al-Hijaab

Kitabu hii kinazunguzia hijabu ya muislam sifa zake na hukumu zake.


al-Hijaab





Mwandishi:
Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn

Mfasiri:
Abu Bakr Khatwiyb al-Atrush


www.firqatunnajia.com








YALIYOMO
1. Ni wajibu kwa mwanamke kuufunika uso wake mbele ya wanaume ajinabi    4
2. Kufunika uso kunachangia kuhifadhi tupu    6
3. Uzuri wa mwanamke uko usoni    8
4. Uso ni mapambo yasiyotakikana kuonekana    9
5. Fitina iko usoni kwa mwanamke    10
6. Uso wa mwanamke ni wenye fitina zaidi kuliko sauti ya mnyororo wake    11
7. Tofauti ya mwanaume mtu mzima na kijana    12
8. Wanawake bora zaidi walikuwa wakijifunika nyuso zao    14
9. Ni wajibu kwa mwanamke ajifunike mbele ya wanaume ajinabi    16
10. Cha kwanza mchumbiaji huangalia huwa ni uso    16
11. Haijuzu kwa mwanamke kutoka kwenda mahala pa kuswalia bila ya mavazi ya juu    18
12. Wanawake wa kwanza walikuwa wakijifunika wanapotoka majumbani    19
13. Ni wajibu kwa mwanamke kufunika miguu yake anapotoka nyumbani    21
14. Mwanamke anaruhusiwa kuonesha uso mtumwa wake    22
15. Wajibu tu ndio iwezayo kuitikisa wajibu nyingine    23
16. Mwanamke kuonesha uso wake kuna madhara zaidi kuliko manufaa    25
17. Mwanamke kuonesha uso wake kunepelekea katika fitina    26
18. Mwanamke kuonesha uso wake kunamwondosha haya    27
19. Mwanamke kuonesha uso kunamfitinisha mwanaume    28
20. Mwanamke kuonesha uso wake kunapelekea katika mchanganyiko    29
21. Dalili juu ya kwamba inajuzu kwa mwanamke kuonesha uso    32
22. Dalili za kujifunika ni zenye kutangulizwa juu ya dalili za kujifunua    35
23. Tafsiri ya maneno ya Ibn ´Abbaas    36
24. Tafsiri ya Hadiyth ya Asmaa´    38
25. Tafsiri ya Hadiyth ya al-Fadhwl    39
26. Tafsiri ya Hadiyth ya mwanamke mwenye mashavu ya kupauka    40
27. Khitimisho ya kitabu "al-Hijaab"    41

 
 
