لِلشَّمْسِ وَلَا لِلْقَمَرِ وَاسْجُدُوا لِلَّـهِ الَّذِي خَلَقَهُنَّ إِن كُنتُمْ إِيَّاهُ تَعْبُدُونَ
”Na katika Aayah Zake, ni usiku na mchana, na jua na mwezi. (Basi) Msisujudie jua na wala (msisujudie) mwezi; bali msujudieni Allaah Ambaye Aliyeviumba (hivyo) ikiwa Yeye Pekee mnawambudu.” (41:37)
Na kauli Yake Ta´ala:
إِنَّ رَبَّكُمُ اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ يُغْشِي اللَّيْلَ النَّهَارَ يَطْلُبُهُ حَثِيثًا وَالشَّمْسَ وَالْقَمَرَ وَالنُّجُومَ مُسَخَّرَاتٍ بِأَمْرِهِ ۗ أَلَا لَهُ الْخَلْقُ وَالْأَمْرُ ۗ تَبَارَكَ اللَّـهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ
”Hakika Mola wenu ni Allaah Ambaye Ameumba mbingu na ardhi katika siku sita, kisha Istawaa juu ya ‘Arshi; (Yuko juu kwa namna inayolingana na Utukufu Wake Yeye Mwenyewe Allaah). Anafunika usiku kwa mchana, unaufuatia upesi upesi na (Ameumba) jua na mwezi na nyota (vyote) vimetiishwa kwa Amri Yake. Tanabahi! Ni Vyake Pekee Uumbaji na Amri. Tabaaraka-Allaahu (Ametukuka Allaah kwa Baraka) Mola wa walimwengu.” (07:54)


Ishaara yaani alama Zake. Na Alivyoviumba, kwani kila kitu mnachokiona kilikuwa hakipo, kisha Allaah ndio Akakileta kwa Kukiumba (Subhaanahu wa Ta´ala). Hakuna yeyote aliyeumba binaadamu, mbu n.k.
Na Aayaat (Ishara) ziko aina mbii:
-     kawniyyah, mbingu, ardhi, nyota, mwezi, jua, bahari n.k.
ambazo unashuhudia mwenyewe. Katika kila kitu kuna ishara inayotolea dalili kuonesha ya kwamba Allaah Yupo. Vipi basi mtu anaweza kupinga na kusema hakuna Muumba? Yaani ulimwengu wote huu na viumbe vimejileta vyenyewe pasina Muumba? Na ikiwa vimeumbwa na Muumba, ni nani Muumbaji huu kuliko Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala)? Kamwe hawezi kupatikana.
أَمْ جَعَلُوا لِلَّـهِ شُرَكَاءَ خَلَقُوا كَخَلْقِهِ فَتَشَابَهَ الْخَلْقُ عَلَيْهِمْ ۚقُلِ اللَّـهُ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ وَهُوَ الْوَاحِدُ الْقَهَّارُ
”Au wamemfanyia Allaah washirika wameumba kama uumbaji Wake, kisha vikawachanganyikia (vilivyoumbwa na washirika wao na Alivyoviumba Allaah) kwao?  Sema: “Allaah (Ndiye) Muumbaji wa kila kitu, Naye ni Al-Waahidul-Qahhaar (Mmoja Pekee - Mshindi Mwenye kudhibiti na kudhalilisha).” (13:16)
-    Na aina ya pili kuna Aayaat al-Qur-aaniyyah.
ambazo zinasomwa tangu ilipoteremshwa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Yote haya yanatolea dalili kuwepo kwa Allaah na kwamba Yeye Mwenyewe Ndiye Anastahiki ´Ibaadah Mmoja asiyekuwa na mshirika. Ishara zake za kawniyyah, ni usiku, mchana, jua na mwezi.
قُلْ أَرَأَيْتُمْ إِن جَعَلَ اللَّـهُ عَلَيْكُمُ اللَّيْلَ سَرْمَدًا إِلَىٰ يَوْمِ الْقِيَامَةِ مَنْ إِلَـٰهٌ غَيْرُ اللَّـهِ يَأْتِيكُم بِضِيَاءٍ ۖ أَفَلَا تَسْمَعُونَ
 
”Sema: “Je, mnaonaje (kama) Allaah Angelikujaalieni usiku (unaoendelea) moja kwa moja (bila ya kukoma) mpaka Siku ya Qiyaamah, nani mungu (mwengine) asiyekuwa Allaah (atayeweza) kukuleteeni mwanga? Je, basi hamsikii?” (28:71)

وَمِن رَّحْمَتِهِ جَعَلَ لَكُمُ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ لِتَسْكُنُوا فِيهِ وَلِتَبْتَغُوا مِن فَضْلِهِ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ
 
”Na kutokana na Rahmah Yake, Amekujaalieni usiku na mchana ili mpate (katika usiku) utulivu humo, na ili mpate (katika mchana) kutafuta katika fadhila Zake, na ili mpate kushukuru.” (28:73)
Hizi ni katika alama za Allaah, kuwepo kwa usiku na mchana.
Isitoshe usiku na mchana vinaenda kwa mpangilio, hakuna kimoja wapo kinachotangulia chenzake wala kubadilika. Vinaenda kwa mpangilio mmoja. Hii ni dalili ya Hekima ya Allaah. Hii ni dalili ya Rubuubiyyah na Uungu Wake. Allaah Ndiye ambaye Kaumba mbingu saba - tabaka moja juu ya nyingine - na juu yake Yuko Yeye Ar-Rahmaan. Na Akaumba pia ardhi saba na vilivyomo ndani yake. Yote haya ni katika Ishara Zake za ulimwengu.
Ni nani anayefanya ulimwengu mzima wote kuwa na giza katika siku moja, kisha anafanya pia unakuwa ni wenye kuangaza katika siku moja? Ni Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).
وَمِنْ آيَاتِهِ اللَّيْلُ وَالنَّهَارُ وَالشَّمْسُ وَالْقَمَرُ ۚ لَا تَسْجُدُوا لِلشَّمْسِ وَلَا لِلْقَمَرِ وَاسْجُدُوا لِلَّـهِ الَّذِي خَلَقَهُنَّ إِن كُنتُمْ إِيَّاهُ تَعْبُدُونَ
”Na katika Aayah Zake, ni usiku na mchana, na jua na mwezi. (Basi) Msisujudie jua na wala (msisujudie) mwezi; bali msujudieni Allaah Ambaye Aliyeviumba (hivyo) ikiwa Yeye Pekee mnawambudu.” (41:37)
Katika viumbe vikubwa ni jua na mwezi. Lakini hata hivyo, haijuzu kuviabudu kwa kuwa navyo ni viumbe havistahiki kuabudiwa. Viumbe vyote havistahiki kuabudiwa, isipokuwa ambaye Anastahiki kuabudiwa ni Allaah Pekee. Anayestahiki kusujudiwa ni Allaah Pekee. Hii ni haki ya Allaah (´Azza wa Jalla).
إِنَّ رَبَّكُمُ اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ يُغْشِي اللَّيْلَ النَّهَارَ يَطْلُبُهُ حَثِيثًا وَالشَّمْسَ وَالْقَمَرَ وَالنُّجُومَ مُسَخَّرَاتٍ بِأَمْرِهِ ۗ أَلَا لَهُ الْخَلْقُ وَالْأَمْرُ ۗ تَبَارَكَ اللَّـهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ
”Hakika Mola wenu ni Allaah Ambaye Ameumba mbingu na ardhi katika siku sita, kisha Istawaa juu ya ‘Arshi; (Yuko juu kwa namna inayolingana na Utukufu Wake Yeye Mwenyewe Allaah). Anafunika usiku kwa mchana, unaufuatia upesi upesi na (Ameumba) jua na mwezi na nyota (vyote) vimetiishwa kwa Amri Yake. Tanabahi! Ni Vyake Pekee Uumbaji na Amri. Tabaaraka-Allaahu (Ametukuka Allaah kwa Baraka) Mola wa walimwengu.” (07:54)
Hii “Inna” yaani maana yake ni “naapa kwa Allaah ya kwamba Mola Wenu ni Allaah” Ambaye Anawalea kwa Kuwaneemesha neema Zake. Na baada ya Kusema hivyo, Akatoa dalili ya kuonesha Uungu Wake kwa kusema:
”Ambaye Ameumba mbingu na ardhi... ”
Hivi kuna yeyote kweli ambaye anaweza kupinga ya kwamba sio Allaah  ambaye Ameumba mbingu na ardhi? Akasema hapana ni mimi, au ni fulani au ni sanamu? Kamwe kabisa. Hakuna yeyote Aliyefanya hivyo. Kaviumba kwa siku sita kwa Hekima Aijuayo Yeye Mwenyewe. Alianza Kuumba siku ya Ijumaa na Akamaliza siku ya Ijumaa. Ndio maana siku ya Ijumaa ikawa ni siku bora na Idi (sikukuu) ya wiki. Kisha Akastawaa juu ya ´Arshi ambayo imebeba Malaika. Na haina maana ya kwamba Allaah Anahitajia ´Arshi bali Yeye Allaah Ndiye Kaiumba na Kuizuia hiyo ´Arshi. Hivyo ´Arshi ndio inamuhitajia Allaah (Jalla wa ´Alaa). Allaah Kastawaa juu yake kwa Hekima.
al-´Uluw ni Sifa ya Dhati. Ama al-Istiwaa ni Sifa ya Kitendo Anafanya hivyo wakati Atakapo. Jua na mwezi vyote vinatembea juu ya ardhi. Na ardhi iko thabiti imestakiri. Kaifanya ardhi imetulia na iko thabiti kwa faida ya waja. Na mwezi, jua na nyote vinazunguka huu yake. Na si kama wanavyosema watu wa leo wanaida elimu wanasema ya kwamba jua ndio liko thabiti na ardhi inazunguka katika jua hilo. Maneno haya ni kinyume na yaliyo katika Qur-aan. Anasema Allaah (Ta´ala):
وَالشَّمْسُ تَجْرِي لِمُسْتَقَرٍّ لَّهَا
”Na jua linatembea kwa muda wake (uliopangwa) wa kustakiri (kituoni) kwake.” (36:38)
Na hawa watu wanasema hapana. Jua liko thabiti. Yaa Subhaana Allaah. Si kwamba haya yanasemwa na makafiri, tatizo ni kwamba baadhi ya Waislamu wanawasadikisha na wanakubali nadharia hii nayo inakwenda kinyume kabisa na Qur-aan Tukufu. Subhaana Allaah! Hili ni batili. “Ni Vyake Pekee Uumbaji na Amri”.
Amri ziko aina mbili:
- Amri za kawniyyah,
- Amri Shar´iyyah.
Kawniyyah ni kama Kuumba Kwake jua, mwezi, mbingu n.k. Ama amri Shar´iyyah ni kama Swalah, Swawm, kufunga na kadhalika. Ikishakuwa Kuumba na Amri zote ni Zake, kumebaki nini tena? Hakuna kilichobaki.
Hapa kuna Radd kwa wale wanaosema Qur-aan imeumbwa. Kwa kuwa Qur-aan ni katika amri. Na amri ya Allaah Haikuumbwa. Allaah Katofautisha baina ya Kuumba na Amri na Hakuvifanya ni kitu kimoja, bali viwili tofauti. Qur-aan inaingia katika Amri kitu ambacho Hakikuumbwa. Na hili ndio jambo ambalo Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) aligombana kwa Jahmiyyah. Walipomwambia aseme kuwa Qur-aan imeumbwa, akasema: “Qur-aan ni katika Uumbaji au Amri?” Wakasema ni katika Amri. Akasema basi haikuumbwa. Allaah Katofautiisha baina ya hivyo viwili. Kafanya Uumbaji ni kitu na Amri ni kitu kingine. Tabaaraka-Allaahu (Ametukuka Allaah kwa Baraka) Mola wa walimwengu. Baraka zote ni za Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Haijuzu kumwambia kiumbe namna hii, bali kiumbe anaambiwa “Baaraka Allaahu fiyka”. Na baraka zinatoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) tu.
Katika Aayah hii kunakukiri kwa Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah na Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah.


Na Mola Ndiye mwenye kuabudiwa. Na dalili ni kauli Yake Ta´ala:
يَا أَيُّهَا النَّاسُ اعْبُدُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُمْ وَالَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ فِرَاشًا وَالسَّمَاءَ بِنَاءً وَأَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَخْرَجَ بِهِ مِنَ الثَّمَرَاتِ رِزْقًا لَّكُمْ ۖ فَلَا تَجْعَلُوا لِلَّـهِ أَندَادًا وَأَنتُمْ تَعْلَمُونَ
”Enyi watu! Mwabuduni Mola wenu Ambae Amekuumbeni na wale wa kabla yenu mpate kuwa na taqwa. Ambaye Amewafanyieni ardhi kuwa ni tandiko na mbingu kuwa ni paa, na Akateremsha kutoka mbinguni maji, Akawatolea kwayo matunda kuwa ni riziki zenu. Basi msimuwekee Allaah waliolingana naye (washirika) na hali ya kuwa nyinyi mnajua (kuwa Allaah Hana Anayelingana nae).” (02:21)

Ibn Kathiyr  amesema: “Muumbaji wa vitu hivi Ndiye Anayestahiki kuabudiwa na kwa aina ya ´Ibaadah ambazo Ameziamrisha, mfano: Al-Islaam Uislamu, Al-Iymaan imani, Al-Ihsaan Ihsani, na miongoni mwazo ni Ad-Du’aa du‟aa, na Al-Khawf khofu (ya kuogopa mtu au adhabu au kitu), na Ar-Rajaa matarajio, na At-Tawakkul  kutegemea au kutawakali,na Ar-Raghbah shauku (utashi na matumaini ya jambo la kupendwa), na Ar-Rahbah tisho au kuogopa, na Al-Khushuu’ unyeyekevu, na  Al-Khashyahkhofu kutokana na utukufu wa Allaah nayo inahusiana na elimu na taqwa (uchaji), na  Al-Inaabah kurejea (kutubu na utiifu), na Al-Isti’aanah kuomba msaada wa mambo ya kidunia au ya Akhera, na  Al-Isti’aadhah kuomba kinga, na Al-Istighaathah kuomba msaada, kuokolewa, au kufarijiwa jambo au haja wakati wa shida au kuokolewa, na Adh-Dhab-hu kuchinja, na AnNadhru kuweka nadhiri, na mengineyo ya aina za ´Ibaadah ambazo Allaah Ameziamrisha. Zote ziwe kwa ajili ya Allaah.

Na dalili ni kauli Yake:

وَأَنَّ الْمَسَاجِدَ لِلَّـهِ فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا
 
”Na kwamba Misikiti ni (kwa ajili) ya Allaah, basi msiombe (msimuabudu) yeyote pamoja na Allaah.” (72:18)
Basi atakayeelekeza (´Ibaadah) yoyote kwa asiyekuwa Allaah, basi yeye ni mshirikina kafiri. Na dalili ni kauli Yake Ta´ala:
وَمَن يَدْعُ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ لَا بُرْهَانَ لَهُ بِهِ فَإِنَّمَا حِسَابُهُ عِندَ رَبِّهِ ۚ إِنَّهُ لَا يُفْلِحُ الْكَافِرُونَ
 
”Na yeyote yule anayeomba (Du’aa au kuabudu) pamoja na Allaah mungu mwengine hana ushahidi wa wazi wa hilo; basi hakika hesabu yake iko kwa Mola wake. Hakika hawafaulu makafiri.” (23:117)

Na katika Hadiyth: ((Du´aa ni kiini cha ´Ibaadah)). [Hadiyth hii ni dhaifu, imepokelewa na At-Tirmidhiy]  - Taz Al-Mishkaat, Na. 2331. Lakini ipo Hadiyth kama hiyo ambayo ni sahihi isemayo ((Du´aa ni ´Ibaadah)) [ Taz. Swahiyhul-Jaami´us-Swaghiyr, Na. 3407]
Na dalili ni kauli Yake Ta´ala:
وَقَالَ رَبُّكُمُ ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ ۚ إِنَّ الَّذِينَ يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِي سَيَدْخُلُونَ جَهَنَّمَ دَاخِرِينَ
 
”Na Mola wenu Anasema: “Niombeni, Nitakuitikieni. Hakika wale wanaotakabari na‘Ibaadah Yangu, watauingika (Moto wa) Jahanam wadhalilike.” (40:60)


Mwenye Kustahiki ´Ibaadah ni Mola, ama asiyekuwa Yeye hastahiki ´Ibaadah kwa kuwa sio Mola. Haya ndio makusudio ya maneno ya Shaykh. Pia haitoshi kwa mtu kukiri Rubuubiyyah bali anatakiwa pia akiri kuwa Yeye Ndiye mwenye kustahiki kuabudiwa na asiyekuwa Yeye hastahiki kuabudiwa. Dalili ni Kauli ya Allaah:
يَا أَيُّهَا النَّاسُ اعْبُدُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُمْ وَالَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ
”Enyi watu! Mwabuduni Mola wenu Ambae Amekuumbeni na wale wa kabla yenu mpate kuwa na taqwa.” (02:21)
Wanasema wanachuoni wito wa kwanza katika Qur-aan ni huu. Hii ni amri. Na hapa ni wito kwa watu wote. Dalili ya Umola Wake ni kwa kuwa Yeye Ndiye Kawaumba; Malaika, wanaadamu, majini na viumbe vyengine visivyokuwa hivyo Yeye Ndiye Kaviumba. Basi mkishalikiri hilo msimfanyie Allaah wanaolingana Naye, yaani washirika hali ya kuwa mnajua ya kuwa hana wanayelingana Nae na hana washirika. Huu ni wito kwa viumbe wote kukiri Rubuubiyyah Yake (Subhaanahu wa Ta´ala) na kukanusha kwa asiyekuwa Yeye. Haya ndio makusudio ya maneno ya Shaykh.
Baada ya Shaykh kusema kuwa Mola ni Yule Mwenye Kuumba. Na akatoa dalili kwa Kauli ya Allaah:
يَا أَيُّهَا النَّاسُ اعْبُدُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُمْ وَالَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ
”Enyi watu! Mwabuduni Mola wenu Ambae Amekuumbeni na wale wa kabla yenu mpate kuwa na taqwa.” (02:21)
Akataka kubainisha maana ya ´Ibaadah na aina zake.
´Ibaadah katika lugha ni kujidhalilisha na kunyenyekea. ´Ibaadah ni mafungu mawili; ´Ibaadah ya jumla waja wote ni wa Allaah: Muislamu, kafiri, muumini n.k. wote ni waja wa Allaah bi maana wako chini ya uendeshaji Wake, na kwamba ni wajibu wamuabudu Allaah (Ta´ala). Hii ni maana ya ´Ibaadah kwa njia ya jumla. Wote wanaitwa waja wa Allaah, bi maana ni viumbe Vyake, vinamnyenyekea Yeye, hakuna hata mmoja Anayetoka katika Uendeshaji Wake na Ufalme Wake. Kama Alivyosema Allaah:
إِن كُلُّ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ إِلَّا آتِي الرَّحْمَـٰنِ عَبْدًا
 
”Hakuna yeyote (yule aliyomo) katika mbingu na ardhi isipokuwa (Siku ya kufufuliwa) atamfikia Ar-Rahmaan (Mwingi wa Rahmah) kuwa ni mja.” (19:93)
Aayah hii imejumuisha viumbe vyote.
Na aina ya pili ni uabudu maalum kwa waumini. Kama Alivyosema Allaah:
وَعِبَادُ الرَّحْمَـٰنِ الَّذِينَ يَمْشُونَ عَلَى الْأَرْضِ هَوْنًا
 
”Na waja wa Ar-Rahmaan (Mwingi wa Rahmah; ni wenye sifa zifuatazo:) ni wale wanaotembea katika ardhi kwa unyenyekevu.” (25:63)