1. Ni wajibu kwa mwanamke kuufunika uso wake mbele ya wanaume ajinabi

Himdi zote ni za Allaah. Tunamhimidi na kumuomba msaada na msamaha. Tunajikinga Kwake kutokana na shari ya nafsi zetu na matendo yetu maovu. Yule mwenye kuongozwa na Allaah, basi hakuna awezae kumpoteza, na yule mwenye kupotezwa na Allaah, basi hakuna awezae kumwongoza. Ninashuhudia ya kwamba hapana mola wa haki isipokuwa Allaah na ninashuhudia ya kwamba Muhammad ni mja na Mtume Wake. Allaah amswalie yeye, kizazi chake, Maswahabah zake na kila mwenye kuwafuata kwa wema mpaka siku ya Qiyaamah.
Amma ba´d:
Allaah (Ta´ala) amemtuma Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na uongofu na dini ya haki ili kuwaondosha watu kutoka gizani na kuwaongoza katika nuru, kwa idhini ya Mola wao, kwenda katika njia [inayoelekeza kwa], Mwenye nguvu na msifiwa. Allaah amemtuma ili aweze kuabudiwa Yeye mwenyewe kwa kukamilisha udhalilikaji na unyenyekevu Kwake Allaah (Tabaaraka wa Ta´ala) kwa kutekeleza maamrisho Yake na kujiepusha na makatazo Yake na kutanguliza hayo mbele ya matamanio na shahawa za nafsi. Allaah amemtuma vilevile ili kutimiza tabia njema na kulingania kwayo kwa kutumia kila njia na kubomoa tabia zote mbaya na kutahadharisha nazo kwa kutumia kila njia. Kwa ajili hiyo ndio maana Shari´ah yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) imekamilika kwa njia zote. Haihitajii kiumbe mwenye kuikamilisha na kuipanga. Ni yenye kutoka kwa mwingi wa hekima na Mjuzi wa yale yote ambayo ni mema kwa waja Wake na ni Mwenye kuwahurumia.
Mfano mmoja wa tabia hizo nzuri alizotumwa nazo Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni haya ambayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameifanya kuwa ni sehemu katika imani. Hakuna yeyote mwenye kupinga ya kwamba Shari´ah na desturi vyote viwili vimemwamrisha mwanamke kuwa na haya na kuwa na tabia nzuri yenye kumkinga na kutumbukia kwenye fitina na hali zenye utata. Ni jambo lisilokuwa na shaka yoyote kwamba katika aina kubwa za kuwa na haya na kujiheshimisha ni pamoja na yeye kujisitiri ikiwa ni pamoja vilevile na kufunika uso wake kwa kuwa limnamlinda na kumkinga na kutumbukia kwenye fitina.
Hapo kabla watu katika mji huu uliobarikiwa - mji wa Wahyiy, ujumbe, haya na heshima - walikuwa ni wazuri katika suala hili. Wanawake walikuwa wakitoka wakiwa na Jilbaab, mbali kabisa na wanaume. Hali bado ni yenye kuendelea hivo katika miji mingi ya kifalme na himdi zote ni Zake Allaah. Lakini pale baadhi ya watu walipozungumzia juu ya Hijaab, kuwatazama wale wasiofanya hivo na kuonelea kuwa ni sawa kwa mwanamke kuonesha uso, ndipo baadhi ya watu wakaanza kutilia shaka Hijaab na kama ni wajibu kufunika uso au imependekezwa. Au ni jambo tu ambalo ni la kimila na kidesturi na sio wajibu wala haikupendekezwa?
Ili kuondoa shaka hii na kubainisha uhakika wa mambo ndipo nikapendelea kuandika yenye kuweka wazi hukumu kwa kutaraji ya kwamba Allaah (Ta´ala) ataifanya iweke haki wazi na kutufanya sisi ni wenye kuongoka na kuiona haki na kuifuata na batili na kuiepuka. Hivyo basi, ninamuomba Allaah mafanikio na kusema:
Enyi waislamu! Tambueni ya kwamba mwanamke kujisitiri na kuufunika uso wake mbele ya wanaume ajinabi ni jambo la wajibu. Uwajibu wake unatolewa dalili na Kitabu cha Mola Wako (Ta´ala), Sunnah za Mtume Wako (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na mtazamo sahihi.

 
2. Kufunika uso kunachangia kuhifadhi tupu

Miongoni mwa dalili za Qur-aan ni:
1- Kauli ya Allaah (Ta´ala):
وَقُل لِّلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ وَيَحْفَظْنَ فُرُوجَهُنَّ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا ۖ وَلْيَضْرِبْنَ بِخُمُرِهِنَّ عَلَىٰ جُيُوبِهِنَّ ۖ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا لِبُعُولَتِهِنَّ أَوْ آبَائِهِنَّ أَوْ آبَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ أَبْنَائِهِنَّ أَوْ أَبْنَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي أَخَوَاتِهِنَّ أَوْ نِسَائِهِنَّ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُنَّ أَوِ التَّابِعِينَ غَيْرِ أُولِي الْإِرْبَةِ مِنَ الرِّجَالِ أَوِ الطِّفْلِ الَّذِينَ لَمْ يَظْهَرُوا عَلَىٰ عَوْرَاتِ النِّسَاءِ ۖ وَلَا يَضْرِبْنَ بِأَرْجُلِهِنَّ لِيُعْلَمَ مَا يُخْفِينَ مِن زِينَتِهِنَّ ۚ وَتُوبُوا إِلَى اللَّـهِ جَمِيعًا أَيُّهَ الْمُؤْمِنُونَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ
"Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao na wahifadhi tupu zao na wala wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa yale yanayodhihirika [kwa kuwa hakuna njia ya kuyaficha]; hivyo waangushe khimari zao mpaka vifuani mwao. Na wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa kwa waume zao, baba zao, baba za waume wao, wana wao wa kiume, wana wa kiume wa waume zao, kaka zao, wana wa kiume wa kaka zao, wana wa kiume wa dada zao, wanawake wao [dada zao wa Kiislamu], wale iliyowamiliki mikono yao ya kuume, watumishi wanaume wasio na matamanio [tena kwa wanawake], au watoto ambao [bado] hawaelewi [kitu kuhusu] yanayohusu uke. Na wala wasipige miguu yao [wanapotembea] yajulikane yale wanayoyaficha katika mapambo yao. Na tubuni kwa Allaah nyote, enyi Waumini ili mpate kufaulu!"
Dalili katika Aayah hii yenye kuonesha kuwa ni wajibu kwa mwanamke kufunika uso wake mbele ya wanaume ajinabi ni ifuatayo:
Ya kwanza: Allaah (Ta´ala) amewaamrisha waumini wanawake kuhifadhi tupu zao. Kile kilichoamrishwa kinaamrisha vilevile kile chenye kupelekea katika hilo. Hakuna mtu yeyote mwenye akili timamu anashaka juu ya kwamba kufunika uso kunachangia kuhifadhi tupu. Kwa sababu kuonesha uso kunapelekea wanaume kuutazama, kuangalia uzuri wake na kuburudika nao. Hilo [hatimae] linapelekea katika hili la lile. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:
"Macho yanazini na kuzini kwake ni kule kuangalia... " mpaka aliposema: "... na tupu ima inasadikisha hilo au kulikadhibisha."

 
3. Uzuri wa mwanamke uko usoni

Ya pili: Allaah Amesema:
وَلْيَضْرِبْنَ بِخُمُرِهِنَّ عَلَىٰ جُيُوبِهِنَّ
"... hivyo waangushe khimari zao mpaka vifuani mwao."
Khimari ni vazi ambalo mwanamke anafunika kichwa chake. Ikiwa ameamrishwa kufunika kifua basi vilevile ameamrishwa kufunika uso. Hilo linafanywa ima ni kwa sababu ni jambo ambalo lisiloweza kuepukwa au kwa sababu ya kipimo [Qiyaas]. Ikiwa ni wajibu kufunika kifua na matiti basi ni jambo la wajibu zaidi kufunika uso ambapo ni sehemu ya uzuri na fitina. Wale ambao wanachotaka ni uzuri wanacholenga huwa ni uso. Uso ukiwa mzuri hawatilii umuhimu mkubwa kitu kingine. Pindi inaposemwa kuwa mwanamke fulani ni mzuri mtu anacholenga huwa ni uso wake. Ni jambo lenye kuonyesha ya kwamba uso ndio mahala uzuri ulipo kwa njia zote. Vipi basi mtu atafikiria kuwa Shari´ah hii yenye hekima imeamrisha kufunika kifua na kuacha uso ukaonekana?
 
4. Uso ni mapambo yasiyotakikana kuonekana

Ya tatu: Allaah (Ta´ala) amekataza kabisa kuonesha mapambo isipokuwa yale yasiyoweza kufichikana kama mavazi ya nje. Ndio maana Amesema:
إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا
"... isipokuwa yale yanayodhihirika..."
Hakusema "... isipokuwa yale wanayodhihirisha...". Kisha akakataza kuonesha mapambo kwa mara nyingine na akawachomoa wale wanaume wanaofaa kuyaona. Hili linathibitisha ya kwamba mapambo ya pili yanatofautiana na mapambo ya kwanza. Mapambo ya kwanza ni ya nje yenye kuonekana na watu wote na ambayo hakuna uwezekano wa kuyaficha. Mapambo ya pili ni yenye kufichikana ambayo anajipamba nayo. Lau mapambo haya ya pili ingelikuwa inajuzu kwa watu wote kuyaona basi kungelikuwa hakuna maana yoyote yenye kujulikana ya kufanya ujumla katika ile hali ya kwanza na umaalum katika ile hali ya pili.

 
5. Fitina iko usoni kwa mwanamke

Ya nne: Allaah (Ta´ala) amemrukhusu mwanamke kuonesha mapambo yake yenye kufichikana kwa mtumishi mwanaume asiyekuwa tena na matamanio kwa wanawake na mtoto ambaye bado hajaelewa kitu kuhusiana na uke. Hili linatolea dalili kuonyesha mambo mawili:
1-Mapambo yenye kufichikana hayatakiwi kuonekana kwa wanaume ajinabi isipokuwa watu hawa aina mbili.
2- Hukumu hii inatokamana na khatari ya fitina kwa mwanamke. Ni jambo lisilokuwa na shaka yoyote kuwa uzuri na fitina iko usoni. Hivyo inakuwa ni wajibu kuufunika mbele ya wanaume wenye matamanio kwa wanaume.

 
6. Uso wa mwanamke ni wenye fitina zaidi kuliko sauti ya mnyororo wake

Ya tano: Allaah (Ta´ala) amesema:
وَلَا يَضْرِبْنَ بِأَرْجُلِهِنَّ لِيُعْلَمَ مَا يُخْفِينَ مِن زِينَتِهِنَّ
"Na wala wasipige miguu yao [wanapotembea] yajulikane yale wanayoyaficha katika mapambo yao."
Hii ina maana ya kwamba haitakiwi kwa mwanamke kupiga miguu wanaume wakaja kujua kuwa amevaa minyororo na mapambo mengine. Ikiwa mwanamke amekatazwa kupiga miguu ili asije akawafitinisha wanaume kwa sauti ya minyororo na mengineyo, basi ni jambo lililo la khatari zaidi kwa uso uliofunuliwa. Ni kipi kilicho na fitina na kuvutia zaidi mwanaume kusikia sauti ya mnyororo wa mwanamke asiyejua kama ni kijana au mzee, mbaya au mzuri, au kuona uso wake uliofunuliwa, mzuri, mwembamba, wenye kung´aa na mzuri? Wanaume wote wenye kuvutikiwa na wanawake wanajua ni kipi chenye fitina zaidi na kilicho muhimu zaidi kufunikwa na kufichikwa.