إِنَّ عِبَادِي لَيْسَ لَكَ عَلَيْهِمْ سُلْطَانٌ

“Hakika waja wangu huna mamlaka nao.” (15:42)
Huu ni uabudu maalum, nao ni uabudu wa utiifu na kujikurubisha kwa Allaah na Tawhiyd. Hawa ni waja wa Allaah waumini. Huu ni uabudu maalum.
Na maana ya ´Ibaadah Kishari´ah wametofautiana wanachuoni kwa ibara yake. Miongoni mwao kuko wanaosema maana yake ni kujidhalilisha na kupenda kwa hali ya juu. Kama Alivyosema Ibnul-Qayyim katika “an-Nuuniyyah”. Na miongoni mwao kuko ambao wamesema ´Ibaadah ni yale Shari´ah iliyoyaamrisha ndio ´Ibaadah. Kwa kuwa ´Ibaadah ni Tawqiyfiyyah. Ibara hii ni sahihi. Lakini ibara iliyo wazi zaidi na ya jumla ni ile iliyosema Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah). Aliposema:
“´Ibaadah ni jina lililokusanya kila kile Anachokipenda Allaah na Kukiridhia, katika ´amali na kauli sawa za dhahiri na zilizojificha.”
Hii ni ibara iliyo wazi zaidi na imekusanya yote Aliyoyaamrisha Allaah. Kufanya yale ambayo Allaah Kaamrisha kwa kumtii Allaah na kuacha yale ambayo Allaah Kakataza kwa kumtii hii ndio ´Ibaadah. Sawa ikiwa hili linaonekana katika viungo vya mwili au likawa ndani ya moyo. Kwa kuwa ´Ibaadah inakuwa katika ulimi, moyo na viungo vya mwili. Ulimi ni kama Tasbiyh, Tahliyl, Dhikr, kutamka Shahaadah na kadhalika. Hali kadhalika  kila yaliyo ndani ya moyo ya kukukurubisha kwa Allaah (´Azza wa Jalla) ni ´Ibaadah; kama khofu, kurejea, kuogopa, shauku, tisho, kutawakali, kumpenda Allaah, kumtakasia Allaah ´Ibaadah, n.k. yote haya ni matendo ya moyoni lakini hatuyaoni. Hizi ni ´Ibaadah za kimoyo. Na hali kadhalika ´Ibaadah inakuwa katika viungo vya mwili; kama Rukuu´, Sujuud, Jihaad, Hijrah, Swawm, zote hizi ni ´Ibaadah za kimwili zinazodhiri katika viungo. Hivyo ´Ibaadah inakuwa katika ulimi, moyo na viugo vya mwili.
Kisha isitoshe, (´Ibaadah) inagawanyika katika ´Ibaadah za kimwili na ´Ibaadah za kimali.
- ´Ibaadah za kimwili ni hizo aina tatu tulizosema; inakuwa katika ulimi, moyo na viungo.
- Na ´Ibaadah inakuwa ya kimali; kama mfano wa kutoa Zakaah, kutoa katika Njia ya Allaah, kutoa katika Jihaad, Hajj – hii imejumuisha ´Ibaadah ya kimwili na ya kimali n.k.
Ama Swalah, na Swawm n.k. hizi ni ´Ibaadah za kimwili zisizokuwa na mali ndani yake. Na mfano wa ´Ibaadah ni kama Uislamu, Imani na Ihsaan. Hizi ndio aina tatu kubwa za ´Ibaadah. Uislamu kwa nguzo zake tano; Shahaadah, Swalah, Zakaah, Swawm na Hajj. Hizi zote ni ´Ibaadah kukiwemo ndani yake za kimali na za kimwili.
Hali kadhalika Imani kwa nguzo zake sita – na ni katika matendo ya kimoyo; kumuamini Allaah, Malaika Zake, Vitabu Vyake, Mitume Wake, Siku ya Mwisho, Qadar kheri na shari.
Hali kadhalika Ihsaan, nayo ni nguzo moja, umuabudu Allaah kana kwamba unamuona na ikiwa wewe humuoni basi yeye Anakuona. Ihsaan ndio aina ya ´Ibaadah iliyo juu zaidi.
Na katika aina za ´Ibaadah ni Du´aa, kwa kuwa ndio aina kubwa ya ´Ibaadah. Na ndio maana kaanza nayo Shaykh. Na Du´aa imegawanyika mafungu mawili; Du´aa ya ´Ibaadah na Du´aa ya mas-alah (maombi).
- Du´aa ya ´Ibaadah ni Kumsifu Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) bila ya kumuomba kitu. Kumsifu, Kumhimidi, Kumtukuza, Kumshukuru, yote haya ni Du´aa ya ´Ibaadah. Kama Ilivyo katika Suurat-ul-Faatihah:
الْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ   مَالِكِ يَوْمِ الدِّينِ  إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ
”Alhamduli-LLaah (Sifa njema zote ni za Allaah)  Mola wa  walimwengu. Ar-Rahmaanir-Rahiym (Mwingi wa Rahmah-Mwenye kurehemu). Maalik (Mfalme)  wa siku ya malipo.” (01:02-04)
Hii yote ni Du´aa ya ´Ibaadah.
إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ
”Wewe Pekee tunakuabudu na Wewe Pekee tunakuomba msaada.” (01:05)
- Hii ni Du´aa ya mas-alah. Du´aa ya mas-alah ni kuomba kitu kutoka kwa Allaah (´Azza wa Jalla). Kuomba uongofu, riziki, elimu kutoka kwa Allaah, Tawfiyq.


Na dalili ya Al-Khawf kukhofu ni kauli Yake Ta´ala:
إِنَّمَا ذَٰلِكُمُ الشَّيْطَانُ يُخَوِّفُ أَوْلِيَاءَهُ فَلَا تَخَافُوهُمْ وَخَافُونِ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ
”Hakika huyo ni shaytwaan anawakhofisha marafiki zake. Basi msiwakhofu, na nikhofuni Mimi mkiwa ni Waumini.” (03:175)


Dalili ni Kauli ya Allaah:
إِنَّمَا ذَٰلِكُمُ الشَّيْطَانُ يُخَوِّفُ أَوْلِيَاءَهُ فَلَا تَخَافُوهُمْ وَخَافُونِ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ
”Hakika huyo ni shaytwaan anawakhofisha marafiki zake. Basi msiwakhofu, na nikhofuni Mimi mkiwa ni Waumini.” (03:175)
 Khofu ni aina ya ´Ibaadah. Na khofu imegawanyika aina mbili:
-    Khofu ya ´Ibaadah
-    Khofu ya kimaumbile
1. Khofu ya ´Ibaadah kumfanyia asiyekuwa Allaah ni Shirki. Kama mtu kumuogopa asiyekuwa Allaah kwa yale asiyoyaweza yeyote isipokuwa Allaah Pekee. Hii ndio khofu ya ´Ibaadah. Kama mtu kuogopa mtu asimfanye akawa mgonjwa, akachukua roho yake, akaua mtoto wake. Kama ilivyo leo watu wengi wanaogopa majini, wachawi n.k. na kwa ajili hiyo ndio maana wanafanya mambo ya Shirki ili wasalimike. Kuwa mgonjwa, kufa, riziki, kuzuia riziki, kuteremsha baraka, kuondoa baraka, haya mambo yakuna ayawezae isipokuwa Allaah. Yeyote akiogopa kwa kitu asichokiweza mtu isipokuwa Allaah, hii ni Shirki kubwa. Kwa kuwa kafanya kitu katika mambo ya ´Ibaadah kumfanyia asiyekuwa Allaah. Ni kama wale wanaogopa makaburi, majini, Mashaytwaan yasiwaletee madhara, wanaenda na kujikurubisha kwa mambo ili kujikinga na madhara yake. Hii ni Shirki kubwa. Kwa kuwa inaitwa khofu ya ´Ibaadah. Wanaogopa makaburi, mawalii, Mashaytwaan na majini.
2. Aina ya pili ni khofu ya kimaumbile, nayo ni kule kuogopa kitu cha dhahiri, anaweza kwa unachomuogopea. Kama kumuogopa aliye hai, nyoka, dhalimu haya ni mambo yako dhahiri na yanajulikana. Kuogopa vitu hivi vilivyo hai na kutahadhari navyo, hii haiitwi kuwa ni Shirki. Hii ni khofu ya kimaumbile. Na ndio maana Allaah Akasema kuhusiana na Muusa:
فَأَوْجَسَ فِي نَفْسِهِ خِيفَةً مُّوسَىٰ
 
”Basi akahisi woga katika nafsi yake Muwsaa.” (20:67)
Hii ni khofu ya kimaumbile.
Lakini inatakiwa kwa Muislamu achukue (afanye) sababu ambazo zitamkinga na madhara haya na amtegemee Allaah (´Azza wa Jalla). Na ambaye anamtegemea Allaah Anamtosheleza.
فَمَن كَانَ يَرْجُو لِقَاءَ رَبِّهِ فَلْيَعْمَلْ عَمَلًا صَالِحًا وَلَا يُشْرِكْ بِعِبَادَةِ رَبِّهِ أَحَدًا
“Hivyo anayetaraji kukutana na Mola wake, na atende ‘amali njema na wala asimshirikishe katika ‘ibaadah za Mola wake yeyote.” (18:110)


Na dalili ya Ar-Rajaa kutaraji ni kauli Yake Ta´ala:
فَمَن كَانَ يَرْجُو لِقَاءَ رَبِّهِ فَلْيَعْمَلْ عَمَلًا صَالِحًا وَلَا يُشْرِكْ بِعِبَادَةِ رَبِّهِ أَحَدًا
“Hivyo anayetaraji kukutana na Mola wake, na atende ‘amali njema na wala asimshirikishe katika ‘ibaadah za Mola wake yeyote.” (18:110)


Kutaraji pia ni aina ya ´Ibaadah. Hivyo haifai mtu kurataji isipokuwa kutoka kwa Allaah. Na Allaah Hakuishia Kusema mtu ataraji peke yake, bali ataraji na afanye ´amali njema kama imevyokuja katika Aayah. Na “´amali” njema ni ile imekusanya sharti mbili:
-    Iwe ndani yake ina Ikhlaasw
-    al-Mutaaba´ah (kufanya kwa kumfuata/kumuiga Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)
Moja ya sharti hizi ikitoka hiyo itakuwa sio ´amali njema na mwenye nayo hakubaliwi bali atarudishiwa yeye mwenyewe.


Na dalili ya At-Tawakkul kutegemea kauli Yake Ta´ala:
وَعَلَى اللَّـهِ فَتَوَكَّلُوا إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ
“Na kwa Allaah Pekee tawakalini ikiwa nyinyi ni Waumini.” (05:23)
Na kauli Yake:
وَمَن يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ فَهُوَ حَسْبُهُ
”Na yeyote (yule) anayetawakali kwa Allaah, basi Yeye Humtosheleza.” (63:03)


وَعَلَى اللَّـهِ فَتَوَكَّلُوا إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ
“Na kwa Allaah Pekee tawakalini ikiwa nyinyi ni Waumini.” (05:23)
Kutegemea pia ni katika aina kubwa ya Imani. Na ndio maana hapa Kaleta kwa kusema “Na kwa Allaah Pekee” yaani kuonesha kama kuzuia. Ni dalili ioneshayo ya kwamba yule asiyetegemea kwa Allaah sio muumini. Muumini daima anamtegemea Allaah (´Azza wa Jalla). Na wala haijuzu kusema namtegemea fulani, kwa kuwa kutegemea ni ´Ibaadah. Bali mtu anaweza kusema nimemuwakilisha fulani, na mtu asiseme namtegemea. Inajuzu kumuwakilisha mtu kwa kitu akiwezacho. Mtu anatakiwa kufanya sababu kisha amtegemee Allaah. Kufanya sababu hakupingani na kumtegemea Allaah, si kwamba mwenye kufanya sababu hamtegemei Allaah. Unapaswa kufanya sababu kisha ndio umtegemee Allaah. Ila usitegemee kitendo chako, bali mtegemee Allaah. Ukioa, kuoa ni sababu ya kupata mtoto, lakini usitegemei kupata mtoto kwa kujivunia vile umeoa, bali unatakiwa kumtegemea Allaah.
Kuna baadhi ya watu hawafanyi sababu na wanasema tunamtegemea Allaah, hili ni makosa. Na wengine kinyume chake wanafanya sababu kisha wanategemea hiyo sababu kwa kusema mimi nimeshafanya sababu basi yatosha ntapata ninachokitaka, hili pia ni makosa. Yule ambaye anamtegemea Allaah, basi Allaah peke Yake Anamtosheleza. Na nia yake ikiwa ni ya kweli, basi Allaah atafikia anachokitaka. Hatohitajia yeyote mwengine. Hii ndio faida na matundo ya kumtegemea Allaah.

Na dalili ya  Ar-Raghbah shauku (utashi na matumaini ya jambo la kupendwa) na Ar-Rahbah (tisho au kuogopa) na  Al-Khushuu’(unyenyekevu) ni kauli Yake Ta´ala:
إِنَّهُمْ كَانُوا يُسَارِعُونَ فِي الْخَيْرَاتِ وَيَدْعُونَنَا رَغَبًا وَرَهَبًا ۖ وَكَانُوا لَنَا خَاشِعِينَ
 
”Hakika wao walikuwa wakikimbilia katika mambo ya kheri, na (walikuwa) wakituomba kwa matumaini na khofu, na walikuwa Kwetu wenye kunyenyekea.” (21:90)


ar-Rahbah na khofu maana yake ni moja. Hali kadhalika unyenyekevu ni aina pia ya ´Ibaadah.
“Hakika wao” hapa inawarejelea Mitume (´alayhimus-Swalaat was-Salaam). Walikuwa wakikimbilia na kuharakia kufanya mambo ya kheri. Walikuwa wakitumai Rahmah ya Allaah na wakiogopa adhabu. Wanamuomba Allaah kwa kumuogopa na wakimuomba pia kwa kutaraji kupata [malipo] kutoka Kwake. Wanamuomba Allaah Awape kheri na Awakinge na shari. Hii ndio maana ya Raghbah na Rahbah. Na walikuwa wakinyenyekea hali kadhalika kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Walikuwa wakijumuisha baina ya sifa tatu: Shauku, kuogopa na kunyenyekea. Hizi ndio sifa za Mitume (´alayhimus-Salaam). Na hizi ndio aina tatu katika aina ya ´Ibaadah.
Na kuna Radd kwa Suufiyyah ambao wanasema sisi hatumuabudu Allaah kwa shauku (kutumaini) kupata thawabu kutoka Kwake wala kuogopa adhabu Yake. Isipokuwa tunamuabudu kwa kumpenda tu. Haya ni maneno ya batili. Mitume wanamuomba Allaah kwa shauku na kuogopa, ilihali wao ndio bora ya viumbe. Je, Suufiyyah ni wakamilifu zaidi kuliko Mitume (´alayhimus-Swalaat was-Salaam)? Kamwe!


Na dalili ya Al-Khashyah kuogopa au uchaji ni kauli Yake Ta´ala:
فَلَا تَخْشَوْهُمْ وَاخْشَوْنِي
”Basi msiwaogope bali Niogopeni Mimi.” (02:150)


al-Khashyah kuogopa ni aina ya khofu, nayo iko chini ya khofu. Hizi ni katika sifa za  Mitume wa Allaah (´alayhimus-Swalaat was-Salaam) na waja wa Allaah wema, na ni aina kubwa katika aina za ´Ibaadah. Na ni katika matendo ya moyo yasiyojua yeyote isipokuwa Allaah.


Na dalili ya Al-Inaabah kurejea (kutubu na utiifu) ni kauli Yake:
وَأَنِيبُوا إِلَىٰ رَبِّكُمْ وَأَسْلِمُوا لَهُ
 
“Na rejeeni (kutubu) kwa Mola, na jisalimisheni Kwake.” (39:54)


Na al-Inaabah maana yake ni kurejea. Na maana yake ni Tawbah. Kurejea na Tawbah maana yake ni moja. Lakini baadhi ya wanachuoni wanasema kurejea ni chini ya Tawbah.
وَأَنِيبُوا إِلَىٰ رَبِّكُمْ وَأَسْلِمُوا لَهُ مِن قَبْلِ أَن يَأْتِيَكُمُ الْعَذَابُ ثُمَّ لَا تُنصَرُونَ
 
“Na rejeeni (tubuni) kwa Mola, na jisalimisheni Kwake kabla haijakufikieni adhabu kisha hamtonusuriwa.” (39:54)
Inapokuja adhabu Tawbah na kurejea Kwake hakukubaliwi. Inapoteremka adhabu ya kuangamiza Tawbah ya mwenye kutubia haikubaliwi. Tawbah ya yule ambaye yuko katika kukata roho haikubaliwi, na Tawbah ya yule ambaye adhabu ya kuangamiza imemteremkia haikubaliwi, na Tawbah pindi jua litapochomoza magharibi kabla ya kusimama kwa Qiyaamah haikubaliwi wakati huo. Tawbah ina wakati wake unaoisha, kwa mtu binafsi na watu wote kwa jumla. Nukta yenyewe, ni kurejea ambako ni kutubu. Hii ni dalili ya kwamba kurejea kwa Allaah ni aina katika aina za ´Ibaadah.


Na dalili ya  Al-Isti’aanah kuomba msaada wa mambo ya kidunia au ya Akhera ni kauli Yake Ta´ala:
إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ
”Wewe Pekee tunakuabudu na Wewe Pekee tunakuomba msaada.” (01:05)

Na katika Hadiyth: ((Ukitaka kuomba msaada, basi mwombe Allaah)) [At-Tirmidhiy ni Hadiyth Swahiyh kama alivyothibitisha Al-Albaaniy]


al-Isti´aanah ni kuomba msaada, na kumegawanyika sehemu mbili:
1.    Kuomba msaada kwa kitu kisichoweza yeyote isipokuwa Allaah (Ta´ala).
Jambo hili kumfanyia (kumuomba) asiyekuwa Allaah ni Shirki. Atakayemuomba asiyekuwa Allaah kwa kitu ambacho hakiwezi yeyoye isipokuwa Allaah huyu kashirikisha, kwa kuwa kamfayia ´Ibaadah asiyekuwa Allaah (´Azza wa Jalla).
2.    Aina ya pili ni kumuomba msaada kwa kitu anachokiweza kiumbe. Anasema Allaah (Ta´ala):
وَتَعَاوَنُوا عَلَى الْبِرِّ وَالتَّقْوَىٰ ۖ وَلَا تَعَاوَنُوا عَلَى الْإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ
“Shirikianeni katika wema na taqwa, na wala msishirikiane   katika dhambi na uadui.” (05:02)
Kuomba msaada kwa mambo ya kawaida ambayo watu wanayaweza; kumuomba aliye hai, yupo (mbele yako) na ni muweza (wa unachomuomba), hili halina ubaya. Allaah Katuamrisha kusaidiana katika wema na uchaji Allaah.
Ama kuwaomba viumbe kwa mambo wasiyoyaweza isipokuwa Allaah; kama kukupa riziki, kukukinga na madhara, haya hafanyiwi yeyote isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Kama kuwaomba msaada maiti, majini Mashaytwaan, watu walioghaibu – wasiokusikia (wala wewe huwaoni) - hii ni Shirki kubwa. Kwa kuwa unaomba msaada kwa kitu asichokiweza kukufanyia.


Na dalili ya Al-Isti’aadhah kuomba kinga ni kauli Yake Ta´ala:
قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ الْفَلَقِ
 
”Sema: “Najikinga na Mola wa mapambazuko.” (113:01)
na
قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ النَّاسِ
 
”Sema: “Najikinga na Mola wa watu.” (114:01)

Na dalili ya  Al-Istighaathah kuomba  msaada, kuokolewa, au  kufarijiwa jambo au haja wakati wa shida ni kauli Yake Ta´ala:
إِذْ تَسْتَغِيثُونَ رَبَّكُمْ فَاسْتَجَابَ لَكُمْ
”Na (kumbukeni) pale mlipomuomba msaada Mola wenu Naye Akakujibuni.” (08:09)

Na dalili ya Adh-Dhab-h kuchinja kauli Yake Ta´ala:

قُلْ إِنَّنِي هَدَانِي رَبِّي إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ دِينًا قِيَمًا مِّلَّةَ إِبْرَاهِيمَ حَنِيفًا ۚ وَمَا كَانَ مِنَ الْمُشْرِكِينَ قُلْ إِنَّ صَلَاتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ لَا شَرِيكَ لَهُ ۖ وَبِذَٰلِكَ أُمِرْتُ وَأَنَا أَوَّلُ الْمُسْلِمِينَ
”Sema: (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): “Hakika mimi, Amenihidi Mola wangu katika njia iliyonyooka, Dini iliyosimama thabiti, Mila ya IbraahiymHaniyfaa (aliyejiengua na dini potofu akaelemea Dini ya haki) na na hakuwa miongoni mwa washirikina. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): “Hakika Swalaah yangu, na Nusukiy(kuchinja kafaara na ‘ibaadah zangu) na uhai wangu na kufa kwangu ni kwa ajili ya Allaah (Pekee) Mola wa walimwengu. Hana mshirika, na kwa hayo ndio nimeamrishwa, nami ni Muislamu wa kwanza  (waliojisilimisha kwa Allaah).” (06:161-163)

Na katika Sunnah:  ((Allaah Amemlaani  aliyechinja kwa ajili ya asiyekuwa Allaah)) [Muslim]

Na dalili ya nadhiri kauli Yake Ta´ala:
يُوفُونَ بِالنَّذْرِ وَيَخَافُونَ يَوْمًا كَانَ شَرُّهُ مُسْتَطِيرًا
 
”(Ambao) Wanatimiza nadhiri (zao), na wanaiogopa siku ambayo shari yake ni yenye kuenea.” (76:07)


al-Isti´aadhah ni kuomba kinga. Na kuomba kinga ni aina katika aina za ´Ibaadah, haijuzu kuomba kinga kwa asiyekuwa Allaah (´Azza wa Jalla). Atakayeomba kinga kaburi, wathan, sanamu, au kitu chochote asiyekuwa Allaah (´Azza wa Jalla) huyu anakuwa mshirikina Shirki kubwa. Anasema Allaah:
وَأَنَّهُ كَانَ رِجَالٌ مِّنَ الْإِنسِ يَعُوذُونَ بِرِجَالٍ مِّنَ الْجِنِّ فَزَادُوهُمْ رَهَقًا

”Na kwamba walikuwa wanaume miongoni mwa watu wanajikinga na wanaume miongoni mwa majini, basi wakawazidishia mzigo (wa madhambi na kufru).” (72:06)

قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ الْفَلَقِ  مِن شَرِّ مَا خَلَقَ
 
”Sema: “Najikinga na Mola wa mapambazuko. Kutokana na shari ya Alivyoviumba.” (113:01-02)
al-Falaq ni asubuhi, yaani unaomba kinga kwa Mola wa mapambazuko ya asubuhi kutokana na shari ya viumbe wote. Ni dalili ya kwamba kuomba kinga ni ´Ibaadah na haijuzu kufanyiwa asiyekuwa Allaah. Usiombe kinga kutoka kwa viumbe. Na yule ambaye ataomba kinga viumbe basi huyo kamshrikisha Allaah (´Azza wa Jalla). Na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anamwambia ´Abdullaah bin ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa):
“Na utakapoomba kinga basi muombe Allaah.”


Msingi Wa Pili: Kujua Dini ya Kiislamu kwa dalili. Nayo ni kujisalimisha kwa Allaah kwa Tawhiyd, na kunyenyekea katika utiifu, na kujiweka mbali na shirki pamoja na watu wake (wa shirki), nao (huo Msingi wa pili) umegawanyika katika daraja tatu; Uislamu, Iymaan, Ihsaan. Na kila daraja ina nguzo.


2.    Msingi wa pili

Baada ya Shaykh kubainisha msingi wa kwanza ambao ni kumjua Allaah kwa dalili, akaenda sasa kubainisha msingi wa pili ambao ni kuijua Dini ya Uislamu kwa dalili. Dini kunakusudiwa utiifu; kufanya aliyoamrishwa mtu na kuacha aliyokatazwa. Na kunaposemwa Dini kunakusudiwa pia hesabu. Kama Kauli ya Allaah:
 مَالِكِ يَوْمِ الدِّينِ
”Maalik (Mfalme)  wa siku ya malipo.” (01:04)
yaani Maalik wa siku ya hesabu.
“... kwa dalili”, dalili ya kwamba kuujua Uislamu hakukuwi kwa kufuata kichwa mchunga. Dini ni lazima mtu aifuate kwa dalili katika Kitabu na Sunnah. Ama mtu ambaye hajui Dini yake na kazi yake yeye ni kufuata watu na akawa kama kipofu. Huyu hakuijua Dini Yake. Na atakapoulizwa ndani ya kaburi, atasema: “Aah, Aah sijui. Niliwasikia watu wakisema kitu nami nikasema.” Hivyo ni lazima kwa mtu kuijua Dini Yake, na aijue kwa dalili kutoka katika Kitabu na Sunnah za Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Na wala hawezi kujua hili isipokuwa kwa kuisoma Dini Yake na kutafuta elimu.
Uislamu maana yake ni kujisalimisha.
بَلَىٰ مَنْ أَسْلَمَ وَجْهَهُ لِلَّـهِ
“Naam! (Hilo ni tamanio lao, bali) Yeyote aliyeusalimisha uso wake kwa Allaah.” (02:112)
yaani kamtakasia ´amali zake Allaah (´Azza wa Jalla) na kunyenyekea Kwake. Kunyenyekea kikamilifu kwa Mola Wake. Ni nani utakayejisalimisha Kwake ikiwa hukujisalimisha kwa Mola Wako? Utajilisalimisha kwa Shaytwaan au maadui? Haifai kwako kujisalimisha kwa maadui, bali watakiwa kujisalimisha kwa Allaah na Mola Wako. Kujisalimisha kwa Allaah kwa Tawhiyd, nako ni kumpwekesha Allaah (Jalla wa ´Alaa) kwa ´Ibaadah. Hii ndio maana ya Tawhiyd. Atakayemuabudu Allaah Mmoja asiyekuwa na mshirika, basi huyo kajisalimisha Kwake, na kunyenyekea kwa utiifu kwa yale Aliyoyaamrisha kwayo na Kukukataza kwayo. Aliyokuamrisha unayafanya na Aliyokukataza unajiweka nayo mbali kwa kumtii Allaah.
Na kujiweka mbali na Shirki na watu wake, kwa kuwa unaamini upotofu wa Shirki. Hivyo watakiwa kujiweka mbali. Na uitakidi uadui wa washirikina, kwa kuwa ni maadui wa Allaah (´Azza wa Jalla). Na wala usiwafanye wakawa ni vipenzi vyako. Bali watakiwa kuwachukulia kuwa ni maadui. Kwa kuwa ni maadui wa Allaah na wa Mtume Wake na wa Dini Yake. Usiwapende na wala usiwafanye kuwa ni mawalii, bali watakiwa kuwakata katika mambo ya dini yao ya ´Ibaadah, ujiweke nayo mbali, na uamini upotofu waliyomo. Usiwapende ndani ya moyo wala usiwanusuru kwa kauli na kitendo. Kwa kuwa ni maadui wa Mola Wako na ni maadui wa Dini yako na ni maadui wa Mtume wako (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Vipi utawapenda na kufanya nao urafiki (ilihali ni maadui wa Mola Wako)? Huu ndio Uislamu.
Haitoshi kwako kule kujisalimisha kwa Allaah na kunyenyekea kwa utiifu, lakini ukawa wewe hujiweki mbali na Shirki na washirikina. Hili haliwezekani. Wala huzingatiwi kuwa wewe ni Muislamu. Mpaka usifike kwa sifa hizi tatu: kujisalimisha kwa Allaah kwa Tawhiyd, na kunyenyekea kwa utiifu – yaani baada ya kujisalimisha unanyenyekea Kwake kwa kufanya ´Ibaadah na utiifu, na kujiweka mbali na yanaokwenda kinyume na hayo, yaani Tawhiyd na utiifu – nayo ni Shirki na watu washirikina. Kwa haya unakuwa wewe ni Muislamu. Utaposifika kwa sifa hizi tatu unakuwa ni Muislamu. Ama ukikosa moja katika hayo, huwi Muislamu.
Na ni Waislamu wangapi wasiojua maana ya Uislamu, kwa kuwa hakusoma mambo haya. Na ukimwambia: “Nini maana ya Uislamu?” Hajui kitu. Hata akihifadhi matamshi haya, haitoshi. Lazima ayafanyie kazi. Elimu pamoja na ´amali. Huu ndio Uislamu kwa kifupi. Lazima uyajue ili uwe Muislamu wa kihakika na si Muislamu wa kujinasibisha na madai tu.
Kwa masikitiko makubwa watu wengi hawajui haya, hata wale wanaodai ya kwamba ni Madu´aat ukiwauliza nini maana ya Uislamu hawatokujibu kwa jibu sahihi. Kwa kuwa hawakusoma mambo haya. Huu ndio Uislamu.


Daraja Ya Kwanza: Uislamu
Na nguzo za Kiislamu ni sita: ((Kukiri kwa moyo na kutamka kwamba hakuna apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah, na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, na kusimamisha Swalah, na kutoa Zakaah, na kufunga Ramadhaan, na kuhiji Nyumba Takatifu ya Allaah))


Ama daraja zake ni tatu: Uislamu, Imani na Ihsaan. Dini ya Uislamu ina daraja zake, baadhi yazo ziko juu kuliko zingine.
Daraja ya kwanza ni Uislamu, daraja ya pili ni Imani na daraja ya tatu ni Ihsaan.
1.    Daraja ya kwanza Uislamu
Muislamu anapoingia katika Uislamu na pengine akawa na mambo yanayokwenda kinyume, maasi mbali mbali na mengineyo, huyu anaitwa Muislamu. Hata wanafiki wanaingia katika Uislamu wanaitwa Waislamu duniani. Wakidhihirisha Uislamu, wakasimama nao na wakaushikilia kwa uinje, wanaitwa ni Waislamu na wanapewa haki za Waislamu duniani. Lakini Aakhirah watakuwa katika tabaka ya chini kabisa Motoni, kwa kuwa hawana Imani. Na Muislamu mwenye madhambi makubwa na madhambi mengi ambaye kasalimika na Shirki pia yeye anaitwa kuwa ni Muislamu, lakini yeye ana kitu katika Imani. Ama mnafiki yeye hana kitu katika Imani kabisa.
2.    Daraja ya pili Imani
Kisha daraja ya pili inakuwa ni Imani. Imani ni kitu maalum kuliko Uislamu, kwa kuwa haambiwi mtu ana Imani isipokuwa yule ambaye ni mkweli.
إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ آمَنُوا بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ ثُمَّ لَمْ يَرْتَابُوا وَجَاهَدُوا بِأَمْوَالِهِمْ وَأَنفُسِهِمْ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ ۚأُولَـٰئِكَ هُمُ الصَّادِقُونَ
 
”Hakika Waumini ni wale waliomwamini Allaah na Mtume Wake, kisha wakawa si wenye shaka, na wakafanya jihaad kwa mali zao na nafsi zao katika njia ya Allaah. Hao ndio  wakweli.” (49:15)
Walipoambiwa bedui hamjaamini, Allaah Aliwabainishia ni kina nani waumini.
إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ آمَنُوا بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ ثُمَّ لَمْ يَرْتَابُوا وَجَاهَدُوا بِأَمْوَالِهِمْ وَأَنفُسِهِمْ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ ۚأُولَـٰئِكَ هُمُ الصَّادِقُونَ
 
”Hakika Waumini ni wale waliomwamini Allaah na Mtume Wake, kisha wakawa si wenye shaka, na wakafanya jihaad kwa mali zao na nafsi zao katika njia ya Allaah. Hao ndio  wakweli.” (49:15)
Haya walikuwa mabedui hawajayafanya. Daraja ya Imani ni ya juu kuliko daraja ya Uislamu, haambiwi mtu ana Imani isipokuwa ambaye ni mkweli moyoni mwake na kashikamana na utiifu anamtii Allaah (´Azza wa Jalla) na kajiepusha na maasi, na anapotekeleza anakimbilia kufanya Tawbah. Huyu ndiye muumini. Na wote – muislamu na muumini – wako Peponi, lakini zinatofautiana daraja zao Peponi kutokana na daraja zao katika Dini. Kama Alivyosema Allaah (Ta´ala):
ثُمَّ أَوْرَثْنَا الْكِتَابَ الَّذِينَ اصْطَفَيْنَا مِنْ عِبَادِنَا ۖ فَمِنْهُمْ ظَالِمٌ لِّنَفْسِهِ وَمِنْهُم مُّقْتَصِدٌ وَمِنْهُمْ سَابِقٌ بِالْخَيْرَاتِ بِإِذْنِ اللَّـهِ 
”Kisha Tukawarithisha Kitabu wale Tuliowachagua miongoni mwa waja Wetu. Basi miongoni mwao (yuko) dhalimu wa nafsi yake (kwa dhambi na maovu mengi), na miongoni mwao (yuko) aliyekuwa wastani (katika kutenda mema na maovu), na miongoni mwao (yuko) aliyesabiki kwa mambo mengi ya kheri kwa idhini ya Allaah.” (35:32)
“Dhalimu wa nafsi yake” huyu ni muumini ambaye ana kitu katika maasi na madhambi makubwa chini ya Shirki. “Aliyekuwa wastani” ni yule kajiepusha na mambo ya haramu na akafanya mambo ya utiifu – na anaweza kuwa na kitu katika mambo ya makruhu na akaacha baadhi ya mambo mengi ya mustahaba. Aliishia kwa haya na wala hakuzidisha kitu katika mambo ya mustahaba. Kashikamana na kufanya mambo ya wajibu na kuacha ya haramu. Huyu ni aliyekuwa wastani. “Aliyesabiki kwa mambo mengi ya kheri” hii ndio daraja ya juu kabisa. Ni yule mtu ambaye kafanya mambo ya wajibu na ya mustahaba, na kaacha mambo ya haramu na ya makruhu na baadhi ya mambo ya mubaahah. Huyu ndiye aliyesabiki kwa mambo mengi ya kheri. Kisha Akasema:
ذَٰلِكَ هُوَ الْفَضْلُ الْكَبِيرُ جَنَّاتُ عَدْنٍ يَدْخُلُونَهَا يُحَلَّوْنَ فِيهَا مِنْ أَسَاوِرَ مِن ذَهَبٍ وَلُؤْلُؤًا
”Hiyo ndio fadhila (ya Allaah) kubwa. Bustani za milele wataziingia, (na) watapambwa humo (Peponi) katika (mapambo ya) vikuku vya dhahabu na lulu.” (35:32-33)
Watu sampuli hii tatu wote wataingia Peponi. “Dhalimu wa nafsi yake, aliyekuwa wastani, aliyesabiki kwa mambo mengi ya kheri”. Wote wataingia Peponi lakini kwa kutofautiana manzilah na daraja zao Peponi. Itatokana na ´amali zao.
3.    Daraja ya tatu Ihsaan
Daraja ya tatu – na ndio ya juu kabisa – ni Ihsaan. Mtu awe na Ihsaan baina yake yeye na Allaah. Afanye Ihsaan katika ´Ibaadah ya Allaah (´Azza wa Jalla). Kaifasiri Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Ihsaan kuwa:
“Ni kumuabudu Allaah kama vile unamuona, na ikiwa wewe humuoni basi Yeye Anakuona.”
Kwa yakini, uwe na yakini kama vile anakuona Allaah (´Azza wa Jalla). Uwe na ujuzi ya kwamba Allaah Anakuona popote ulipo. Huyu ndiye Muhsin na ndio aliyesabiki kwa mambo mengi ya kheri. Waislamu wako daraja mbali mbali; miongoni mwao kuna Muislamu, Muumini na Muhsin. Inategemea na ´amali zao na wanayosimama kwayo moyoni mwao. Lakini wote – Alhamdulillaah – ni Waislamu. Hawaambiwi Waislamu wote kuwa ni Muhsinuun, na wala hawaambiwi Waislamu wote kuwa ni waumini, lakini wote wanaambiwa kuwa ni Waislamu. Uislamu ni jina la kijumla na pana. Na kila daraja katika daraja hizi tatu zina nguzo zake. Uislamu una nguzo zake, Imani ina nguzo zake na Ihsaan ina nguzo zake.
Nguzo za Uislamu ni tano:
1.    Kushahidilia ya kwamba hapana mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah,
2.    Kusimamisha Swalah,
3.    Kutoa Zakaah,
4.    Kufunga Ramadhaan, na
5.    Kwenda kuhiji Nyumba ya Allaah Tukufu
Uislamu hausimami isipokuwa kwa nguzo hizi tano. Zikivunjika, Uislamu hausimami. Uislamu ni mpana, lakini hizi ndio nguzo zake. Na baki ya utiifu, ni yenye kukamilisha nguzo hizi. Utiifu wote na matendo ya kheri ni yenye kukamilisha nguzo hizi. Kama alivyosema hilo Jibriyl (´alayhis-Salaam) katika Hadiyth maarufu.


Na dalili ya Shahada ni kauli Yake Ta´ala:
شَهِدَ اللَّـهُ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ وَالْمَلَائِكَةُ وَأُولُو الْعِلْمِ قَائِمًا بِالْقِسْطِ ۚ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ
”Allaah Ameshuhudia kwamba hapana ilaaha (Anayestahiki kuabudiwa kwa haki) ila Yeye; na Malaika, na wenye elimu (wote wameshuhudia kwamba Yeye) ni Mwenye kusimamisha (uumbaji Wake) kwa uadilifu. Hapana ilaaha ila Yeye Al-‘Aziyzul-Hakiym (Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika daima - Mwenye hikmah wa yote daima).” (03:18)

Na maana yake ni: Hakuna muabudiwa wa haki ila Yeye, Pekee. (Laa ilaaha – hapana mungu) inakanusha kila kinachoabudiwa pasi Naye. (illaAllaah – isipokuwa Allaah)  na  kuthibitisha ´Ibaadah zote kwa ajili ya Allaah Pekee. Hana mshirika katika ´Ibaadah Zake kama Alivyokuwa hana mshirika katika Ufalme (Umiliki Wake wa Ulimwengu) Wake.
Na tafsiri inayobainisha wazi (Shahada), ni kauli Yake Ta´ala:
وَإِذْ قَالَ إِبْرَاهِيمُ لِأَبِيهِ وَقَوْمِهِ إِنَّنِي بَرَاءٌ مِّمَّا تَعْبُدُونَإِلَّا الَّذِي فَطَرَنِي فَإِنَّهُ سَيَهْدِينِ وَجَعَلَهَا كَلِمَةً بَاقِيَةً فِي عَقِبِهِ لَعَلَّهُمْ يَرْجِعُونَ 
”Na (taja ee  Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم pale) Ibraahiym alipomwambia baba yake na watu wake: “Hakika mimi najitoa dhima (sina jukumu) na yale mnayoyaabudu. “Isipokuwa Yule Ameniumba, basi hakika Yeye Ataniongoa. Na akalifanya neno (la ilaaha illaa-Allaah) lenye kubakia katika kizazi chake ili wapate kurejea.” (43:26)

Na kauli Yake:
 قُلْ يَا أَهْلَ الْكِتَابِ تَعَالَوْا إِلَىٰ كَلِمَةٍ سَوَاءٍ بَيْنَنَا وَبَيْنَكُمْ أَلَّا نَعْبُدَ إِلَّا اللَّـهَ وَلَا نُشْرِكَ بِهِ شَيْئًا وَلَا يَتَّخِذَ بَعْضُنَا بَعْضًا أَرْبَابًا مِّن دُونِ اللَّـهِ ۚ فَإِن تَوَلَّوْا فَقُولُوا اشْهَدُوا بِأَنَّا مُسْلِمُونَ
”Sema: “Enyi Ahlal-Kitaabi! Njooni katika neno lililo sawa baina yetu na baina yenu, kwamba tusiabudu isipokuwa Allaah Pekee, na wala tusimshirikishe na chochote, na wala tusichukue baadhi yetu sisi kwa sisi waungu badala ya Allaah.” Wakikengeuka; basi semeni: “Shuhudieni kwamba sisi ni Waislamu”.” (03:64)


Dalili ya Shahaadah ni Kauli Yake (Ta´ala):
شَهِدَ اللَّـهُ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ وَالْمَلَائِكَةُ وَأُولُو الْعِلْمِ قَائِمًا بِالْقِسْطِ ۚ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ
”Allaah Ameshuhudia kwamba hapana ilaaha (Anayestahiki kuabudiwa kwa haki) ila Yeye; na Malaika, na wenye elimu (wote wameshuhudia kwamba Yeye) ni Mwenye kusimamisha (uumbaji Wake) kwa uadilifu. Hapana ilaaha ila YeyeAl-‘Aziyzul-Hakiym (Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika daima - Mwenye hikmah wa yote daima).” (03:18)
 Allaah Kajitolea ushahidi Mwenyewe ya kwamba hakuna apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Yeye, Ushahidi wa Allaah ndio ushahidi mkubwa kabisa. Na Yeye ndiye Mkweli kabisa wa wakweli. Ushahidi Wake Yeye (Subhaanah) ndio Ushahidi mkubwa na wa kweli kabisa, kwa kuwa umetoka kwa Al-Hakiym, Al-Khabiyr, Al-´Aliym – Mwenye Kujua kila kitu. Na Malaika pia wameshuhudia ya kwamba hakuna apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Yeye. Malaika ni viumbe walioumbwa na Allaah ili wamuabudu. Waja wema.
يُسَبِّحُونَ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ لَا يَفْتُرُونَ
 
”Wanamsabihi usiku na mchana, wala hawazembei.” (21:20)
Kawaumba Allaah na Kuwawakilisha ili watekeleze amri Zake katika ulimwengu, Anayowaamrisha Allaah katika mambo ya ulimwengu. Na kila mmoja kawekwa kwa kazi yake. Na ushahidi wa Malaika ushahidi wao ni ushahidi wa kweli. Kwa kuwa ni wajuzi, wachaji Allaah na wenye kumjua Allaah (´Azza wa Jalla). Ni ushahidi ambao wametoa kwa ujuzi, maarifa na Ikhlaasw. Na wao ni katika viumbe bora. Na wenye elimu pia wameshuhudia hilo. Bila ya shaka ushahidi wa wenye elimu sio kama ushahidi wa wajinga, wenye elimu ni katika viumbe Wake, na hawashuhudii isipokuwa kwa yaliyo ya haki. Tofauti na wajinga, wao ushahidi wao hauzingatiwi. Na kila mwenye elimu anamtolea ushahidi Allaah kwa Umoja, ya kwamba hakuna apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Yeye. Hapa kuna cheo kwa wale wenye elimu kwa kule Allaah Kukubali ushahidi wao pamoja na Ushahidi Wake (Subhaanahu wa Ta´ala) na ushahidi wa Malaika Wake. Kawashahidisha wale wenye elimu katika viumbe Wake. Ni dalili ya kuonesha fadhila na hadhi yao (ya wanachuoni).
Makusudio ya wale wenye elimu ni elimu ya Kishari´ah na si kama wanavyosema baadhi ya watu ya kwamba ni wale wenye elimu za kidunia. Hawa hawaambiwi kuwa ni Ahl-ul-´Ilm, elimu yao ni yenye mipaka. Kunasemwa huyu ni mwenye elimu ya (ni msomi wa) hesabu, uhandisi, utabibu n.k. Na wala hawaambiwi kuwa ni Ahl-ul-´Ilm. Kunasemwa ni ´ulamaa wa utabibu, ´ulamaa wa uhandisi n.k. Ama kuambiwa kuwa ni Ahl-ul-´Ilm hapana. Hili haliambiwi isipokuwa wale wenye elimu ya Kishari´ah.
Isitoshe, watu hawa wengi wao ni Malaahidah.  Hawa wenye elimu za kidunia aghlabu elimu yao inawazidishia ujinga wa kutomjua Allaah (´Azza wa Jalla), kiburi na Ilhaad.  Kama mnavyoona wenyewe, leo jamii za kikafiri wamebobea katika elimu za kudunia lakini aghlabu wanakuwa makafiri, wengi wao ni makafiri. Vipi mtu atasema ya kwamba hawa ndio Ahl-ul-´Ilm ambao Allaah Kawataja katika Kauli Yake? Hapana. Hili haliingii akilini kamwe. Ndani yake kuna Malaahidah, mayahudi, manaswara, washirikana, waabudu makaburi, waabudu ng´ombe na kadhalika. Na hawa ni wenye elimu za kidunia. Pamoja na hili ni makafiri Malaahidah washirikina wapotofu. Hivyo sio wao ambao wamekusudiwa katika Aayah hii. Hali kadhalika katika Kauli Yake:
إِنَّمَا يَخْشَى اللَّـهَ مِنْ عِبَادِهِ الْعُلَمَاءُ
 