 
7. Tofauti ya mwanaume mtu mzima na kijana

2- Kauli ya Allaah (Ta´ala):
وَالْقَوَاعِدُ مِنَ النِّسَاءِ اللَّاتِي لَا يَرْجُونَ نِكَاحًا فَلَيْسَ عَلَيْهِنَّ جُنَاحٌ أَن يَضَعْنَ ثِيَابَهُنَّ غَيْرَ مُتَبَرِّجَاتٍ بِزِينَةٍ ۖ وَأَن يَسْتَعْفِفْنَ خَيْرٌ لَّهُنَّ ۗ وَاللَّـهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ
"Na wanawake, ambao hawapati tena hedhi na ambao hawataraji kuolewa, basi hakuna lawama yoyote kwao wakikhafifisha kitu katika baadhi ya nguo zao, bila ya kuibusha mapambo ya kike. Na kama wakijisitiri [kwa kujifunika vyema] ni bora kwao. Na Allaah ni Mwenye kusikia yote, Mjuzi wa yote."
Kusudio katika Aayah hii ni kwamba Allaah anasema kuwa wanawake watu wazima, ambao hawataraji kuolewa kwa sababu wanaume hawavutiki nao kutokana na ukubwa wa umri wao, hawapati dhambi lau watakhafifisha mavazi midhali hawakusudii kujishaua kwa kuonyesha mapambo yao. Bila ya shaka Aayah haikusudii wavue mavazi kiasi cha kwamba wabaki hali ya kuwa uchi. Aayah inakusudia vazi linalowekwa juu ya kanzu na mfano wake ambalo asli linaonyesha tu uso na vitanga vya mikono. Mavazi wanayofaa kuvua ni yale yenye kuufunika mwili mzima. Kwa vile Aayah inawahusu wanawake watu wazima tu, hiyo ina maana ya kwamba wanawake vijana ambao bado wanataraji kuolewa hawana hukumu moja. Lau hukumu ingelikuwa inawagusa wote, basi kungelikuwa hakuna faida yoyote ya kuwalenga wanawake watu wazima. Vilevile isitoshe Allaah (Ta´ala) anasema:
غَيْرَ مُتَبَرِّجَاتٍ بِزِينَةٍ
"... bila ya kuibusha mapambo ya kike."
Ni dalili nyingine yenye kuonesha kuwa ni wajibu kwa mwanamke kijana ambaye anataraji kuolewa kujisitiri. Mwanamke anapoonyesha uso wake mara nyingi hutaka kuonesha mapambo na uzuri wake ili wanaume waweze kumsifu na mfano wa hayo. Wanawake wasiofikiria hivo ni nadra na nadra haina hukumu.

 
8. Wanawake bora zaidi walikuwa wakijifunika nyuso zao

3- Kauli ya Allaah (Ta´ala):
يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَاءِ الْمُؤْمِنِينَ يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِن جَلَابِيبِهِنَّ ۚ ذَٰلِكَ أَدْنَىٰ أَن يُعْرَفْنَ فَلَا يُؤْذَيْنَ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا
"Ee Nabii! Waambie wake zako na mabinti zako - na wanawake [wote] wa Waumini - ya kwamba [nje ya nyumbani] wajiteremshie mavazi yao ya juu; hivyo kunapeleka karibu zaidi watambulikane [kuwa ni wanawake wa heshima] na wasiudhiwe. Na Allaah ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu."
Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:
"Allaah amewaamrisha wanawake pindi wanapotoka majumbani wafunike nyuso zao kwa mavazi yao ya juu na waoneshe jicho moja tu."
Tafsiyr ya Swahabah ni hoja. Kuna wanachuoni waliyofikia mpaka kusema kuwa ina hukumu moja kama ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kauli yake (Radhiya Allaahu ´anh) "... na waoneshe jicho moja tu" ni kwa sababu tu amelazimika kuona njia. Ama ikiwa hana haja hiyo, hafai hata kuonesha jicho hilo. Mavazi ya juu, Jilbaab, ni yale yanayowekwa juu ya kichwa. Umm Salamah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema baada ya kuteremka Aayah hii:
"Wanawake wa Answaar walitoka walikuwa watulivu kana kwamba kunguru amekaa juu ya vichwa vyao. Walikuwa wamevaa mavazi ya juu meusi."
´Abiydah as-Salmaaniy na wengine wameeleza jinsi wanawake waumini walivokuwa na mavazi yao juu ya vichwa vyao ili kusionekana chochote zaidi ya macho yao tu kwa ajili ya njia.