”Hakika wanaomkhofu Allaah (kikweli kweli) miongoni mwa waja Wake ni Ma’ulaamaa.” (35:28)
Makusudio ni wanachuoni wenye elimu za Kishari´ah ambao wanamjua Allaah ukweli wa kumjua na wanamuabudu ukweli wa kumuabudu na wanamuogopa. Ama watu hawa (wenye elimu za kidunia) wengi wao hawamuogopi Allaah (´Azza wa Jalla), bali wanamkufuru Allaah na kumkanusha. Na wanadai ya kwamba ulimwengu hauna Mola na wanaamini kuwa ni mazingira ndio yanaendesha mambo. Wanamkanusha Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) pamoja na kwamba wako na elimu za kudunia. Vipi mtu atasema kuwa hawa ndio Ahl-ul-´Ilm? Hili ni kosa.
Jina Ahl-ul-´Ilm ni jina tukufu na haliambiwi hawa Malaahidah na makafiri na kusema kuwa hawa ndio Ahl-ul-´Ilm.
Malaika na Ahl-ul-´Ilm wamemshuhudia Allaah (kuwa na) Umoja.
Alipotaja dalili ya Shahaadah akaibainisha na kuiweka wazi maana yake. Maana yake ni hakuna muabudiwa wa haki isipokuwa Allaah. Na maana yake si kama wanavyosema Ahl-ul-Baatwil: “Hakuna Muumba, Mwenye Kuruzuku isipokuwa Allaah.” Kwa kuwa hili ni Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah. Wanalikubali washirikana. Maana ya laa ilaaha ila Allaah maana yake sio hakuna Muumba na Mwenye Kuruzuku isipokuwa Allaah, kwa kuwa maana hii wanaikubali washirikana na wao hawasemi laa ilaaha illa Allaah. Anasema (Ta´ala):
إِنَّهُمْ كَانُوا إِذَا قِيلَ لَهُمْ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا اللَّـهُ يَسْتَكْبِرُونَ
”Hakika wao walipokuwa wakiambiwa: “Laa ilaaha illa Allaah” (Hapana mungu anayestahiki kuabudiwa kwa haki ila Allaah) hutakabari.” (37:35)

yaani kuacha mungu wao. Wanasema kumwambia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwa ndio mwendawazimu kwa kuwa kawakataza ´Ibaadah ya kuabudu masanamu. Na alipowaambia semeni “laa ilaaha illa Allaah” walisema:
أَجَعَلَ الْآلِهَةَ إِلَـٰهًا وَاحِدًا ۖ إِنَّ هَـٰذَا لَشَيْءٌ عُجَابٌ
 
“Amewafanya miungu (wote) kuwa ni Ilaah Mmoja (Anayestahiki kuabudiwa kwa haki)? Hakika hili ni jambo la ajabu mno!” (38:05)
Wao wanataka miungu wengi. Kila mmoja awe na mungu wake. Hawataki mungu mmoja.
Ni dalili kuonesha maana yake ni “hakuna mola wa haki”, na lau maana yake ingekuwa: “Hakuna Muumba wala Mwenye Kuruzuku ila Allaah”, hakika hili walikuwa wanalikiri (makafiri) na wala halikuwaingiza katika Uislamu. Maana yake ni kukanusha ´Ibaadah badala ya Allaah. Hii ndio maana yake sahihi.
Na lazima mtu aseme “... kwa haki”, lau utasema hakuna mungu isipokuwa Allaah hili ni kosa kubwa. Itakuwa masanamu yote na vinavyoabudiwa vyote ndio Allaah. Ametakasika Allaah na hilo. Lazima useme “hakuna muabudiwa wa haki... ”, au “hakuna muabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah”. Ama kusema hakuna mwenye kuabudiwa isipokuwa Allaah hili ni kosa kubwa. Na haya ndio madhehebu ya Wahdat-ul-Wujuud. Kwa masikitiko makubwa baadhi ya ´Awwaam wanasema “wala hakuna muabudiwa badala yake”, hata katika Swalah wakati wa kufungulia Swalah wanasema hivi. Hili ni kosa kubwa.
“Laa ilaaha” huku ni kukanusha kila kinachoabudiwa badala ya Allaah. “... illa Allaah” huku ni kuthibitisha ´Ibaadah zote kwa Allaah Pekee asiyekuwa na mshirika. Laa ilaaha illa Allaah imekusanyika juu ya kukanusha na kuthibitisha. Na ni lazima katika kumpwekesha Allaah kuwepo kukanusha na kuthibitisha, haitoshi kuthibitisha peke yake, na wala haitoshi kukanusha peke yake. Bali ni lazima kukanusha na kuthibitisha.
 فَمَن يَكْفُرْ بِالطَّاغُوتِ وَيُؤْمِن بِاللَّـهِ
“Basi atakayemkanusha twaaghuwt (miungu ya uongo) na akamwamini Allaah." (02:256)
وَاعْبُدُوا اللَّـهَ وَلَا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا
“Na mwabuduni Allaah na wala msimshirikishe na chochote.” (04:36)
Huku ni kukanusha na kuthibitisha. Lau utasema: “Allaah Ndiye Mungu” je yatosha? Hapana. Bali ni lazima kujumuisha baina yazo mpaka uhakikishe Tawhiyd na Shirki itokomee. Lau utasema: “Laa ilaahah hakuna mungu” peke yake, haya yatakuwa ni maneno ya Malaahidah ambao wanapinga kuwepo kwa Mola. Na lau utasema: “Allaahu Ilaah Allaah Ndiye Mungu” hili pia halitoshi, kwa kuwa halikanushi vinavyoabudiwa badala ya Allaah (´Azza wa Jalla). Lazima kuwepo ukanushaji na kuthibitisha.
Kamaliza (Rahimahu Allaah) kubainisha maana ya Shahaadah. Na dalili ya hilo ipo katika Kitabu cha Allaah. Laa ilaaha illa Allaah ina nguzo mbili: Kukanusha na kuthibitisha. Ukiulizwa: Ni zipi nguzo za laa illaaha illa Allaah, utasema nini? Utasema ni kukanusha na kuthibitisha. Hizi ndio nguzo za laa ilaaha illa Allaah.
Sharti zake ni saba.
Laa ilaaha illa Allaah haikunufaishi isipokuwa kwa sharti hizi saba:
1.    Elimu
Elimu kinyume chake ni ujinga wa kutoijua maana ya laa ilaaha illa Allaah. Yule mwenye kuitamka kwa ulimi lakini hajui maana yake, huyu haitomfaa laa ilaaha illa Allaah. Hii ni sharti ya kwanza mtu ajue maana yake.
2.    Yakini
Uwe na yakini. Yaani usiwe na shaka. Baadhi ya watu wanaweza kuwa wanajua lakini wana shaka kwa ujuzi huu. Ni lazima uwe na yakini. Yakini ya kwamba hakuna apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah na kwamba ni haki.
3.    Ikhlaasw
Kuwa na Ikhlaasw, na kinyume chake ni Shirki. Baadhi ya watu wanasema laa ilaaha illa Allaah lakini hawaachi Shirki. Na ndio yanayofanywa leo na waabudu makaburi. Hawa haitowafaa kitu laa ilaaha illa Allaah. Kwa kuwa katika sharti zake (laa ilaaha illa Allaah) ni kuacha Shirki.
4.    Ukweli
Ukweli na kinyume chake ni uongo. Kwa kuwa wanafiki wanasema laa ilaaha illa Allaah lakini wanadanganya moyoni mwao hawaitakidi maana yake.
قَالُوا نَشْهَدُ إِنَّكَ لَرَسُولُ اللَّـهِ ۗ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ إِنَّكَ لَرَسُولُهُ وَاللَّـهُ يَشْهَدُ إِنَّ الْمُنَافِقِينَ لَكَاذِبُونَ
 
 “Wanafiki wakisema: “Tunashuhudia kwamba wewe bila shaka ni Mtume wa Allaah.” Na Allaah Anajua (vyema) kuwa hakika wewe ni Mtume Wake, na Allaah Anashuhudia kuwa hakika wanafiki bila shaka ni waongo.” (63:01)

5.    Mapenzi
Unatakiwa kuipenda kalima hii na watu wake (wanaoitamka). Uwapende. Ama yule ambaye haipendi au hawapendi watu wake (wanaoitamka), huyu haitomfaa.
6.    Kunyenyekea
Kunyenyekea. Kunyenyekea kwa yale yanayotolewa dalili katika kumuabudu Allaah Pekee Asiyekuwa na mshirika na kutekeleza amri Zake. Maadamu umekubali na kushahidilia ya kwamba hapana mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah, basi ni lazima unyenyekee Ahkaam Zake na Dini Yake. Ama kutamka laa ilaaha illa Allaah lakini hunyenyekei Ahkaam za Shari´ah ya Allaah, haitokufaa kitu laa ilaaha illa Allaah.
7.    Kuikubali
Kuikubali, kutokataa kwa kurudisha kitu. Usirudishe kitu katika haki za laa ilaaha illa Allaah na yanayotolewa dalili kwayo, bali ukubali kila kinachotolewa dalili na laa ilaaha illa Allaah. Ukikubali.
- Na kuna sharti ya nane imeongezwa, kujiweka mbali na Shirki. Mtu hawi mpwekeshaji mpaka ajiweke mbali na Shirki.
وَإِذْ قَالَ إِبْرَاهِيمُ لِأَبِيهِ وَقَوْمِهِ إِنَّنِي بَرَاءٌ مِّمَّا تَعْبُدُونَ
”Na (taja ee  Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم pale ) Ibraahiym alipomwambia baba yake na watu wake: “Hakika mimi najitoa dhima (sina jukumu) na yale mnayoyaabudu.” (43:26)
Hizi ndio sharti nane za laa ilaaha illa Allaah.


Na dalili ya kushuhudia kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah ni kauli Yake Ta´ala:
لَقَدْ جَاءَكُمْ رَسُولٌ مِّنْ أَنفُسِكُمْ عَزِيزٌ عَلَيْهِ مَا عَنِتُّمْ حَرِيصٌ عَلَيْكُم بِالْمُؤْمِنِينَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ
”Kwa yakini amekujieni Mtume anayetokana na nyinyi wenyewe, ni magumu juu yake (yanamhuzunisha) yanayokutaabisheni, anakuhangaikieni (kwa kukujalini), mwenye huruma (na mwenye mapenzi) kwa Waumini, na mwenye rahmah.” (09:128)

Na maana ya kushuhudia kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, ni kumtii aliyoyaamrisha, na kumsadikisha aliyojulisha, na kujiepusha na aliyoyakataza na  aloyatahadharisha, na kwamba Allaah asiabudiwe isipokuwa kwa kufuata  yale (yeye Mtume)  aliyoyawekea Shari´ah (aliyotumwa nayo na Allaah).


Hivi sasa anaenda katika “ash-Hadu anna Muhammad Rasuulu Allaah”, kwa kuwa nguzo ya kwanza ina mambo mawili: “Kushahidilia ya kwamba hapana mola apasaye kuabudiwa kwa haki ila Allaah”, na hii tumeimaliza. Kitu cha pili ni “kushahidilia ya kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah”, ni nguzo moja. Sehemu ya kwanza ni kuwa na Ikhlaasw katika ´Ibaadah, na sehemu ya pili ni al-Mutaaba´ah kumfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Mtume ambaye ni jinsi moja na nyinyi amewajia; amewajia wanaadamu na majini wote mawili. Kushahidilia ya kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ina maana na muqtadhwa yake pamoja. Sio matamshi yanayosemwa tu. Maana yake ni ujue (ukiri) kwa ulimi wako na moyo wako ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ushahidilie hilo kwa ulimi wako na uitakidi hilo kwa moyo wako ya kwamba ni Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hii ndio maana ya ash-Hadu anna Muhammad Rasuulu Allaah. Ama kutamka kwa ulimi na kupinga hilo kwa moyo, hii ni katika njia ya wanafiki.
Na pia haitoshi kukiri moyoni ya kwamba ni Mtume wa Allaah, ni lazima kutamka kwa ulimi. Isitoshe, haitoshi kutamka hilo kwa ulimi na kukiri hilo moyoni, bali ni lazima kuje jambo la tatu nalo ni al-Ittiba´ah. Anasema (Ta´ala):
فَالَّذِينَ آمَنُوا بِهِ وَعَزَّرُوهُ وَنَصَرُوهُ وَاتَّبَعُوا النُّورَ الَّذِي أُنزِلَ مَعَهُ ۙأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ
”Basi wale waliomwamini na wakamtukuza, na wakamsaidia na wakafuata Nuru (Qur-aan) ambao imeteremshwa pamoja naye; hao ndio wenye kufaulu.” (07:157)
Hivyo ni lazima kumfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Anasema:
مَّن يُطِعِ الرَّسُولَ فَقَدْ أَطَاعَ اللَّـهَ
Atakayemtii Mtume basi kwa yakini amemtii Allaah.” (04:80)

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن رَّسُولٍ إِلَّا لِيُطَاعَ بِإِذْنِ اللَّـهِ
”Na Hatukutuma Mtume yeyote ila atiiwe kwa idhini ya Allaah.” (04:64)

 وَأَطِيعُوا اللَّـهَ وَالرَّسُولَ
”Na mtiini Allaah na Mtume.” (03:132)

Kafanya kumtii Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kumtii Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala). Na Kafanya kumuasi Mtume ni Kumuasi Yeye.
وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَيَتَعَدَّ حُدُودَهُ يُدْخِلْهُ نَارًا خَالِدًا فِيهَا وَلَهُ عَذَابٌ مُّهِينٌ
”Na yeyote atakayemuasi Allaah na Mtume Wake na akapindukia mipaka Yake Atamuingiza Motoni adumu humo milele na atapata adhabu inayodhalilisha.” (04:14)

وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَإِنَّ لَهُ نَارَ جَهَنَّمَ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا
 
”Na yeyote yule atakayemwasi Allaah na Mtume Wake, basi hakika atapata Moto wa Jahannam wadumu humo milele.” (72:23)
وَإِن تُطِيعُوهُ تَهْتَدُوا
”Na mkimtii Mtume wa Allaah mtaongoka.” (24:54)

وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ
 
”Na mtiini Mtume ili mpate kurehemewa.” (24:56)

فَإِن لَّمْ يَسْتَجِيبُوا لَكَ فَاعْلَمْ أَنَّمَا يَتَّبِعُونَ أَهْوَاءَهُمْ ۚ وَمَنْ أَضَلُّ مِمَّنِ اتَّبَعَ هَوَاهُ بِغَيْرِ هُدًى مِّنَ اللَّـهِ
 
”Na wasipokuitikia (kukuletea Kitabu au kuamini ujumbe wako), basi elewa kwamba hakika wanafuata matamanio yao. Na nani mpotofu zaidi kuliko yule aliyefuata matamanio yake bila ya Hidaayah kutoka kwa Allaah?.” (28:50)
Hivyo ni lazima kumtii (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Yule ambaye anakiri kuwa ni Mtume wa Allaah, ni lazima amtii kwa aliyoyaamrisha.
وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا
“Na lolote (lile) analokupeni Mtume (Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) basi lichukueni, na (lolote lile) analokukatazeni, basi acheni.” (59:07)
فَلْيَحْذَرِ الَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنْ أَمْرِهِ أَن تُصِيبَهُمْ فِتْنَةٌ أَوْ يُصِيبَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ
“Basi watahadhari wale wanaokhalifu amri yake, isije kuwasibu fitnah au ikawasibu adhabu iumizayo.” (24:63)
Ni lazima kumtii Mtume (´alayhis-Swalaat was-Salaam).
“Kumsadikisha aliyoelezea”, Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kaelezea mambo mengi ya Ghayb, kaelezea kutoka kwa Allaah na kaelezea mambo yatakayokuja huko mbele; kama kusimama kwa Qiyaamah, alama za Qiyaamah, Pepo, Moto. Na kaelezea mambo yaliyopita, hali za Ummah zilizotangulia. Ni lazima kumsadikisha kwa aliyoelezea. Kwa kuwa ni ya ukweli yasiyokuwa na uongo ndani yake. Anasema (Ta´ala):
وَمَا يَنطِقُ عَنِ الْهَوَىٰ إِنْ هُوَ إِلَّا وَحْيٌ يُوحَىٰ
 
”Na wala hatamki kwa matamanio (yake). Hayo (ayasemayo) si chochote isipokuwa ni Wahy unaofunuliwa (kwake).” (53:03-04)
Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) haelezei khabari kutoka kwake, bali anaongea kwa Wahyi kutoka kwa Allaah (´Azza wa Jalla). Maelezo yake ni ya kweli (´alayhis-Salaam). Na yule asiyemsadikisha kwa aliyoelezea huyo sio muumini na wala sio mkweli katika Shahaadah yake ya kwamba ni Mtume wa Allaah. Vipi atashahidilia ya kwamba ni Mtume wa Allaah kisha amkadhibishe kwa aliyoyaeleza? Vipi atashahidilia ya kwamba ni Mtume wa Allaah na asitii amri zake? Hivyo kutakuwa hakuna faida ya Shahaadah.
“Kujiepusha aliyoyakataza na  aloyatahadharisha”, kakukataza maneno, vitendo na mambo mengi. Na wala hakatazi Mtume isipokuwa kwa kitu chenye madhara na shari. Na wala haamrishi isipokuwa kwa kitu kilicho na kheri. Ikiwa mtu hajiepushi na aliyoyakataza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), atakuwa hakumshahidilia Risaalah. Haya ni mambo yanagongana. Vipi mtu atashahidilia ya kwamba ni Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wala hajiepushi na aliyokataza Mtume.
وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا
“Na lolote (lile) analokupeni Mtume (Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) basi lichukueni, na (lolote lile) analokukatazeni, basi acheni.” (59:07)
Anasema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):
“Yale niliyowakataza, basi jiepusheni nayo. Na yale niliyowaamrisha, yafanyeni kadiri muwezavyo.”
Hivyo ni lazima kujiepushe na aliyoyakaza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).
“Allaah asiabudiwe isipokuwa kwa kufuata  yale aliyoyawekea Shari´ah”, asilete ´Ibaadah ambazo hazikuweka Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hata kama makusudio yake yatakuwa mazuri, hata kama atakuwa anataka ujira, lakini hichi ni kitendo cha batili hakikuleta Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Nia haitoshelezi, lazima kuwepo al-Ittibaa´ah. ´Ibaadah ni Tawqiyfiyyah, haijuzu kuleta ´Ibaadah ambazo hazikuleta Mtume wa Allaah. Anasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):
“Atakayefanya ´amali isiyokuwemo humo amri yetu, basi atarudishiwa”
Na kasema:
“Shikamaneni na Sunnah zangu na Sunnah za Makhalifah wangu waongofu. Ziumeni kwa magego yenu. Na tahadharini na mambo ya kuzua. Hakika kila kitakachozushwa ni upotofu, na kila upotofu ni Motoni.”
Kuleta ´Ibaadah ambazo hazikuweka Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), huzingatiwa ni Bid´ah munkari zilizokatazwa. Hata kama zimejuzisha fulani na fulani, au zimefanya mtu fulani, maadamu hazikuleta (kuweka) Mtume ni Bid´ah na upotofu. Bid´ah, mambo ya kuzua na ukhurafi, yote haya ni mambo ya batili, kasoro na upotofu kwa yule aliyezileta. Hata kama anakusudia kheri na anataka ujira, ibra sio makusudio bali ibra ni al-Ittibaa´ah, utiifu na kunyenyekea.
Mwenye kuzusha hakushahidilia ya kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), mwenye kuzusha kitu na kwenda kinyume na aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), hii ni dalili inaonesha ya kwamba hakushahidilia Shahaadah ya kihakika. Yule ambaye anashahidilia Shahaadah ya kihakika basi anyenyekee kwa yale aliyoyawekea Shari´ah (Mtume) na wala asizue kitu kutoka kwake au akafuata kitu kilichozushwa na waliotangulia. Hii ndio maana ya ash-Hadu anna Muhammad Rasuulu Allaah. Sio matamshi yanayotamkwa ulimini peke yake.