 
9. Ni wajibu kwa mwanamke ajifunike mbele ya wanaume ajinabi

4- Kauli ya Allaah (Ta´ala):
لَّا جُنَاحَ عَلَيْهِنَّ فِي آبَائِهِنَّ وَلَا أَبْنَائِهِنَّ وَلَا إِخْوَانِهِنَّ وَلَا أَبْنَاءِ إِخْوَانِهِنَّ وَلَا أَبْنَاءِ أَخَوَاتِهِنَّ وَلَا نِسَائِهِنَّ وَلَا مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُنَّ ۗوَاتَّقِينَ اللَّـهَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدًا
"Si jambo lenye kulaumika juu yao [endapo watazungumza wazi wazi na] baba zao na watoto wao wa kiume na kaka zao na watoto wa kiume wa kaka zao na watoto wa kiume wa dada zao na wanawake wenzao [wa Kiislamu] na iliyowamiliki mikono yao ya kulia. Na mcheni Allaah [enyi wanawake wote]! Hakika Allaah juu ya kila kitu ni Mwenye kushuhudia." 
Ibn Kathiyr (Rahimahu Allaah) amesema:
"Wakati Allaah alipoamrisha wanawake kujifunika mbele ya wanaume ajinabi akabainisha kuwa sio wajibu kufanya hivo na wale ndugu ambao amewavua katika Suurat-un-Nuur pindi aliposema:
وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا لِبُعُولَتِهِنَّ أَوْ آبَائِهِنَّ أَوْ آبَاءِ بُعُولَتِهِنَّ
"Na wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa kwa waume zao, baba zao, baba za waume wao..."
Aayah hizi tukufu nne zinawajibisha kwa mwanamke kujifunika mbele ya wanaume ajinabi na ile Aayah ya kwanza ina nukta tano.
10. Cha kwanza mchumbiaji huangalia huwa ni uso

Miongoni mwa dalili za Sunnah ni:
1- Kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):
"Mmoja wenu akimchumbia mwanamke hakuna neno akamwangalia pasina yeye kujua ikiwa kama anamwangalia ili amchumbie."
Ameipokea Ahmad. al-Haythamiy amesema katika "Majma´-uz-Zawaa´id":
"Wanaume wake ni wanaume Swahiyh."
Kinacholengwa ni kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kuwa sio dhambi kwa mchumbiaji peke yake kumwangalia yule anayefikiria kumuoa ikiwa malengo ni kutaka kumchumbia. Ni dalili inayoonesha kuwa ni haramu kwa hali yoyote kwa yule asiyefikiria kuchumbia. Hali kadhalika ikiwa mchumbiaji hana nia ya kuchumbia isipokuwa anamwangalia kwa sababu tu ya kutaka kuburudika na mfano wa hayo.
Huenda mtu akasema Hadiyth haikuweka wazi ni kipi cha kuangalia; inawezekana ikawa ni kifua na matiti. Pamoja na hivyo kila mtu ni mwenye kujua kwamba anacholenga mchumbiaji ni uzuri wa uso. Aghlabu vinginevyo huwa si lengo. Mchumbiaji hutazama uso. Ni jambo lisilokuwa na shaka mwenye kutaka uzuri anacholenga huwa ni uso.

 
11. Haijuzu kwa mwanamke kutoka kwenda mahala pa kuswalia bila ya mavazi ya juu

2- Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipoamrisha wanawake kutoka kwenda mahala pa kuswalia Idi, alisema:
"Ee Mtume wa Allaah! Baadhi yetu hawana mavazi ya juu ya kutokea?" Akasema: "Dada yake amvishe moja katika mavazi yake ya juu."
Ameipokea al-Bukhaariy, Muslim na wengine.
Hadiyth hii dalili inayoonyesha kuwa iliwa ni katika mazowea ya wanawake wa Maswahabah kutotoka isipokuwa kwa mavazi ya juu na ikiwa hana hatoki. Ndio maana (Radhiya Allaahu ´anhunn) wakamtajia kizuizi hichi pindi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipowaamrisha kutoka kwenda mahala pa kuswalia Idi wakati wa Idi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawatatulia tatizo hili, waazime kutoka kwa kina dada. Pamoja na hivyo hakuwaacha wakatoka  bila ya mavazi ya juu hata kama imewekwa katika Shari´ah na kuamrishwa kwa wanaume na wanawake kutoka na kwenda mahapa pa kuswalia Idi. Ikiwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuwaacha wakatoka bila ya mavazi ya juu kwa kitu ambacho kimeamrishwa, ni vipi angeliwaacha wakatoka bila ya mavazi ya juu na kwenda kwa kitu ambacho hakikuamrishwa wala kisichokuwa na haja kama mfano wa masoko na kuchanganyika na wanaume na kuangalia mambo yasiyokuwa na faida. Kuamrishwa kwa mavazi ya juu ni jambo lenye kutolea dalili kuonyesha kuwa ni wajibu kwa mwanamke kujifunika na Allaah ndiye anajau zaidi.

 
12. Wanawake wa kwanza walikuwa wakijifunika wanapotoka majumbani

3- Imethibiti katika al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye amesema:
"Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiswali Fajr na wanawake wa waumini wakiswali pamoja naye, wamejigubika mavazi yao. Wanapoenda nyumbani hakuna yeyote awezae kuwajua kwa sababu ya giza." 
Amesema (Radhiya Allaahu ´anhaa) pia:
"Lau Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) angeliona kwa wanawake yale tunayoyaona sisi, basi angeliwakataza kwenda misikitini kama jinsi Banuu Israaiyl walivyowakataza wanawake wao."
´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amepokea mfano wake. Kinacholengwa katika Hadiyth hii ni kifuatacho:
Kwanza: Wanawake wa Maswahabah, ambao walikuwa ni karne bora, walikuwa na ada ya kujisitiri na kujifunika. Wao ni karne tukufu zaidi, bora na kamilifu mbele ya Allaah inapokuja katika tabia, adabu, imani na matendo. Wao ni viigizo. Allaah awawie radhi na wale wenye kuwaiga. Allaah (Ta´ala) amesema:
السَّابِقُونَ الْأَوَّلُونَ مِنَ الْمُهَاجِرِينَ وَالْأَنصَارِ وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَانٍ رَّضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ وَأَعَدَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي تَحْتَهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ۚ ذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ
"Na wale waliotangulia awali, miongoni mwa Muhaajiriyn [waliohajiri kutoka Makkah] na Answaar [wakaazi wa al-Madiynah waliowasaida], na wale waliowafuata kwa wema - Allaah Ameridhika nao nao wameridhika Naye: Amewaandalia mabustani ipitayo chini yake mito, humo [watakuwa] ni wenye kudumu milele. Huko ndiko kufuzu kukuu."
Ikiwa hayo ndio yalikuwa matendo ya Maswahabah, mtu anaweza kujiuliza ni vipi inaweza kutustahikia kwenda kinyume na njia ambayo Allaah (Ta´ala) ameridhika nayo. Allaah (Ta´ala) amesema:
وَمَن يُشَاقِقِ الرَّسُولَ مِن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُ الْهُدَىٰ وَيَتَّبِعْ غَيْرَ سَبِيلِ الْمُؤْمِنِينَ نُوَلِّهِ مَا تَوَلَّىٰ وَنُصْلِهِ جَهَنَّمَ ۖ وَسَاءَتْ مَصِيرًا
"Na yule atakayempinga Mtume baada ya kuwa imeshambainikia uongofu na akaifuata njia isiyokuwa ya waumini; hyuo Tutamgeuza alikogeukia na Tutamuingiza Motoni - na ubaya ulioje marudio ya mwisho!"
Pili: Mama wa waumini ´Aaishah na ´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anhumaa) - wenye kujulikana kwa elimu, uelewa na umaizi uliyobobea katika dini ya Allaah na kuwatakia mema waja Wake - wameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) angeliwakataza wanawake kwenda misikitini lau angeliona yale wanayoyaona. Hali ilibadilika kiasi kikubwa katika masiku ya karne bora ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), mpaka kufikia kuwakataza wanawake kwenda misikitini. Vipi tusemeje leo baada ya miaka elfu moja na mia nne? Mambo yamezidi kuwa mabaya, haya imekuwa ndogo zaidi na dini dhaifu na dhaifu kwenye mioyo ya watu wengi.
Kutokana na ukamilifu wa Shari´ah ´Aaishah na Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anhumaa) wakafahamu kuwa kila kinachopelekea katika uharamu nacho pia haramu.
 