Na dalili ya Swalah na Zakaah na tafsiri ya At-Tawhiyd ni kauli Yake Ta´ala:
وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ وَيُقِيمُوا الصَّلَاةَ وَيُؤْتُوا الزَّكَاةَ ۚ وَذَٰلِكَ دِينُ الْقَيِّمَةِ
 
”Na hawakuamrishwa (chochote kile) isipokuwa wamwabudu Allaah wakiwa wenye kumtakasia Dini, Hunafaa (wakielemea haki na kujiengua na upotofu) na wasimamishe Swalaah na watoe Zakaah; na hiyo ndiyo Dini iliyosimama imara.” (98:05)


Dalili ya Swalah na Zakaah ni Kauli ya Allaah:
وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ وَيُقِيمُوا الصَّلَاةَ وَيُؤْتُوا الزَّكَاةَ ۚ وَذَٰلِكَ دِينُ الْقَيِّمَةِ
 
”Na hawakuamrishwa (chochote kile) isipokuwa wamwabudu Allaah wakiwa wenye kumtakasia Dini, Hunafaa (wakielemea haki na kujiengua na upotofu) na wasimamishe Swalaah na watoe Zakaah; na hiyo ndiyo Dini iliyosimama imara.” (98:05)
Swalah ni kuisimamisha kama Alivyoamrisha Allaah (Jalla wa ´Alaa); kwa sharti zake, nguzo zake na wajibu wake. Ama kujisalia tu haitoshi. Ndio maana Allaah Hakusema: “Na waswali”, bali Kasema: “Wasimamishe Swalah”. Na Swalah haiwi ni yenye kusimama isipokuwa itapoletwa kama Alivyoiamrisha Allaah; kwa sharti zake, nguzo zake na wajibu wake. Ama yule mwenye kujiswalia tu kwa wakati autakao, au bila ya Twahaarah, bila ya utulivu na kadhalika huyu hakusimamisha Swalah. Na ndio maana Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwambia mtu yule aliyeswali kimakosa Swalah yake, akamwambia: “Rudi ukaswali, kwani kwa hakika hujaswali.”
Na watoe Zakaah yaani waitoe kuwapa wale wenye kustahiki. Ambao Allaah (Ta´ala) Kawaweka wazi katika Kauli Yake:
إِنَّمَا الصَّدَقَاتُ لِلْفُقَرَاءِ وَالْمَسَاكِينِ وَالْعَامِلِينَ عَلَيْهَا وَالْمُؤَلَّفَةِ قُلُوبُهُمْ وَفِي الرِّقَابِ وَالْغَارِمِينَ وَفِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَابْنِ السَّبِيلِ ۖ فَرِيضَةً مِّنَ اللَّـهِ
”Hakika Swadaqah (Zakaah) ni kwa ajili ya mafakiri na masikini na wanaozitumikia, na wanaotiwa nguvu nyoyo zao (katika Uislamu) na kuwakomboa watumwa, na (kuwasaidia) wenye deni na katika fiy-SabiliLlaah(Njia zote za kutengeneza mambo Aliyoyaamrisha Allaah), na msafiri (aliyeharibikiwa). Ni faradhi itokayo kwa Allaah.” (09:60)
Haijuzu kuwapa watu wasiokuwa hawa. Atakayetoa kuwapa wasiokuwa watu hawa hiyo haitokuwa Zakaah hata ikiwa ni milioni na biliari ya mapesa. Isitoshe itolewe kwa wakati wake, isitolewe kwa kuchelewa au kwa uzembe na mfano wa hayo.


Na dalili ya Swawm ni kauli Yake Ta´ala:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ
”Enyi mlioamini! Mmeandikiwa Swawm kama ilivyoandikwa kwa wale ambao wa kabla yenu mpate kuwa na taqwa.” (02:183)


Dalili ya Hajj ni Kauli Yake Ta´ala:
وَلِلَّـهِ عَلَى النَّاسِ حِجُّ الْبَيْتِ مَنِ اسْتَطَاعَ إِلَيْهِ سَبِيلًا ۚ وَمَن كَفَرَ فَإِنَّ اللَّـهَ غَنِيٌّ عَنِ الْعَالَمِينَ
”Na kwa ajili ya Allaah ni wajibu kwa watu watekeleze Hajj katika Nyumba hiyo kwa mwenye uwezo. Na atakayekanusha, basi hakika Allaah ni Ghaniyy (Mkwasi) kwa walimwengu.” (03:97)


“Nyumba” ni Ka´abah. “Kwa mwenye uwezo” hii ni sharti ya uwajibu; yule mwenye kuweza kimwili na uwezo wa kimali.  Kimwili awe anaweza kutembea, kurukuu, kutoka katika mji wake mpaka Makkah, huu ni uwezo wa kimwili. Yule ambaye ana maradhi yasiyotarajiwa kupona na ni mzee sana, hawa hawana uwezo wa kimwili, wakiwa na uwezo wa kimali basi wataweka mtu awezae kuwahijia.
“Na atakayekufuru (kanusha)”, yule atakayekataa kuhiji ilihali ana uwezo, basi ni kafiri. Kwa kuwa Allaah (Ta´ala) Kasema:
“Na atakayekufuru (kanusha)”, yaani mwenye kukataa naye ana uwezo wa kuhiji hii ni kufuru; inaweza kuwa kufuru kubwa na inaweza kuwa kufuru ndogo. Atakayekataa kwa kupinga uwajibu wake, hii ni kufuru kubwa kwa Ijmaa´ ya Waislamu. Ama yule mwenye kukubali uwajibu wake lakini na akaiacha kwa kuzembea (uvivu), hii ni kufuru ndogo. Katika Aayah hii kuna dalili ya kuhiji.


Daraja Ya Pili: Iymaan
Nayo  ((Ina tanzu  [matawi] sabini na kitu. Ya juu yake ni kauli ya “laa ilaaha illaAllaah” [hapana apasaye kuabudiwa kwa haki ila Allaah], na ya chini yake kabisa ni kuondosha uchafu njiani. Na kuona hayaa ni utanzu [tawi] katika tanzu za imani)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

Tumemaliza daraja ya kwanza ambayo ni Uislamu. Daraja ya pili – nayo ni ya juu – ni ya Imani. Na Imani iko juu kuliko Uislamu, kila muumini ni Muislamu, na si kila Muislamu ni muumini. Imani kilugha ni kusadikisha. Anasema (Ta´ala):
وَمَا أَنتَ بِمُؤْمِنٍ لَّنَا وَلَوْ كُنَّا صَادِقِينَ
”Nawe hutotuamini japo tukiwa ni  wakweli.” (12:17)
yaani si mwenye kutusadikisha. Hivyo Imani kilugha ni kusadikisha.
Ama Imani Kishari´ah, ni kama walivyoifasiri Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah:
“Ni kutamka kwa ulimi, kuamini moyoni na matendo ya viungo vya mwili; inazidi kwa utiifu na inapungua kwa kufanya maasi.”
Hii ndio maana ya Imani [Kishari´ah] kwa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah.
Imani na Uislamu vikitajwa vyote viwili, kila kimoja kinakuwa na maana yake. Na kikitajwa kimoja, kinaingia kimoja kwenye kingine. Vikitajwa vyote, Uislamu unafasiriwa kwa matendo ya dhahiri ambayo ni zile nguzo tano za Uislamu, na Imani inafasiriwa kwa matendo ya ndani ambayo ni zile nguzo sita (za Imani). Na ni lazima mtu awe Muislamu muumini, aamini nguzo tano za Uislamu na nguzo sita za Imani.
“Ya juu yake ni kauli ya “laa ilaaha illa Allaah” hii ni dalili kuwa kauli (kutamka) ni katika Imani. “... ya chini yake ni kuondosha uchafu njiani” hii ni dalili ya kwamba kuondosha uchafu ni katika Imani. “... kuona hayaa ni tawi katika Imani” hii ni ´amali ya moyoni. Hii ni dalili ya kwamba Imani ni kutamka kwa ulimi, kuamini moyoni na matendo ya viungo.
Imani ina nguzo zake, ikitoweka moja ya nguzo Imani inaondoka. Kwa kuwa hakuna kitu kinachosimama isipokuwa juu ya nguzo zake. Ama matawi ni yenye kukamilisha, Imani haiondoki kwa kutoweka kitu katika Imani ambacho ni chenye kukamilisha. Chenye kukamilisha, ima cha wajibu au mustahaba. Mtu akiacha kitu katika mambo ya wajibu au akafanya kitu katika mambo ya haramu, Imani haindoki yote kwa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah, lakini kinachoondoka ni Imani yake kutokuwa kamili na mtu huyu anakuwa ni mwenye Imani pungufu, au muumini Faasiq. Kwa mfano mtu akanywa pombe, akaiba, au akazini au akafanya kitu katika madhambi makubwa, huyu anakuwa kafanya dhambi kubwa katika madhambi makubwa. Lakini hakufuru kwa hilo na wala si kwamba hana Imani kabisa, bali Imani yake inakuwa pungufu na anaitwa Faasiq. Na atasimamishiwa hadd (adhabu) ikiwa ni maasi yanayohitajia hadd (adhabu).
Hali kadhalika atakayeacha wajibu; kama kuacha kuwatendea wema wazazi, kuunga jamaa wa karibu, haya ni katika mambo ya wajibu. Mwenye kuacha haya Imani yake inakuwa pungufu na anakuwa ni muasi kwa kuacha jambo la wajibu na anakuwa muasi ima kwa kuacha jambo la wajibu au kwa kufanya jambo la haramu. Kwa vovyote ni kwamba mtu huyu hatoki katika Imani (Uislamu). Haya ndio madhehebu ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah tofauti na Khawaarij na Mu´tazilah ambao wanawakufurisha wenye kufanya madhambi makubwa. Khawaarij  wanamkufurisha na kumtoa katika Dini. Ama Mu´tazilah wanamtoa katika Dini lakini hawamhukumu ukafiri, isipokuwa tu wanamuweka katika manzilah baina ya manzilah mbili: Sio muumini na wala sio kafiri. Ama Khawaarij wanasema kuwa ni kafiri katoka katika Imani na kuingia kwenye kufuru. Haya ndio madhehebu yao na ni madhehebu yaliyozushwa na yanakhalifu dalili na yanakhalifu waliyomo Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah.
Mwenye kuacha kitu katika nguzo anakufuru. Mwenye kukanusha Tawhiyd na akamshirikisha Allaah (´Azza wa Jalla) huyu anakufuru kwa kuwa hakuamuamini Allaah (´Azza wa Jalla). Mwenye kupinga Mtume mmoja, Risaalah ya Mtume katika Mitume (´alayhimus-Salaam) anakufuru kwa kuwa kaacha nguzo. Hali kadhalika nguzo zilizobakia. Mwenye kupinga kuwepo kwa Malaika anakufuru na kutoka katika Dini. Mwenye kupinga kufufuliwa, au akakanusha Pepo au Moto, Swiraat, Mizaan, au kitu katika yaliyothibiti kwa hilo anakufuru. Kwa kuwa kapinga nguzo katika nguzo za Imani. Hali kadhalika mwenye kupinga Qadar, akasema hakuna Qadar na wala asisadikishe (asikubali) kuwa ni Qadar kutoka kwa Allaah (´Azza wa Jalla) na kusema mambo yanajitokea yenyewe tu na wala hakuna Qadar – kama wanavyosema Mu´tazilah – anakufuru pia. Kwa kuwa kapinga Qadar. Ama mwenye kuacha kitu katika matawi, huyu Imani yake inapungua [tu], kupungua huku inakuwa ima kwa kuacha jambo la wajibu au kufanya jambo la haramu, lakini hakufuru kwa hilo.
Na dalili ya kwamba Imani inazidi na kupungua ni kauli Yake (Ta´la):
إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ إِذَا ذُكِرَ اللَّـهُ وَجِلَتْ قُلُوبُهُمْ وَإِذَا تُلِيَتْ عَلَيْهِمْ آيَاتُهُ زَادَتْهُمْ إِيمَانًا
”Hakika Waumini ni wale ambao anapotajwa Allaah nyoyo zao, zinajaa khofu (na hushtuka), na wanaposomewa Aayah Zake huwazidishia iymaan.” (08:02)
Ni dalili ioneshayo ya kwamba Imani inazidi. Na Kauli Yake (Ta´ala):
وَإِذَا أُنزِلَتْ سُورَةٌ أَنْ آمِنُوا بِاللَّـهِ وَجَاهِدُوا مَعَ رَسُولِهِ اسْتَأْذَنَكَ أُولُو الطَّوْلِ مِنْهُمْ وَقَالُوا ذَرْنَا نَكُن مَّعَ الْقَاعِدِينَ
”Na inapoteremka Suwrah (ya Qur-aan inayosema): “Muamimini Allaah, na fanyeni jihaad pamoja na Mtume Wake,” wanakuomba idhini wale (wanafiki) wenye wasaa miongoni mwao, na husema: “Tuache (tusiende vitani) tuwe pamoja na wanaokaa”.” (09:86)
Ni dalili ioneshayo pia ya kwamba Imani inazidi, kwa kuteremka Qur-aan, kusikiliza na kuizingatia. Na Kauli ya Allaah (Ta´ala):
وَمَا جَعَلْنَا أَصْحَابَ النَّارِ إِلَّا مَلَائِكَةً ۙ وَمَا جَعَلْنَا عِدَّتَهُمْ إِلَّا فِتْنَةً لِّلَّذِينَ كَفَرُوا لِيَسْتَيْقِنَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ وَيَزْدَادَ الَّذِينَ آمَنُوا إِيمَانًا
 
”Na Hatukuweka walinzi wa Moto isipokuwa ni Malaika, na Hatukuifanya idadi yao (hiyo ya kumi na tisa) isipokuwa iwe (ni) jaribio kwa wale waliokufuru; ili wayakinishe wale waliopewa Kitabu, na iwazidishie iymaan wale walioamini.” (74:31)
Ni dalili ioneshayo ya kwamba Imani inazidi kwa utiifu na kusadikisha.
Ama kupungua, kila kitu chenye kuzidi hupungua. Dalii ni kauli yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Hadiyth Swahiyh kwamba Allaah (Subhaanah) siku ya Qiyaamah Atasema:
“Mtoeni Motoni yule ambaye katika moyo wake kuna Imani sawa na mbegu ya haradali ya Imani”
Ni dalili ya kwamba Imani inapungua mpaka inakuwa kiasi cha (mbegu ya) haradali moyoni. Hali kadhalika Kauli Yake (Ta´ala):
 هُمْ لِلْكُفْرِ يَوْمَئِذٍ أَقْرَبُ مِنْهُمْ لِلْإِيمَانِ
Wao siku hiyo kwa ukafiri (walikuwa wako) karibu zaidi kuliko iymaan.” (03:167)
Ni dalili ya kwamba Imani inapungua mpaka inakuwa karibu na kufuru. Anasema tena Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):
“Yeyote yule atakayeona kitendo kiovu akiondoe (abadilishe) kwa mkono wake, ikiwa hawezi basi kwa ulimi wake (alikemee au kukataza), na ikiwa hawezi basi kwa moyo wake (achukie) na huo (yaani kuona baya na kunyamaza) ni udhaifu wa Imani.”
Ni dalili ya kwamba Imani inadhoofika, yaani inapungua. Kwa hivyo Imani inazidi kwa utiifu na inapungua kwa kufanya maasi.
 

Na nguzo zake ni sita kama katika Hadiyth: ((Ni kumwamini Allaah, na Malaika Wake, na Vitabu Vyake, na Mitume Yake na Siku ya Mwisho, na  kuamini Al-Qadr [makadirio] ya kheri na shari zake)) [Muslim]

Na dalili ya hizi nguzo sita hizi ni kauli Yake Ta´ala:
لَّيْسَ الْبِرَّ أَن تُوَلُّوا وُجُوهَكُمْ قِبَلَ الْمَشْرِقِ وَالْمَغْرِبِ وَلَـٰكِنَّ الْبِرَّ مَنْ آمَنَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ وَالْمَلَائِكَةِ وَالْكِتَابِ وَالنَّبِيِّينَ
”Si wema (pekee) kuwa mnaelekeza nyuso zenu upande wa Mashariki na Magharibi lakini wema (khasa) ni mwenye kuamini Allaah na Siku ya Mwisho na Malaika na Kitabu na Manabii.” (02:177)
Na dalili ya Al-Qadr (makadirio au kipimo) ni kauli ya Allaah:
إِنَّا كُلَّ شَيْءٍ خَلَقْنَاهُ بِقَدَرٍ
 
”Hakika sisi Tumekiumba kila kitu kwa makadirio.” (54:49)


Nguzo ya kwanza ni kumwamini Allaah, kunaingia vigawanyo vya Tawhiyd vitatu. Kuamini ya kwamba Allaah ni Mmoja Pekee, hana mshirika katika Rubuubiyyah Yake, wala hana mshirikina katika Ilaahiyyah ´Ibaadah Yake wala Majina na Sifa Zake. Huku ndio kumuamini Allaah (´Azza wa Jalla).
Nguzo ya pili ni kuamini Malaika. Na Malaika ni viumbe katika viumbe vya Allaah ambavyo viko Ghayb (havionekani). Allaah Kawaumba ili wamuabudu na watekeleze amri Zake  (Subhaanahu wa Ta´ala). Na wako aina mbali mbali, kila mmoja ana kazi yake Aliyopewa na anaifanya pasina kumuasi Allaah kabisa. Kuna ambao wamewakilishwa kwa Wahyi naye ni Jibriyl (´alayhis-Salaam) na ndio Malaika bora, na Ndiye Roho Mwaminifu Mwenye nguvu nyigni. Na kuna ambao wamewakilishwa kwa kubebe ´Arshi. Miongoni mwao (Malaika) kuko ambao wana mbawa sitini – kama Jibriyl (´alayhis-Salaam). Na kuna ambaye kawakilishwa kwa kazi ya kupuliza parapanda naye ni Israafiyl (´alayhis-Salaam). Na kuna ambao wamewakilishwa kwa kazi ya kutoa roho, naye ni Malakul-Mawt (Malaika wa kutoa roho), na yuko na wenzake katika Malaika. Na kuko ambao wamewakilishwa kupulizia watoto roho ndani ya matumbo ya mama zao. Na kuko ambao wamewakilishwa kuandika matendo ya wanaadamu, usiku na mchana. Na kuko ambao wamewakilishwa kumuhifadhi binaadamu, maadui, mabaya na mengineyo katika mambo ya khatari. Na yale yatakayomfika binaadamu ni yale Aliyomuandikia Allaah kukiwemo mauti. Na kuko Malaika ambao wanahudhuria vikao vinavyomdhukuru Allaah. Hakuna ajuae sifa na walivyo Malaika isipokuwa Allaah (Ta´ala). Lakini yaliyokuja katika nususi za Qur-aan au Hadiyth za Mtume Swahiyh tunazisadikisha na kuziamini. Na yale ambayo hatukutajiwa tunayanyamazia na wala hatuyafanyii utafiti. Kwa kuwa haya ni katika mambo ya Ghayb.
Kuamini Malaika ni nguzo katika nguzo za Uislamu. Mwenye kupinga kuwepo kwa Malaika, kama kusema “hakuna Malaika, hatuwaoni, maadamu hatuwaoni hivyo sio sahihi”, huyu ni kafiri Mulhid. Kwa kuwa hakuamini Ghayb.
Mtu hawezi kuwaona Malaika kwa sura zao za kihakika kutokana na maslahi kwa binaadamu, kwa kuwa hawezi hili kuwaona kwa umbile (sura) Alilowaumba kwalo Allaah. Bali mtu anaweza kuwaona kwa sura ya mtu binaadamu. Na wala mtu hawezi kuwaona kwa sura yao ya kihakika isipokuwa tu wakati wa adhabu:
يَوْمَ يَرَوْنَ الْمَلَائِكَةَ لَا بُشْرَىٰ يَوْمَئِذٍ لِّلْمُجْرِمِينَ وَيَقُولُونَ حِجْرًا مَّحْجُورًا
 
”Siku watakayowaona Malaika hakutakuwa na furaha Siku hiyo kwa wakhalifu (makafiri, washirikina, watendao madhambi); na (Malaika) watasema: “Kizuizi kimepigwa marufuku..” (25:22)
Na wakati wa mauti, mtu atawaona Malaika wa mauti. Lakini duniani wakati wa uhai mtu hawezi kuwaona.
Allaah (Ta´ala) Kawaumba Malaika kutokana na nuru. Na Kawaumba Mashaytwaan kutokana na moto. Na kamuumba binaadamu kwa udongo. Na Allaah ni Muweza wa kila kitu.
Nguzo ya tatu ni kuamini vitabu ambavyo Allaah Kaviteremsha kwa Mitume Wake (´alayhimus-Salaam) kutokana na Hidaayah ya mtu. Tunaviamini, sawa vile ambavyo Allaah Katutajia na vile ambavyo Hakututajia. Miongoni mwa ambavyo Allaah Katutajia ni pamoja na Tawrat, Injiyl, Zabuur, Qur-aan Tukufu, Suhuf Ibraahiym. Tunaviamini. Na tunaamini vile ambavyo Allaah Hakututajia.
Imani (kuamini) vitabu vya kale ni Imani ya ujumla, na Imani (ya kuamini) Qur-aan ni Imani al-Mufaswswal ufafanuzi kwa kila kilichomo. Ni Kitabu chetu alichoteremshiwa Mtume wetu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Yule ambaye atakanusha Aayah moja humo au herufi, atakayekanusha herufi moja tu katika herufi zake huyo ni kafiri karitadi kutoka katika Uislamu. Hali kadhalika yule ambaye ataamini baadhi [ya sehemu ya] Qur-aan na akaamini baadhi [ya sehemu yake nyingine] huyo ni kafiri. Hali kadhalika yule atakayeamini baadhi ya vitabu na akakufuru baadhi, huyo ni kafiri. Atakayesema “mimi naamini Qur-aan na wala siamini Tawrat na Injiyl” ni kafiri. Au akasema “naamini Tawrat na Injiyl na wala siamini Zabuur aliyoteremshiwa Daawuud (´alayhis-Salaam)”, ni kafiri. Au akapinga Suhuf Ibraahiym ni kafiri. Kwa kuwa anamkadhibisha Allaah (´Azza wa Jalla) na anawakadhibisha Mitume, huyo ni kafiri. Kwa kuwa kapinga nguzo katika nguzo za Imani. Imani ya kuamini Mitume wote (´alayhimus-Salaam), kuanzia wa mwanzo wao mpaka wa mwisho wao, wale Aliyowataja Allaah na wale ambao Hakuwataja tunawaamini wote na kwamba ni Mitume wa Allaah wa haki, wamekuja na Risaalah na wakaifikisha kwa Ummah wao. Yule ambaye atamkufuru Mtume mmoja, basi kawakufuru wote.
إِنَّ الَّذِينَ يَكْفُرُونَ بِاللَّـهِ وَرُسُلِهِ وَيُرِيدُونَ أَن يُفَرِّقُوا بَيْنَ اللَّـهِ وَرُسُلِهِ وَيَقُولُونَ نُؤْمِنُ بِبَعْضٍ وَنَكْفُرُ بِبَعْضٍ وَيُرِيدُونَ أَن يَتَّخِذُوا بَيْنَ ذَٰلِكَ سَبِيلًا أُولَـٰئِكَ هُمُ الْكَافِرُونَ حَقًّا ۚ وَأَعْتَدْنَا لِلْكَافِرِينَ عَذَابًا مُّهِينًا وَالَّذِينَ آمَنُوا بِاللَّـهِ وَرُسُلِهِ وَلَمْ يُفَرِّقُوا بَيْنَ أَحَدٍ مِّنْهُمْ أُولَـٰئِكَ سَوْفَ يُؤْتِيهِمْ أُجُورَهُمْ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا
”Hakika wale waliomkanusha Allaah na Mitume Yake; na wanataka kufarikisha baina ya Allaah na Mitume Yake; na wanasema:  “Tunaamini baadhi na tunawakanusha baadhi”; na wanataka kuchukua njia iliyo baina (kati kati) ya hayo. Hao ndio makafiri wa kweli. Na Tumewaandalia makafiri adhabu ya kudhalilisha. Na wale waliomwamini Allaah na Mitume Yake na hawakumfarikisha yeyote baina yao; hao Atawapa ujira wao. Na Allaah ni Ghafuwrar-Rahiymaa (Mwingi wa kughufiria - Mwenye kurehemu).” (04:150-152)
Kumkufuru Mtume mmoja au Nabii mmoja ni kuwakufuru wote. Na kwa hili Kasema:
كَذَّبَتْ قَوْمُ نُوحٍ الْمُرْسَلِينَ
 
“Watu wa Nuwh walikadhibisha Mitume.” (25:105)
Pamoja na kuwa walimkanusha Nuuh (peke yake), kumkanusha kwao Nuuh ni kuwakanusha baki ya Mitume wengine wote. Hali kadhalika atakayemkadhibisha ´Iysa - kama mayahudi, au kumkadhibisha ´Iysa na Muhammad - kama mayahudi, au kumkadhibisha Muhammad basi mtu huyo anakuwa kawakadhibisha wote. Mayahudi na manaswara wanawakubali Mitume (´alayhimus-Swalaat was-Salaam) isipokuwa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mayahudi wanamkadhibisha pia ´Iysa. Hivyo atakayemkadhibisha mmoja basi kawakadhibisha wote. Kwa hivyo ni lazima kuwaamini Mitume wote (´alayhimus-Swalaat was-Salaam), sawa wale ambao Allaah Katutajia na wale ambao Hakututajia.
Nguzo ya tano ni Imani ya kuamini siku ya Mwisho, nayo ni nguzo ya tano. Yawm-ul-Aakhirah siku ya mwisho makusudio ni siku ya Qiyaamah. Imeitwa ni siku ya mwisho kwa kuwa dunia ndio siku ya kwanza na Qiyaamah ndio siku ya mwisho. Imani kuamini siku ya Mwisho yaani maana yake ni Imani kuamini yaliyo baada ya mauti, na si kwamba ni Imani kuamini yaliyo baada ya kufufuliwa, hapana. Ni Imani kuamini yaliyo baada ya mauti ndio inaanza; adhabu ya ndani ya kaburi, neema zake, maswali ya Malaika wawili kwenye kaburi, yote haya ni katika Imani kuamini siku ya Mwisho. Kisha kuamini kufufuliwa, kisimamo kwenye kiwanja, hesabu, kupimwa kwa ´amali, madaftari ya ´amali, Swiraat, Mizaan, Pepo, Moto na mengine yote yatakayopitika siku ya Qiyaamah tunayaamini kwa ujumla na kwa ufafanuzi. Kuanzia wakati wa mauti mpaka watakapoingia watu wa Pepo Peponi na watu wa Moto Motoni. Yote haya tunayaamini na wala hatushuku kitu katika hayo. Yule ambaye atashuku kitu katika hayo ni kafiri karitadi kutoka katika Uislamu.
Nguzo ya sita ni kuamini Qadar; kheri na shari yake. Tunaamini ya kwamba yanayopitika katika ulimwengu huu ya kheri na shari, ya kufuru na Imani, ya neema na yasiyokuwa neema, raha na shida, maradhi na afya, uhai na mauti, yote yanayopitika katika ulimwengu huu ni kwa Qadhwaa na Qadar ya Allaah. Na kwamba yaliyokufika hayakuwa yakukukosa, na yaliyokukosa hayakuwa yakukufika, haya ni kwa Qadhwaa na Qadar ya Allaah.  Anasema (Ta´ala):
مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي أَنفُسِكُمْ إِلَّا فِي كِتَابٍ مِّن قَبْلِ أَن نَّبْرَأَهَا ۚ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ
 
”Hakuna msiba wowote unaokusibuni katika ardhi au katika nafsi zenu isipokuwa umo katika Kitabu (Lawhum-Mahfuudhw) kabla Hatujauumba (huo msiba). Hakika hayo kwa Allaah ni sahali.” (57:22)
Hii ndio Imani ya kuamini Qadar. Na Imani ya kuamini Qadar kunajumuisha mambo haya manne. Yule ambaye haamini haya manne sio mwenye kuamini Qadar.
1.     (Elimu) Imani ya kuamini ya kwamba Allaah Alijua kila kitu. Yaliyoko na yatakayokuweko. Alijua yaliyoko kabla ya kuweko na kupitika, Aliyajua kwa Elimu Yake kuu. Atakayepinga hili ni kafiri.
 
2.    (Kuandikwa) Yameandikwa kwenye Lawh al-Mahfuudh. Ya kwamba Allaah Kaandika kila kitu katika Lawh al-Mahfuudh. Hapapitiki kitu isipokuwa tayari kimeshaandikwa kwenye Lawh al-Mahfuudh. Hakuna kitu kinachopitika (katika ulimwengu huu) na hakipo Lawh al-Mahfuudh. Allaah Kaandika kwenye Lawh al-Mahfuudh makadirio ya kila    kitu.

Kitu cha kwanza Alichoumba Allaah ni kamalu, Akaiambiwa: “Andika”. Ikasema: “Niandike nini?” Akasema: “Andika yatakayokuwepo mpaka siku ya Qiyaamah.”

Yote yameandikwa kwenye Lawh al-Mahfuudh. Atakayekanusha hili akasema “Allaah Anajua kila kitu lakini hayakuandikwa kwenye Lawh al-Mahfuudh”, huyu ni kafiri karitadi katika Dini ya Kiislamu.

3.    (Utashi) Utashi wa Allaah unaoendelea. Ya kwamba Allaah Hutaka vitu [na hutokea], hakuna kitu kinachotokea isipokuwa Allaah Kishakitaka [kitokee] kama jinsi kilivyo kwenye Lawh al-Mahfuudh na kama Alivyokijua (Subhaanahu wa Ta´ala). Hutaka kila kitu kwa wakati wake. Hakikupitika bila ya Matakwa na Utashi wa Allaah. Mwenye kusema mambo yanapitika bila ya Allaah Kutaka, huyu ni kafiri.

4.    (Umbaji) Uumbaji. Allaah Ndiye Muumba wa kila kitu, Kaumba Alivyotaka (Subhaanahu wa Ta´ala). Na kila kitu kimeumbwa na Allaah (´Azza wa Jalla).
Hizi daraja nne ni lazima kuziamini, la sivyo mtu anakuwa haamini Qadar. Yote haya ni lazima kuyaamini. Mwenye kupinga kitu katika hayo anakuwa ni kafiri katika Dini ya Uislamu. Kwa kuwa kapinga nguzo katika nguzo za Imani.


Daraja Ya Tatu: Ihsaan.
Nguzo yake ni moja kama katika Hadiyth: ((Umwabudu Allaah kama kwamba unamuona, na hata kama humuoni, basi Yeye Anakuona)) [Muslim]
Na dalili ni kauli Yake Ta´ala:
إِنَّ اللَّـهَ مَعَ الَّذِينَ اتَّقَوا وَّالَّذِينَ هُم مُّحْسِنُونَ
”Hakika Allaah Yu Pamoja na wenye taqwa, na wale ambao wao ni wema.” (16:128)

Na kauli Yake Ta´ala:

وَتَوَكَّلْ عَلَى الْعَزِيزِ الرَّحِيمِ الَّذِي يَرَاكَ حِينَ تَقُومُ وَتَقَلُّبَكَ فِي السَّاجِدِينَ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ 
 
”Na tawakali kwa Al-’Aziyzir-Rahiym (Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika daima – Mwenye kurehemu). Ambaye Anakuona wakati unaposimama. Na mageuko yako (ya kuinama na kusimama katika Swalaah na) katika wenye kusujudu. Hakika Yeye Ndiye As-Samiy’ul-‘Aliym (Mwenye kusikia yote daima - Mjuzi wa yote daima).” (26:217-220)
Na kauli Yake Ta´ala:
وَمَا تَكُونُ فِي شَأْنٍ وَمَا تَتْلُو مِنْهُ مِن قُرْآنٍ وَلَا تَعْمَلُونَ مِنْ عَمَلٍ إِلَّا كُنَّا عَلَيْكُمْ شُهُودًا إِذْ تُفِيضُونَ فِيهِ
”Na hushughuliki (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) katika jambo lolote, na wala husomi humo (chochote) katika Qur-aan, na wala (enyi Watu) hamtendi ‘amali yoyote isipokuwa Tunakuwa Mashahidi juu yenu mnaposhughulika nayo.” (10:26)


Daraja ya tatu katika daraja za Dini ni daraja ya Ihsaan, nayo ndio iko juu kabisa. Ihsaan haina nguzo, isipokuwa ni kitu kimoja. Ihsaan  imegawanyika sehemu mbili:
1.    Ihsaan baina ya mja na Mola Wake. Na hapa ndicho kinachokusudiwa. Ihsaan baina ya mja na Mola katika ´Ibaadah yake.
2.    Ihsaan baina ya mja na watu.
3.    Na kuna Ihsaan ya tatu ambayo ni mtu kukifanya kitu vizuri kabisa. Huitwa Ihsaan pia.
Ihsaan baina  ya mja na Mola Wake kabainisha hilo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pindi alipomuuliza Jibriyl (´alayhis-Salaam). Akasema:
“Ni kumuabudu Allaah kama kwamba unamuona, na ikiwa humuoni, basi Yeye Anakuona.”
Ihsaan baina ya mja na Mola Wake ni kuifanya ´amali yake Aliyomkalifisha kwayo Allaah, mtu aifanye sahihi kwa kuitakasa Akitafuta Uso wa Allaah (´Azza wa Jalla). Ihsaan baina ya mja na Mola Wake ni ile iliyo na Ikhlaasw kwa Allaah (´Azza wa Jalla) na kumfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hivyo ´amali haiwi hasanan njema na Ihsaan isipokuwa ikiwa mtu kaifanya kwa ajili ya Allaah Pekee (´Azza wa Jalla) na kwa usawa kwa mujibu wa Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).
Isitoshe, kabainisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba Ihsaan iko juu ya daraja mbili, moja wapo iko juu kuliko nyingine.
1.    Ya kwanza ni wewe kumuabudu Allaah kama vile unamuona, uwe na yakini na Imani kumuamini Allaah kama kwamba unamshuhudia Allaah. Huna shaka yoyote ile, bali [uwe na yakini] kama kwamba Allaah Yuko mbele yako (Subhaanahu wa Ta´ala) na unamuona. Yule atakayefikia daraja hii ndiye mwenye Ihsaan ya juu kabisa. Allaah Haonekani duniani na ndio maana kasema [Mtume]:

“... kama vile unamuona.”

Kwa kuwa Allaah Haonekani duniani bali Ataonekana Aakhirah. Kwa ajili hiyo watalipwa watu wa Ihsaan Aakhirah kwa kumuona (Subhaanahu wa Ta´ala). Watapomuabudu kama vile wanamuona duniani, Allaah Atawalipa kwa kuwawezesha wamuone (Subhaanahu wa Ta´ala).
لِّلَّذِينَ أَحْسَنُوا الْحُسْنَىٰ وَزِيَادَةٌ
”Kwa wale waliofanya wema watapata (jazaa ya ihsaan; nayo ni) al-Husnaa (Pepo) na zaidi (ya hayo ni kupata taadhima ya kumuona Allaah).” (10:26)
Kwa vile wamefanya Ihsaan, Allaah Atawapa “al-Husnaa” nayo ni Pepo. Na “zaidi” nayo ni kumuona Allaah (´Azza wa Jalla).
2.    Dara ya pili – ikiwa hukufikia daraja hii kubwa – muabudu kwa njia ya kama vile Yeye Anakuona, Anajua hali yako, na Anajua yaliyomo ndani ya nafsi yako. Haikustahiki wewe kumuasi na kwenda kinyume na amri Zake Naye Anakuona. Na hii ni hali nzuri lakini ni ndogo kuliko ile ya kwanza. Ya kwanza ni kana kwamba wewe unamuona Allaah, na ya pili unamuabudu Allaah na ujue ya kwamba Yeye Anakuona. Maadamu unajua ya kwamba Anakuona hivyo ifanye vizuri kabisa (Ihsaan) ´Ibaadah Yake. Kwa kuwa unajua ya kwamba Allaah Anakuona.
Hizi ndio daraja za juu kabisa za Dini. Yule anayefikia daraja hizi, basi huyo kafikia daraja za juu kabisa za Dini.


Na dalili katika Sunnah ni Hadiyth mashuhuri ya Jibriyl:
“Imepokelewa kutoka kwa 'Umar (رضى الله عنه) ambaye amesema: Siku moja tulikuwa tumekaa na Mtume ( صلى الله عليه وسلم), hapo alitokea  mtu ambaye  nguo zake zilikuwa nyeupe pepe na nywele zake zilikuwa nyeusi sana; hakuwa na alama  ya machofu ya safari na wala hapakuwa na hata mmoja katika sisi aliyemtambua. Alienda akakaa karibu na Mtume ( صلى الله عليه وسلم) akaweka magoti yake karibu na magoti yake (Mtume) na akaweka viganja vyake juu ya mapaja yake kisha akasema; Ewe Muhammad! Niambie kuhusu Uislamu. Mjumbe wa Allaah  ( صلى الله عليه وسلم) alisema:  Uislamu ni kukiri kuwa hakuna mola isipokuwa  Allaah na Muhammad ni Mjumbe wake, kusimamisha Swalah, kutoa Zakaah, kufunga Ramadhaan na kwenda kuhiji (Makkah) ukiweza.
(Akasema yule mtu yaani Jibriyl) Umesema kweli. Tulipigwa na mshangao kwa kumuuliza kwake Mtume na kumsadikisha.  Na akasema tena: Niambie  kuhusu Iymaan.  Akasema (Mtume صلى الله عليه وسلم) Ni kumwamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Yake na siku ya Qiyaama, na  kuamini ya kuwa kheri na shari zinatoka Kwake (Allaah سبحانه وتعالى  ). (Akasema Jibriyl): Umesema kweli, akasema hebu nielezee kuhusu Ihsaan.  Akasema Mtume ( صلى الله عليه وسلم): Ni kumuabudu Allaah سبحانه وتعالى )  kama vile unamuona na kamahumuoni basi Yeye Anakuona.  Akasema (Jibriyl):  Niambie    kuhusu Qiyaama.  Akajibu (Mtume ( صلى الله عليه وسلم): Muulizwaji si mjuzi kama asivyo vilevile Muulizaji. Kisha akamwambia: Nijulishe alama zake: Akajibu (Mtume صلى الله عليه وسلم): Kijakazi atazaa bibi yake, na utaona wachunga wenda miguu chini, wenda uchi (wasio na uwezo wa kumiliki hata mavazi), mafukara (wasiokuwa hata na sehemu ya kuishi kwa umaskini) wakishindana kujenga majumba ya fahari. Kisha akaondoka (Jibriyl) na nilitulia kidogo (nikitafakari). Kisha akasema Mtume ( صلى الله عليه وسلم)" Ewe 'Umar! Je, unamjua ni nani yule aliyekuwa akiuliza? Nikasema: Allaah na Mjumbe wake wanajua zaidi.  Akasema Mtume  ( صلى الله عليه وسلم): Ni Jibriyl, alikuja kuwafundisha dini yenu.”

Jibriyl (´alayhis-Salaam) alikuja kwa sura ya mtu kwa kuwa akiwajia kwa sura ya Malaika hawaliwezi hili. Hapa pengine alimwita ee Muhammad ili wasimjue wadhani ya kwamba (Jibriyl) ni katika mabedui. Kwa kuwa ada ya mabedui walikuwa wakimwita kwa jina lake. Akamtajia nguzo sita za Imani baada ya kumtajia nguzo za Uislamu.
Uislamu na Imani vikitajwa pamoja: Uislamu maana yake ni vitendo vya dhahiri na Imani maana yake ni vitendo vya moyoni na yakini, ya usadikishaji na ya elimu anayosimama nayo mtu. Vikitajwa vyote kila kimoja kinakuwa na maana yake maalum. Na kinapotajwa kimoja wapo kimoja kinaingia kwenye kingine. Kunapotajwa Uislamu, Imani inaigia humo. Na inapotajwa Imani peke yake, Uislamu unaingia humo. Kwa kuwa hausihi Uislamu bila ya Imani, na Imani hausihi bila ya Uislamu. Ni mambo mawili yanaenda sambamba. (Jibriyl) akamuuliza kuhusu vitendo vya dhahiri na vya ndani. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akambainishia nguzo za Uislamu na Imani.
“ Muulizwaji si mjuzi kama asivyo vilevile Muulizaji.” yaani si mimi wala wewe hakuna ajuae. Allaah Hakumuachia Mtume yeyote wala Malaika kujua lini Qiyaamah kitakuwa. Hii ni Elimu Aijuae Yeye Mwenyewe.
Maulamaa wanasema Qiyaamah kina alama aina tatu:
1.    Alama ndogo
2.    Alama za kati kati
3.    Alama kubwa
Alama ndogo na kubwa zote zimeshaonekana, au nyingi katika hizo.
Ama alama kubwa: Kuchomoza jua kutoka magharibi, kujitokeza kwa ad-Dajjaal, kutoka kwa mnyama, kutoka kwa Ya´jjuuj na Ma´jjuuj. Hizi zitachelewa kuja, zitakuwa karibu na kusimama Qiyaamah. Na zitafuatana [itapoanza moja haitokawia kufuatia nyingine].
Katika Hadiyth (ya Jibriyl) tunapata mafunzo (faida) nyingi:
1.    Dini imegawanyika katika daraja tatu: Uislamu, Imani na Ihsaan. Na kila daraja iko juu kuliko iliyo kabla. Na kila daraja ina nguzo zake.

2.    Kufunza kwa njia ya [kuuliza] swali na jibu. Na njia hii ni ya mafunzo.

3.    Mwenye kuuliza kuhusu elimu na akawa hajui, aseme: “Allaah na Mtume Wake ndio wenye kujua.” Asijikakame na kusema kitu asichokijua. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kasema: “Muulizwaji si mjuzi kama asivyo vilevile muulizaji.” Na alipowauliza Maswahabah (Radhiya Allahau ´anhum): “Mnamjua ni nani muulizaji?” Wakasema: “Allaah na Mjumbe Wake wanajua zaidi.”
Ni dalili ya kwamba masuala ya Shari´ah haijuzu kujikakama.