13. Ni wajibu kwa mwanamke kufunika miguu yake anapotoka nyumbani

4- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:
"Allaah hatomwangalia mtu mwenye kuburuta mavazi yake kwa kiburi." Umm Salamah akasema: "Wanawake wafanye nini na viburuta vyao?" Akasema: "Wafanye iwe shibri moja." Akasema: "Miguu yao itaonekana." Ndipo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: "Wafanye iwe dhiraa moja na wasizidishe."
Hadiyth hii inatolea dalili kuonyesha kuwa ni wajibu kwa mwanamke kufunika miguu yake, jambo ambalo lilikuwa linajulikana kwa wanawake wa Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum). Ni jambo lisilokuwa na shaka kuwa miguu ni yenye fitina kidogo kuliko uso na vitanga vya mikono. Uzinduzi juu ya kidogo kwa dhati yake ni uzinduzi juu ya kikubwa. Shari´ah yenye hekima haiwezi kuwajibisha kitu kilicho na fitina kidogo kufunikwa na kuruhusu kilicho na fitina kidogo kuonyeshwa. Ni mgongano usiyowezekana kwa hekima na Shari´ah ya Allaah.

 
14. Mwanamke anaruhusiwa kuonesha uso mtumwa wake

5- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:
"Ikiwa mmoja wenu [wanawake] ana mtumwa mwenye kulipa kwa ajili ya kutaka kujiacha huru, basi ajisitiri mbele yake."
Imepokelewa na watano isipokuwa ni an-Nisaa´iy na ni Swahiyh kwa mujibhu wa at-Tirmidhiy.
Chenye kulengwa katika Hadiyth hii kwamba mmiliki mwanamke anaruhusiwa kuonesha uso wake kwa mtumwa wake midhali bado anammiliki. Pale tu ambapo anakuwa huru basi ni wajibu kwake kujisitiri kwa sababu mtumwa huyo amekuwa ni ajinabi kwake. Ni dalili yenye kuonesha kuwa mwanamke ni wajibu kujifunika mbele ya mwanaume ajinabi.

 
15. Wajibu tu ndio iwezayo kuitikisa wajibu nyingine

6- ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:
"Wapanda farasi wanaume walikuwa wakitupitia na sisi tuko kwenye Ihraam pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wanapotujongelea, kila mmoja wetu anateremsha mavazi yake ya juu, Jilbaab, usoni mwake. Wanapokuwa wameshapita, tunajifunua tena."
Ameipokea Ahmad, Abu Daawuud na Ibn Maajah.
Katika maneno yake "Wanapokuwa wameshapita, tunajifunua tena" kuna dalili yenye kuonesha kuwa ni wajibu kufunika uso. Kwa sababu imewekwa katika Shari´ah kufunua uso katika Ihraam. Lau kusingelikuwepo kizuizi kikubwa kungelibaki kuwa ni wajibu kuufunua uso. Mwanamke kufunua uso katika Ihraam ni wajibu kwa mujibu wa wanachuoni wengi. Lililo la wajibu linaweza kutikiswa tu na la wajibu lingine. Lau isingelikuwa ni wajibu kufunika uso mbele ya wanaume ajinabi, basi isingeliruhusiwa kuufunika katika Ihraam. Imethibiti katika al-Bukhaariy, Muslim na wengine ya kuwa hairuhusiwi kwa mwanamke mwenye kuhirimia kuvaa Niqaab wala vifuniko vya mikono . Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:
"Hili linaonyesha kuwa Niqaab na vifuniko vya mikono ilikuwa ni mambo yenye kujulikana kwa wanawake mbali na Ihraam, jambo lenye kupelekea kufunika nyuso zao na mikono yao."
Dalili hizi sita ni zenye kuonesha kuwa ni wajibu kwa mwanamke kujisitiri na kufunika uso wake mbele ya wanaume ajinabi. Tukiongezea juu yake na zile dalili nne za Qur-aan inakuwa dalili kumi.

 
16. Mwanamke kuonesha uso wake kuna madhara zaidi kuliko manufaa

Dalili ya kumi na moja ni mtazamo sahihi na kipimo imara kilichokuja na Shari´ah hii yenye hekima. Nacho kinatokamana na kuhakikisha manufaa na kila chenye kupelekea na kuita katika manufaa hayo na kukataza madhara na kila chenye kupelekea katika madhara hayo na kuyakemea. Kila ambacho aidha kina manufaa matupu au manufaa yenye uzito zaidi kuliko madhara basi ima ni wajibu au kimependekezwa. Na kila ambacho aidha kina madhara matupu au madhara yenye uzito zaidi kuliko manufaa basi ima ni haramu au kimechukizwa.
Tukiangalia [suala la] mwanamke kufunua uso wake mbele ya wanaume ajinabi, basi tutapata madhara mengi. Ikiwa kutapatikana manufaa fulani, basi ni madogo na yanashinda manufaa. Baadhi ya madhara yanapatikana ifuatavyo:

 
17. Mwanamke kuonesha uso wake kunepelekea katika fitina

Tukiangalia [suala la] mwanamke kufunua uso wake mbele ya wanaume ajinabi, basi tutapata madhara mengi. Ikiwa kutapatikana manufaa fulani, basi ni madogo na yanashinda manufaa. Baadhi ya madhara yanapatikana ifuatavyo:

1- Fitina. Mwanamke hujifitinisha mwenyewe pindi anapojipamba uso wake na hujionyesha katika muonekano wenye kufitinisha. Hii ni moja ya sababu kubwa ya shari na ufisadi.
 