Na alikuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anapoulizwa baadhi ya maswali na hana Wahyi kutoka kwa Allaah (´Azza wa Jalla) anasubiri mpaka unapokuja Wayhi kutoka kwa Allaah. Na wasiokuwa wao ni aula zaidi. Wanapouliza na hawana jibu wasubiri mpaka watapoenda kuuliza wenye elimu zaidi yao au katika vitabu vya wanachuoni na kutazama wanavyosema.

4.    Katika Hadiyth kuna dalili adabu ya mwenye kujifunza. Jibriyl (´alayhis-Salaam) naye ni kiongozi wa Malaika kakaa mbele ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaweka magoti yake karibu na magoti yake na kuuliza kwa adabu. Hii ni kwa sababu awafunze watu jinsi ya kuwa na adabu pamoja na mwalimu wao (Mtume). Kuwa na adabu kwa mwenye kujifunza na mwalimu pia. Pindi aliposema Mtume: “Muulizwaji si mjuzi kama asivyo vilevile muulizaji.”

5.    Baadhi ya alama za Qiyaamah.


Msingi Wa Tatu: Kumjua Nabii wenu Muhammad ( صلى الله عليه وسلم).
Naye ni Muhammad bin ´Abdillaah bin ´Abdul-Muttwalib bin Haashim. Na Haashim ni kutoka katika (kabila la) la Quraysh. Na Quraysh ni katika Waarabu. Na Waarabu ni kutokana na kizazi cha Ismaa´iyl bin Ibraahiym Al-Khaliyl Swalah na salamu bora kabisa ziwafikie yeye na Mtume wetu. Naye alikuwa na umri wa miaka sitini na tatu, miaka arubaini kabla yakupewa utume, na miaka ishirini na tatu akiwa katika utume. Akapewa utume kwa  ((Iqraa - Soma)) na akatumwa (kulingania) kwa  ((Al-Muddath-thir – mwenye kujigubika)). Na nchi yake ni Makkah.


3.    Msingi wa tatu

Alipokuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni waasitwah mkatikati baina ya Allaah na baina ya waja Wake katika kufikisha Dini na Risaalah Yake, ikawa ni wajibu kumjua (´alayhis-Swalaat was-Salaam). La sivyo vipi utamfuata mtu usiyemjua? Haikupasi wewe kumfuata mtu nawe humjui. Unapoulizwa “Ni nani Mtume Muhammad?” Unasema “Sijui”. Vipi basi utamfuata mtu usiyemjua. Ni jambo lisiloingia akilini.
Allaah Kakutumia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ni nani Mtume huyu? Hivyo ni lazima umjue: Jina lake, mji wake alipoishi, kukulia na alipohamia. Umri wake, aliishi muda kiasi gani katika maisha haya kabla ya kupewa utume na baada ya kupewa utume, na alipohama na kabla ya kuhama (kwenda Madiynah), lini alianza kuteremshiwa Wahyi, dalili zinazotolea utume na Risaalah yake, nasaba yake, ni katika kabila gani. Ni lazima uyajue mambo haya.
Jina lake ni Muhammad, na ana majina mengine lisilokuwa hilo. Lakini asli ya jina lake na lililosemwa sana ni hili. Ni Muhammad na Ahmad. Na maana yake ni mwingi wa sifa au mwenye kusifiwa. Na katika majina yake ni Nabiyy ar-Rahmah (Mtume wa Rahmah) na Nabiyy al-Malhamah (Mtume wa Jihaad katika njia ya Allaah). Mwenye kutaka kumjua zaidi arejee (kitabu) “Dalaail afhaam was-Swalaat was-Salaam ´alaa khayril anaam” cha Imaam Ibn al-Qayyim (Rahimahu Allaah). Hili ndio jina lake.
Ama nasabu yake ni Muhammad bin ´Abdillaah bin ´Abdil-Muttwalib bin Haashim bin ´Abdil-Manaaf bin Quswaiy bin Kilaab na inaendelea nasabu yake mpaka kwa Nabii Ismaa´iyl.
Kabila lake ni Quraysh kabila ambalo ni bora ya makabila. Na al-Quraysh ni katika kizazi cha Ismaa´iyl (´alayhis-Salaam) kutoka katika waarabu, na waarabu ni kutoka katika kizazi cha kiarabu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anatoka katika Baniy Haashiym, na Baniy Haashiym ni katika kizazi cha Ismaa´iyl (´alayhis-Salaam). Babu wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ´Abdul-Muttwalib jina lake sio hili, jina lake ni Shaybah. ´Abdul-Manaaf ana watoto wanne: Haashim, Muttwalib, ´Abdus-Shams, Mawfal. Baniy Haashim wanaitwa Haashimiyyuun. Na Baniy Muttwalib wanaitwa Muttwalibiyyuun.
Ama ´Abdus-Shams miongoni mwao kuna ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anhu), miongoni mwao kuna Baniy ´Umayyah, hawa ni katika ´Abdus-Shams.
Hali kadhalika Mawfal ana watoto, miongoni mwao ni Zubayr bin Mutw´im, Hakiym. Mkisoma vitabu vya nasabu mtajua haya. Ishqaah ni baba wa Baniy Israaiyl, na Mitume wote wote ni katika kizazi cha Ishqaah isipokuwa Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yeye ni katika kizazi cha Ismaa´iyl (´alayhis-Salaam). A Hii ndio nasabu yake (´alayhis-Swalaat was-Salaam), nasabu bora na kubwa.
Ama kuzaliwa kwake, kazaliwa (´alayhis-Swalaat was-Salaam) mwezi wa tembo. Mwezi ambao Maalik wa Yemen alikuja kutaka kuivunja al-Ka´abah na alikuwa na tembo kubwa. Alipofika mahali baina ya Muzdalifah na Minaa na palikuwa hapakubaki isipokuwa aingie Makkah na kuvunja Ka´abah na watu wa Makkah wakakimbia kwenye milima kwa kuwa hawakuwa na uwezo wa kupambana nae, basi tembo ikakataa kusimama kutoka katika ardhi. Akiielekeza kwenye jiha isiyokuwa ya Makkah inasimama na kwenda, na inapoelekezwa kwenye jiha ya Makkah inagoma na wala haiwezi kutembea. Basi ndo Kukatumwa ndege, kila ndege ilikuwa na mawe mawili kuja kuwaangamiza na Allaah (´Azza wa Jalla) Akawa Amewaangamiza. Ndipo Allaah Alipoteremsha Suurat al-Fiyl.
أَلَمْ تَرَ كَيْفَ فَعَلَ رَبُّكَ بِأَصْحَابِ الْفِيلِ أَلَمْ يَجْعَلْ كَيْدَهُمْ فِي تَضْلِيلٍ وَأَرْسَلَ عَلَيْهِمْ طَيْرًا أَبَابِيلَ  تَرْمِيهِم بِحِجَارَةٍ مِّن سِجِّيلٍ فَجَعَلَهُمْ كَعَصْفٍ مَّأْكُولٍ
 
”Je, huoni jinsi Mola wako Alivyowafanya watu wa ndovu (tembo)? Je, Hakujaalia mbinu zao kwenye kupotea? Na Akawatumia juu yao ndege makundi kwa makundi? Wakiwarembea kwa mawe ya udongo uliookwa (motoni). Akawafanya kama nyasi zilizoliwa.” (105:01-05)
 Hichi ndio kisa cha tembo. Allaah Akaihifadhi Nyumba Yake na Akawaangamiza watu hawa. Katika mwezi huu ndio alizaliwa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mwezi wa tembo. Na katika kuzaliwa kwake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kulidhihiri Aayaat Ishara na nuru.
Alizaliwa Makkah kwa Haliymah as-Sa´diyyah. Na baba yake alikufa alipokuwa tumboni mwa mama yake. Alikufa ´Abdullaah pindi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa tumboni mwa mama yake. Kisha akafariki pia mama yake baada ya kuzaliwa kwake. Akawa na babu yake ´Abdul-Muttwalib, kisha naye akafariki. Akaenda kwa ami (mjomba) wake Abu Twaalib, na akaishi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) miaka arubaini, alikuwa akijulikana kuhifadhi amaanah, ukweli, kujiepusha na ´Ibaadah za masanamu, kunywa pombe na kadhalika. Na alikuwa anakwenda katika pango linaloitwa Ghar hira na akimuabudu Allaah juu ya Mila (Dini) ya Ibraahiym ya Tawhiyd. Kisha alipofikisha miaka arubaini (´alayhis-Salaam) Wahyi ukamteremkia. Alimjia Jibriyl (´alayhis-Salaam) naye yuko kwenye pango akamwambia:
“Iqraa (soma)”. Akasema: “Mimi sio msomi” yaani siwezi kusoma. Akamlazimisha na kumwambia “Soma”. Akasema: “Mimi sio msomi”. Akamlazimisha mara ya pili na kumwambia: “Soma”. Akasema: “Mimi sio msomi”. Akamwambia:
اقْرَأْ بِاسْمِ رَبِّكَ الَّذِي خَلَقَ خَلَقَ الْإِنسَانَ مِنْ عَلَقٍ
 
“Soma kwa Jina la Mola wako Aliyeumba. Amemuumba bin-Aadam kutokana na pande la damu linaloning’inia.” (96:01-02)
Huu ndio utume wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Allaah Kamjaalia kuwa Mtume kwa Suurat ya kwanza Iqraa.
Akaenda nyumbani kwake akiwa na khofu kwa kufikwa na kitu ambacho alikuwa hajawahi. Akamuhadithia yaliyopitika bibi Khadiyjah (Radhiya Allaahu ´anha). Akamwambia: ”Hapana ewe Muhammad. Wallaahi, Allaah hawezi kukuhizi kamwe, kwani wewe ni mkweli muaminifu, uliyetakasika mwenye kuwaendea watu wako na mwenye kuwasaidia wenye kuhitaji na kumuokoa mwenye dhiki.”
Akamtaka Mtume (Swallah Allaahu ´alayhi wa sallam) avae nguo haraka na afuatane naye mpaka kwa mzee mmoja msomi aliyekuwa wakati huo akiitwa Waraqah bin Nawfal ili amhadithie yale aliyoyaona. Waraqah akamwambia:
“Huyu ndiye Jibriyl ambaye Allaah Aliwateremshia Mitume wa kabla Muusa na ´Iysa, yareti kama ningeliishi mpaka pale watu wako watakapokutoa nchini kwako”. Mtume (Swallah Allaahu ´alayhi wa sallam) akamuuliza: “Hivyo watakuja kunitoa?” Waraqah akasema: “Ndiyo, hapana aliyekuja na haya uliyokuja nayo wewe isipokuwa lazima atafanyiwa uadui, na nikijaaliwa kuishi mpaka siku hiyo, basi nitakusaidia mpaka utakapopata ushindi.”


Allaah Amemtuma kuonya kuhusu shirki na kulingania katika Tawhiyd.
Na dalili ni kauli Yake Ta´ala:
يَا أَيُّهَا الْمُدَّثِّرُقُمْ فَأَنذِرْوَرَبَّكَ فَكَبِّرْوَثِيَابَكَ فَطَهِّرْوَالرُّجْزَ فَاهْجُرْوَلَا تَمْنُن تَسْتَكْثِرُوَلِرَبِّكَ فَاصْبِرْ
”Ee uliyejigubika. Simama na uonye. Na Mola wako mtukuze (kwa takbira). Na nguo zako zitwaharishe. Na Ar-Rujz (masanamu) epukana nayo. Na wala usifanye ihsani kwa ajili ya kutaraji kukithirishiwa (manufaa ya kidunia). Na kwa ajili ya Mola wako subiri.” (74:01-07) 
Na maana ya ((Inuka uonye)) ni aonye kuhusu shirki na alinganie katika Tawhiyd.
((Na Mola wako Mtukuze)) yaani: Mtukuze kwa Tawhiyd.
((Na nguo zako zitakase)) yaani:  Twaharisha ´amali zako kutokana na shirk.
((Na  Ar-Rujz – uchafu au najisi)): Uchafu au  najsi ni masanamu. Na kuyahama ni kuepukana nayo  kabisa  na kujiweka mbali nayo na watu wake.


Kisha ikamtemremkia Kauli Yake (Ta´ala):
يَا أَيُّهَا الْمُدَّثِّرُ قُمْ فَأَنذِرْ
“Ee uliyejigubika. Simama na uonye.” (74:01-02)
Alibaki Makkah miaka kumi akiwalingania watu katika Tawhiyd na kuacha ´Ibaadah ya kuabudu masanamu. Kukapitika maudhi baina yake yeye na washirikina kutokana na waliokuwa wakimuamini na kumfuata. Na kabla ya kufanya Hijrah kwenda Madiynah, alienda katika Bayt-ul-Maqdiys na akapandishwa mbinguni na kupewa Swalah tano. Na akaswali Makkah miaka mitatu. Kisha akawa katika hali ngumu ya maudhi, Allaah Akampa idhini kufanya Hijrah kwenda Madiynah.
Alifariki alipokuwa na miaka sitini na tatu (´alayhis-Salaam). Muda wa umri wake akiwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni miaka ishirini na tatu. Na Jihaad alizofanya, juhudi na mengineyo yote aliyafanya katika kipindi hichi cha miaka ishirini na tatu kwa miujiza, fadhila, baraka na Uwezo wa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).
Na hili ndio la wajibu kwa Madu´aat katika Da´wah yao, waliwekee umuhimu mkubwa suala la kuonya Shirki na kulingania katika Tawhiyd kabla ya kila kitu. La sivyo Da´wah yao haitokuwa juu ya Manhaj ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wamekalia kuwalingania watu katika kuwa na ukweli, kuacha Bid´ah na haramu, lakini Shirki hawaijali na wala hawaikatazi kabisa. Hii sio Da´wah kwa kuwa inakhalifu mfumo wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Allaah Kamtuma ili akataze Shirki na alinganie katika Tawhiyd. Ni lazima mtu aanze kwa kitu hichi kwanza kisha baada ya hilo ndio mtu aende katika mambo mengine. Kwa kuwa hakuna faida ya kitu ikiwa watu wako juu ya Shirki. Lau watu wataacha Zinaa, kunywa pombe, kuiba na wakasifika na kila fadhila katika fadhila za matendo na tabia njema lakini hawakuacha Shirki hakuna faida ya mambo haya. Kinyume chake, ikiwa mtu kasalimika na Shirki na akawa na madhambi makubwa chini ya Shirki, anatarajiwa Allaah Kumsamehe, au akaadhibiwa kadiri na madhambi yake lakini mwisho wake ni Peponi kwa kuwa ni Muwahhid. Tawhiyd ndio asli na ndio msingi.


Amechukua (Mtume) miaka kumi akilingania katika Tawhiyd kwa haya. Na baada ya miaka kumi, alipandishwa mbinguni (Mi´iraaj) na zikafaridhiswha Swalah tano, akaswali Makkah miaka mitatu, na baada ya hapo akaamrishwa kuhama kwenda Madiynah. Na Hijra ni kuhama kutoka nchi ya shirki kwenda katika nchi ya Kiislamu.


Aliishi Mtume Makkah miaka kumi na tatu. Katika miaka mikumi alikuwa akiamrisha Tawhiyd na kukataza Shirki kabla ya kufaradhishiwa chochote; si Swalah, Zakaah, Swawm, Hajj. Mtume (´alayhis-Salaam) alikuwa akiwalingania watu katika Tawhiyd na kuwakataza na Shirki. Alikuwa akiwaambia sehemi “laa ilaaha illa Allaah” mtaokoka. Nao wanasema:
أَجَعَلَ الْآلِهَةَ إِلَـٰهًا وَاحِدًا ۖ إِنَّ هَـٰذَا لَشَيْءٌ عُجَابٌ
 
“Amewafanya miungu (wote) kuwa ni Ilaah Mmoja (Anayestahiki kuabudiwa kwa haki)? Hakika hili ni jambo la ajabu mno!” (38:05)
Alibaki miaka kumi katika hali hii, akiwakataza Shirki na akiwalingania katika Tawhiyd. Huu ndio msingi. Kisha baada ya miaka kumi, mwanzoni wa mwaka wa kumi na moja ndio akasafiri usiku kutoka Masjid al-Haraam na kwenda Masjid al-Aqswaa.
سُبْحَانَ الَّذِي أَسْرَىٰ بِعَبْدِهِ لَيْلًا مِّنَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ إِلَى الْمَسْجِدِ الْأَقْصَى
”Subhaanah!  (Ametakasika - Allaah) Ambaye Amemchukua mja Wake (sehemu ya) usiku kutoka Al-Masjid Al-Haraam (wa Makkah) mpaka Al-Masjid Al-Aqswaa (Baytul-Maqdis, Palestina).” (17:01)
Alikuja Jibriyl na mnyama unaoitwa “al-Buraaq”. Akasafiri nao Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwenda nao Bayt-ul-Maqdis usiku. Na hili ni khaaswa kwake yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na katika miujiza yake. Akapandishwa mbinguni kwa Jibriyl kumsaidia (´alayhimas-Swalaat was-Salaam), akakutana (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na watu wa mbinguni, na kila alipokuwa akifika katika mbingu Jibriyl anamfungulia mpaka alipofika katika mbingu ya saba. Kisha akapanda juu ya mbingu [ya saba] mpaka kwenye Sidrat-ul-Muntahaa, na hapo ndipo Alipomuongelesha Allaah (´Azza wa Jalla) Wahyi Wake kwa ayatakayo na Akafaradhishiwa Swalah tano. Alimfaradhishia Swalah khamsini mchana na usiku, lakini Muusa (´alayhis-Salaam) akamshauri amuombe Mola Wake ampunguzie kwa kuwa watu wako hawatoweza Swalah khamsini mchana na usiku. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawa anarudi na kumuomba mpaka zilipofika Swalah tano.
Swalah tano mchana na usiku huzingatiwa ni Swalah khamsini katika mizani. Kwa kuwa [mwenye kufanya] jema moja ni sawa na kumi mfano wake. Swalah moja ni sawa na Swalah kumi, Swalah tano ni sawa na khamsini. Hii ni fadhila ya Allaah (´Azza wa Jalla) kwa Ummah huu.
Na ni lazima kuamini ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisafiri na kupandishwa kwa roho na mwili wake vyote pamoja na sio ndotoni. Kwa kuwa baadhi ya watu wanasema alipandishwa kwa roho yake, ama mwili wake haukutoka Makkah. Haya ni maneno ya batili. Bali alisafirishwa kwa roho na mwili wake (´alayhis-Salaam) na akafasiri na Buraaq. Ingelikuwa ni kwa roho yake tu au ingelikuwa ni ndotoni (usingizini). Allaah Asingelisema:
سُبْحَانَ الَّذِي أَسْرَىٰ
”Subhaanah!  (Ametakasika - Allaah) Ambaye Amemchukua mja Wake.” (17:01)
Na neno “abdihi (mja Wake)” ni roho pamoja na mwili. Haiwezekani kusema roho peke yake kuwa ni mja, na wala mwili peke yake kusema ni mja, isipokuwa ni roho pamoja na mwili vyote viwili. Hakusema:
”Subhaanah!  (Ametakasika - Allaah) Ambaye Amechukua roho ya mja Wake.”
Bali Kasema:
سُبْحَانَ الَّذِي أَسْرَىٰ
”Subhaanah!  (Ametakasika - Allaah) Ambaye Amemchukua mja Wake.” (17:01)
Na mja ni roho pamoja na mwili. Na Allaah (Jalla wa ´Alaa) Hashindwi na kitu. Ni Muweza wa kila kitu.
Akafaradhishiwa Swalah tano Makkah, akaswali Makkah kwa kipindi cha miaka mitatu. Na alikuwa akiswali Rakaa mbili mbili. Mwanzoni kulipofaradhishwa Swalah, kulikuwa kunaswaliwa Rakaa mbili mbili. Alipofanya Hijrah kuhama Mtume, Swalah za Rakaa nne akawa anaziswali kwa kutimiza Rakaa nne. Swalah ya Fajr inaswaliwa kama ilivyo mbili, na ya Maghrib inaswali tatu kama ilivyo kwa kuwa ni Witr ya usiku. Ama Dhuhr, ´Aswr na ´Ishaa alikuwa anaswali Makkah Rakaa mbili mbili mpaka alipohama ndio akawa anakamilisha Rakaa nne nne.
Swalah imefaradhishwa Makkah hili ni kwa Ijmaa´ ya wanachuoni, lakini  wametofautiana imefaradhishwa kabla ya Hijrah kwa miaka mitatu, mitano, mwaka huyo huyo au mwaka na nusu? Na hii ndio kauli yenye nguvu ya wanachuoni na kama alivyosema Shaykh kwamba ni kabla ya Hijrah kwa miaka mitatu.  Je, Swalah imefaradhishwa pamoja na kitu kingine? Kuna khilaaf pia hapa. Kuko ambao wanaona Zakaah ilifaradhishwa pamoja na Swalah Makkah. Kauli ya pili – na ndio ya Shaykh – ni kwamba Zakaah imefaradhishwa Madiynah na sio Makkah isipokuwa tu nguzo ya kwanza ambayo ni Tawhiyd na Swalah ambayo ni nguzo ya pili. Hii ndio dhahiri kwa maneno ya Shaykh.


Hijrah ni fardhi kwa Ummah huu (Waislamu wote kwa ujumla) kuhama kutoka katika nchi ya shirki kwenda nchi ya Kiislamu. Nayo  itaendelea kubakia hadi itakaposimama Saa (Qiyaamah).
Na dalili ni kauli Yake Ta´ala:
إِنَّ الَّذِينَ تَوَفَّاهُمُ الْمَلَائِكَةُ ظَالِمِي أَنفُسِهِمْ قَالُوا فِيمَ كُنتُمْ ۖ قَالُوا كُنَّا مُسْتَضْعَفِينَ فِي الْأَرْضِۚ قَالُوا أَلَمْ تَكُنْ أَرْضُ اللَّـهِ وَاسِعَةً فَتُهَاجِرُوا فِيهَا ۚ فَأُولَـٰئِكَ مَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ ۖ وَسَاءَتْ مَصِيرًا إِلَّا الْمُسْتَضْعَفِينَ مِنَ الرِّجَالِ وَالنِّسَاءِ وَالْوِلْدَانِ لَا يَسْتَطِيعُونَ حِيلَةً وَلَا يَهْتَدُونَ سَبِيلًا  فَأُولَـٰئِكَ عَسَى اللَّـهُ أَن يَعْفُوَ عَنْهُمْ ۚ وَكَانَ اللَّـهُ عَفُوًّا غَفُورًا
”Hakika wale ambao Malaika wamewafisha, hali wamejidhulumu nafsi zao; (Malaika) watawaambia: “Mlikuwa katika hali gani?” Watasema: “Tulikuwa tukikandamizwa katika ardhi.”  (Malaika) Watasema: “Je, kwani ardhi ya Allaah haikuwa ya wasaa mkahajiri? Basi hao makazi yao yatakuwa ni (Moto wa) Jahannam, na ubaya ulioje mahali pa kurejea. Isipokuwa wale waliokandamizwa kati ya wanaume na wanawake na watoto ambao hawakuweza kupata (mpango wa) hila yoyote wala hawawezi kuongoza njia. Basi hao huenda Allaah Akawasamehe. Na Allaah ni ‘Afuwwan-Ghafuwraa (Mwingi wa kusamehe - Mwingi wa kughufiria).” (04:97-99)


Baada ya maudhi na shari ya Quraysh kuzidi Allaah Aliwapa ruhusa (Subhaanahu wa Ta´ala) Waislamu kuhama kwenda Habashah (Ethiopia) ili waweza kudhihirisha Dini yao. Wakahama waliohama kwenda Habashah, na hii ndio inaitwa Hijrah ya kwanza. Quraysh wakamtumia ujumbe mfalme wa huko kwamba wawarudishe watu hao waliokimbia, lakini Najaash (Rahimahu Allaah) akawasikiliza Muhaajiruun watavyosema na wakawa wamechagua kubaki zao Habashah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamlingania Najaash akasilimu (Rahimahu Allaah). Alipokufa Najaash, akamsalia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yeye na Maswahabah zake Swalat-ul-Ghayb. Kuhama kwao kule [Maswahabah] ikawa kheri kwake pia, Allaah Akamuongoza na akaingia katika Uislamu.
Hijrah kilugha ni kuacha kitu, ama Kishari´ah – kama alivyosema Shaykh – ni kuhama kutoka katika nchi (mji) ya kufuru na kwenda nchi ya Kiislamu. Hii ndio Hijrah ya Kishari´ah. Na Hijrah ni ´amali kubwa, Allaah Kailinganisha na Jihaad katika Aayah nyingi. Na pindi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipohama kwenda Madiynah walikuja Muhaajiruun waliokuwa Habashah. Walitoka Habashah wakaja Madiynah. Wakakusanyika Waislamu Madiynah na wakafanya Dola Madiynah Muhaajiruun na Answaar na wenye kusilimu wakawa wanakuja kwao. Wakati huo ndipo Allaah Alipowekea Shari´ah mambo mengine yaliobakia ya Dini na Akafaradhishiwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Swawm mwaka wa pili, Hajj mwaka wa tisa kutokana na kauli yenye nguvu na hivyo zikawa zimekamilika nguzo za Uislamu.
Tunachojifunza hapa ni kuelewa ya kwamba Tawhiyd ndio msingi wa kwanza wa Da´wah, na kwamba ni mtu anaanza nayo kabla ya Swalah, Swawm, Zakaah au Hajj. Kwa kuwa Mtume – kama mlivyosikia – alibakia (Makkah) miaka kumi akilingania Tawhiyd na akikataza Shirki na wala hakuamrisha Swalah, Zakaah, Swawm wala Hajj. Faradhi hizi zililetwa baada ya kuihakikisha Tawhiyd.
Na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipokuwa anamtuma Mu´aadh (Radhiya Allaahu ´anhu) anamuamrisha awalinganie watu kwanza katika Tawhiyd, kama ilivyokuja katika Hadiyth ya Mu´aadh:
“Hakika wewe unawaendea watu katika Ahl-ul-Kitaab, basi iwe kitu cha kwanza utakachowalingania kwacho “hapana mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah, na kwamba Muhammad ni mja wake na Mtume Wake. Wakikuitikia (wakikukubalia) kwa hilo, waambie ya kwamba Allaah Kawafaradhishia juu yao Swalah tano... “
Ni dalili ya kwamba hakuamrishwi Swalah, Zakaah, Swawm ila baada ya kuhakikisha Tawhiyd. Ama mwenye kuanza kitu kingine badala ya Tawhiyd Da´wah yake ni batili na Manhaj yake ni potofu inakhalifu Manhaj ya Mitume wote (´alayhimus-Swalaat wa-Salam). Mitume wote walikuwa wakianza kwa Tawhiyd na kuzisahihisha ´Aqiydah. Hili ni jambo muhimu Waislamu wanapaswa kulijua.
Kuna jambo lingine muhimu sana kulijua linalowachanganya watu wengi. Ni upi mji wa Kiislamu na mji wa kikafiri?
Mji wa kikafiri ni ule ambao hukumu yake ni kinyume na Aliyoteremsha Allaah. Inahukumu kinyume na Aliyoteremsha Allaah, huu ndio mji wa kikafiri.
Mji wa Kiislamu ni ule ambao unahukumu kwa yale Aliyoteremsha Allaah, huu ndio mji wa Kiislamu.
Hijrah ni faradhi, imelinganishwa na Jihaad katika njia ya Allaah. Ni yenye kubaki na haikufutwa. Ni wajibu kwa Muislamu mwenye uwezo kuhama, na haijuzu kwa Muislamu kuishi katika nchi (mji) ya kikafiri naye hawezi kuidhihirisha Dini yake. Ni wajibu kwake kuhama katika nchi (mji) ya Kiislamu. Anasema Allaah:
إِنَّ الَّذِينَ تَوَفَّاهُمُ الْمَلَائِكَةُ ظَالِمِي أَنفُسِهِمْ قَالُوا فِيمَ كُنتُمْ ۖ قَالُوا كُنَّا مُسْتَضْعَفِينَ فِي الْأَرْضِۚ قَالُوا أَلَمْ تَكُنْ أَرْضُ اللَّـهِ وَاسِعَةً فَتُهَاجِرُوا فِيهَا ۚ فَأُولَـٰئِكَ مَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ ۖ وَسَاءَتْ مَصِيرًا
”Hakika wale ambao Malaika wamewafisha, hali wamejidhulumu nafsi zao; (Malaika) watawaambia: “Mlikuwa katika hali gani?” Watasema: “Tulikuwa tukikandamizwa katika ardhi.”  (Malaika) Watasema: “Je, kwani ardhi ya Allaah haikuwa ya wasaa mkahajiri? Basi hao makazi yao yatakuwa ni (Moto wa) Jahannam, na ubaya ulioje mahali pa kurejea.” (04:97)
Aayah hii iliteremka kwa wale ambao hawakuhama na wanaweza kuhama.
وَمَن يُهَاجِرْ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ يَجِدْ فِي الْأَرْضِ مُرَاغَمًا كَثِيرًا وَسَعَةً ۚ وَمَن يَخْرُجْ مِن بَيْتِهِ مُهَاجِرًا إِلَى اللَّـهِ وَرَسُولِهِ ثُمَّ يُدْرِكْهُ الْمَوْتُ فَقَدْ وَقَعَ أَجْرُهُ عَلَى اللَّـهِ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا
”Na anayehajiri katika Njia ya Allaah atapata katika ardhi mahali pengi pa kukimbilia na wasaa. Na atakayetoka nyumbani kwake akiwa ni mwenye kuhajiri kwa ajili ya Allaah na Mtume Wake, kisha mauti yakamfikia, basi ujira wake umeshatokea kwa Allaah. Na Allaah ni Ghafuwrar-Rahiymaa (Mwingi wa kughufiria – Mwenye kurehemu).” (04:100)
Akihama mtu na akafa njiani, Allaah Anamwandikia kuwa kafanya Hijrah.
Katika Aayah hizi mbili kuna tishio kwa yule ambaye kaacha kuhama na anaweza kuhama, na kwamba mafikio yake ni Motoni na ni makazi mabaya sana. Katishiwa Moto – hata kama hatoki katika Uislamu – lakini nususi hizi ni za tishio. Vinginevyo ni kwamba mwenye kuacha kuhama kaacha jambo la wajibu miongoni mwa mambo ya wajibu na anakuwa ni muasi lakini hatoki katika Uislamu kwa kuacha kuhama. Lakini ana tishio kubwa.
Kisha Allaah Kabainisha Aayah zilizo baada yake udhuru wa kumzuia mtu na Hijrah:
إِلَّا الْمُسْتَضْعَفِينَ مِنَ الرِّجَالِ وَالنِّسَاءِ وَالْوِلْدَانِ لَا يَسْتَطِيعُونَ حِيلَةً وَلَا يَهْتَدُونَ سَبِيلًا
”Isipokuwa wale waliokandamizwa kati ya wanaume na wanawake na watoto ambao hawakuweza kupata (mpango wa) hila yoyote wala hawawezi kuongoza njia.” (04:98)
“al-wildaan” yaani watoto. “hiylah” yaani hawana uwezo wa kufanya Hijrah.
“Wala yahtaduuna sabiyla” hawajui njia ya mji wanapokwenda Madiynah. Kwa kuwa Hijrah inahitajia safari, ikiwa mtu hajui njia anapotea. Udhuru wao ni kwa mambo mawili: “laa yastatwi´uuna hiylah” kwa kutokuwa na uwezo wa kimali. “Wala yahtaduuna sabiyla” hata akiwa na uwezo wa kimali, hajui njia atayopita. Hana wa kumuonesha. Huu ndio udhuru sahihi.
Ama mtu mwenye uwezo na anajua njia, huyu hana udhuru hata ikiwa atajisemesha “sisi tumekandamizwa” Hili sio sahihi. Allaah Hakuwapa udhuru na wala hakuwachukulia kuwa ni wenye kukandamizwa katika ardhi. Bali Kawatishia Moto na ni makazi mabaya kabisa.


Na Kauli Yake Ta´ala:
يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّ أَرْضِي وَاسِعَةٌ فَإِيَّايَ فَاعْبُدُونِ
“Enyi waja Wangu ambao mmeamini! Hakika ardhi Yangu ni pana, basi Mimi (Pekee) Niabuduni.” (29:56)

Amesema Al-Baghaawiy : “Aayah hii imeteremshwa kwa sababu ya Waislamu waliokuwa Makkah ambao hawakuhajiri. Allaah Amewaita kwa jina la Waumini.
Na dalili ya Hijrah (kuhajiri) katika Sunnah ni kauli yake (صلي الله عليه وسلم):  ((Hijrah haikatiki mpaka ikatike tawbah. Na tawbah haikatiki mpaka jua lichomoze kutoka Magharibi))  [Abu Daawuud, Ahmad, Ad-Daarimiy na ni Swahiyh kwa mujibu wa Al-Albaaniy katika Swahiyhul-Jaami´ As-Swaghiyr    7346]


Katika Aaya hii kuna amri ya kufanya Hijrah. Ukiwa katika mji ambapo huwezi kudhihirisha Dini yako humo, ardhi ya Allaah ni kubwa na pana. Usibaki ukajibana humo, toka uende katika ardhi pana. Allaah Kakufanyia ardhi kuwa pana (Subhaanahu wa Ta´ala). Hata kama itakuwa ni katika milima nenda. Na Kauli Yake:
يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّ أَرْضِي وَاسِعَةٌ فَإِيَّايَ فَاعْبُدُونِ
 
“Enyi waja Wangu ambao mmeamini! Hakika ardhi Yangu ni pana, basi Mimi (Pekee) Niabuduni.” (29:56)
Kuna dalili ya kwamba mwenye kuacha kufanya Hijrah ni katika waumini na kwamba hakufuru. Ni dalili ya kwamba Aayah iliyopo katika Suurat-un-Nisaa ni ya tishio.

Baada ya kutulia kimakazi Madiynah  [Mtume]  aliamrisha Shari´ah za Kiislamu zilobakia kama; Zakaah, Swawm, Hajj, Adhaan, Jihaad, kuamrisha mema na kukataza maovu na mengineyo ya Shari´ah ya Kiislamu. Amefanya hayo miaka kumi akafariki baada ya hapo, Swalah na salamu ziwe juu yake. Na Dini  yake  imebaki. Na hii Dini yake, hakuna kheri  isipokuwa kawaelekeza kwayo Ummah, na hakuna shari ila amewatahadharisha nayo. Na kheri aliyowaongoza kwayo ni Tawhiyd na yote Anayoyapenda Allaah na Anayoyaridhia. Na shari ambazo amezitahadharisha ni shirki na yote yanayomchukiza Allaah  na Asiyoyaridhia. Allaah Amemtuma  [yeye]  kwa watu wote, na Amefaradhisha Ath-Thaqalayn [walimwengu wawili]; majini na watu kumtii yeye [Mtume]. Na dalili ni kauli Yake Ta´ala:
قُلْ يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنِّي رَسُولُ اللَّـهِ إِلَيْكُمْ جَمِيعًا
“Sema (ee Mtume Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): “Hakika mimi ni Mtume wa Allaah kwenu nyinyi nyote.” (07:158)
Na Allaah Ameikamilisha hii Dini kwa kupitia kwake. Na dalili ni kauli ya Yake Taala:
الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا
”Leo wamekata tamaa (kabisa) wale ambao wamekufuru katika Dini yenu.” (05:03)
Na dalili ya kifo chake (صلي الله عليه وسلم): ni kauli Yake Ta´ala:
إِنَّكَ مَيِّتٌ وَإِنَّهُم مَّيِّتُونَثُمَّ إِنَّكُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ عِندَ رَبِّكُمْ تَخْتَصِمُونَ
”Hakika wewe ni mfu (utakufa) na wao pia wafu (watakufa). Kisha hakika nyinyi Siku ya Qiyaamah mbele ya Mola wenumtakhasimiana.” (39:39-40)
Na watu watakapokufa watafufuliwa. Na dalili ni kauli Yake Ta‟ala:
مِنْهَا خَلَقْنَاكُمْ وَفِيهَا نُعِيدُكُمْ وَمِنْهَا نُخْرِجُكُمْ تَارَةً أُخْرَىٰ
”Kutoka humo (ardhini) Tumekuumbeni, na huko Tutakurudisheni, na kutoka humo Tutakutoeni mara nyingine.” (20:55)

Na kauli Yake Ta´ala:
وَاللَّـهُ أَنبَتَكُم مِّنَ الْأَرْضِ نَبَاتًا ثُمَّ يُعِيدُكُمْ فِيهَا وَيُخْرِجُكُمْ إِخْرَاجًا
 
”Na Allaah Amekuotesheni katika ardhi muotesho (kama mimea). Kisha Atakurudisheni humo (ardhini), na Atakutoeni (tena) mtoke  (kuwa hai Siku ya kufufuliwa).” (71:17-18)

Na baada ya kufufuliwa watahesabiwa na watalipwa kwa ´amali zao. Na dalil ni kauli Yake Ta´ala:
وَلِلَّـهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ لِيَجْزِيَ الَّذِينَ أَسَاءُوا بِمَا عَمِلُوا وَيَجْزِيَ الَّذِينَ أَحْسَنُوا بِالْحُسْنَى
 
”Na ni vya Allaah Pekee vyote vilivyomo mbingunu na ardhini ili Awalipe (adhabu ya Moto) wale waliofanya uovu kwa yale waliyoyatenda, na (ili) Awalipe wale waliofanya wema kwa mazuri.” (53:31)

Na anayekadhibisha kufufuliwa amekufuru.
زَعَمَ الَّذِينَ كَفَرُوا أَن لَّن يُبْعَثُوا ۚ قُلْ بَلَىٰ وَرَبِّي لَتُبْعَثُنَّ ثُمَّ لَتُنَبَّؤُنَّ بِمَا عَمِلْتُمْ ۚ وَذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ
 
”Waliokufuru wamedai kwamba hawatofufuliwa kamwe. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) Bali hapana! Naapa kwa Mola wangu, bila shaka mtafufuliwa, kisha mtajulishwa kwa yale (yote) mliyoyatenda, na hayo kwa Allaah ni sahali.” (64:07)

Na Allaah Ametuma Mitume wote wakiwa ni wabashiriaji (mema) na waonyaji. Na dalili ni kauli Yake Ta´ala:
رُّسُلًا مُّبَشِّرِينَ وَمُنذِرِينَ لِئَلَّا يَكُونَ لِلنَّاسِ عَلَى اللَّـهِ حُجَّةٌ بَعْدَ الرُّسُلِ
”Mitume ni wabashiriaji na waonyaji ili pasikuweko kutoka kwa watu hoja yoyote juu ya Allaah baada ya (kuletwa) Mitume.” (04:165)

Na wa kwanza wao ni Nuuh  na wa mwisho wao ni Muhammad (صلي الله عليه وسلم) naye ndiye Mtume wa mwisho. Na dalili kwamba Nuuh ndio wa mwanzo wao ni kauli Yake Ta´ala:
إِنَّا أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ كَمَا أَوْحَيْنَا إِلَىٰ نُوحٍ وَالنَّبِيِّينَ مِن بَعْدِهِ
”Hakika Tumekuletea Wahy (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kama Tulivyomletea Nuwh na Mitume baada yake.” (04:163)

Na kila Ummah Allaah Ameupelekea Mtume, kuanzia Nuuh hadi kwa Muhammad (صلى الله عليه وسلم). Akiwaamrisha kumwabudu Allaah Pekee, na Akiwakataza kuabudu miungu ya kitwaghuti (miungu yote ya uongo  na vyote viabudiwavyo kwa batili  kama mashetani, masanamu, mizimu, watu n.k.). Na dalili ni kauli Yake Ta´ala:
وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ
”Na kwa yakini Tulituma katika kila ummah Mtume (awaamrishe watu wake) kwamba: “Mwabuduni Allaah na jiepusheni na twaaghuwt (miungu ya uongo).” (16:36)

Na Allaah Akafaridhisha kwa waja wote wakanushe [´Ibaadah za] twaghuti na kumwamini Allaah (wamwabudu Yeye Pekee). Ibnul Qayyim  amesema: “Maana  ya twaghuti ni kila anachopindukia mja mipaka yake; ikiwa ni kinachoabudiwa, au kinachofuatwa au kinachotiiwa. Na matwaghuti ni wengi. Wakuu wao ni watano; Ibliys -laana za Allaah ziwe juu yake-, na anayeabudiwa hali ya kuwa yeye yuko radhi, na anayeita watu wamwabudu yeye, na anayedai kujua elimu ya ghayb (isiyoonekana na kujulikana isipokuwa na Allaah), na anayehukumu Asiyoyateremsha Allaah”. Na dalili ni kauli Yake Ta´ala:
لَا إِكْرَاهَ فِي الدِّينِ ۖ قَد تَّبَيَّنَ الرُّشْدُ مِنَ الْغَيِّ ۚ فَمَن يَكْفُرْ بِالطَّاغُوتِ وَيُؤْمِن بِاللَّـهِ فَقَدِ اسْتَمْسَكَ بِالْعُرْوَةِ الْوُثْقَىٰ لَا انفِصَامَ لَهَا ۗ وَاللَّـهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ
”Hapana kulazimisha katika (kuingia) Dini (kwenye moyo wa mtu), kwani imekwishabainika kati ya Uongofu na upotofu. Basi atakayemkanusha twaaghuwt (miungu ya uongo) na akamwamini Allaah kwa hakika atakuwa ameshikilia imara kishikilio madhubuti kisichovunjika, na Allaah ni Samiy’un-‘Aliym (Mwenye kusikia yote daima - Mjuzi wa yote daima).” (02:256)

Na hii ndio maana ya  Laa ilaaha illa-Allaah (hapana mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah). Na katika Hadiyth:  ((Kichwa cha jambo ni Uislamu, na nguzo yake ni Swalah, na juu ya nundu yake ni Jihaad katika Njia ya Allaah)) [At-Tirmidhiy, Ibn Maajah na ni Swahiyh kwa mujibu wa Al-Albaaniy katika Swahiyh Sunan At-Tirmidhiy 2110]



Na Allaah Anajua zaidi  na Swalah na salaam zimwendee Mtume Muhammad na Ahli zake na Maswahaba wake.