 
18. Mwanamke kuonesha uso wake kunamwondosha haya

2- Kuodoka kwa haya. Mwanamke haya yake humtoka ambayo ni sehemu katika imani na maumbile yake yanayotakikana. Mwanamke alikuwa akitolewa methali wakati kunapotajwa haya. Ilikuwa inasemwa:
"Ana haya zaidi kuliko bikira kwenye chumba chake."
Wakati haya inapomtoka mwanamke imani yake hupungua na kadhalika hupoteza maumbile yake aliyoumbwa kwayo.

 
19. Mwanamke kuonesha uso kunamfitinisha mwanaume

3- Wanaume wanatiwa kwenye mtihani na khaswa ikiwa ni mwanamke mzuri mwenye kuvutia, kucheka na kutupia macho huku na kule. Inasemwa kuwa jicho linapelekea katika salamu, salamu inapelekea katika maongezi, maongezi yanapelekea katika makubaliano na makubaliano yanapelekea katika kukutana. Shaytwaan hutembelea kwenye [mwili wa] binaadamu kama damu. Ni mara ngapi maneno, kicheko na furaha inamfanya mwanaume kudata kwa mwanamke au mwanamke kwa mwanaume ambapo hatimae kunatokea maovu yasiyoepukika! Tunamuomba Allaah afya.


 
20. Mwanamke kuonesha uso wake kunapelekea katika mchanganyiko

4- Wanawake kuchanganyika na wanaume. Pindi mwanamke anapoona kuwa ni kama mwanaume kwa kuonesha uso, hatoogopa kuchanganyika na kusongamana na wanaume. Hilo lina fitina kubwa ndani yake na ufisadi wenye kuenea. Siku moja wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipotoka msikitini akaona wanaume wako pamoja na wanawake njiani. Hivyo akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwaambia wanawake:
"Tokeni. Hakika hamna haki ya kutembea kati kati ya njia. Tembeeni pembezoni mwa njia."
Ndipo wanawake wakaanza kutembea pembezoni kabisa na kuta mpaka mavazi yao yakagusana nazo. Haya yametajwa na Ibn Kathiyr wakati wa kufasiri Kauli ya Allaah (Ta´ala):
وَقُل لِّلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ
"Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao... "
 Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema kuwa ni wajibu kwa wanawake kujifunika mbele ya wanaume ajinabi. Amesema:
"Allaah amegawanya mapambo sehemu mbili; mapambo yenye kuonekana na mapambo yasiyoonekana. Inajuzu kwa mwanamke kuonesha mapambo yake yenye kuonekana wanaume mbali na mume wake na ndugu wasiyoweza kumuuoa. Kabla ya Aayah yenye kuamrisha kujificha, Hijaab, wanawake walikuwa wakitoka bila ya mavazi ya juu. Wanaume walikuwa wanaweza kuona nyuso na mikono yao. Kipindi hicho ilikuwa bado inajuzu kuonesha uso na vitanga vya mikono na ilikuwa inajuzu kumtazama kwa vile ilikuwa inajuzu kwake kuonesha uso. Wakati Allaah alipoteremsha:
يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَاءِ الْمُؤْمِنِينَ يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِن جَلَابِيبِهِنَّ
"Ee Nabii! Waambie wake zako na mabinti zako - na wanawake [wote] wa Waumini - ya kwamba [nje ya nyumbani] wajiteremshie mavazi yao ya juu."
wanawake wakajifunika kwa wanaume."
Kisha akasema:
"Mavazi ya juu, Jilbaab, ni ile ambayo Ibn Mas´uud na wengine wanaita "mavazi ya kutia juu". ´Awwaam wanaita kuwa ni "pazia". Ni pazia kubwa inayofunika kichwa na mwili mzima. Ikiwa waliamrishwa kuvaa mavazi ya juu ili wasijulikane, hiyo ina maana uso unatakiwa kufunikwa au kuvishwa Niqaab, hivo ina maana ya kuwa uso na mikono ni katika mapambo ambayo hayatakiwi kuoneshwa mbele ya wanaume ajinabi. Mengineyo katika mavazi ya juu wanaume wanaweza kuona. Ibn Mas´uud ametaja suala la pili na Ibn ´Abbaas ametaja suala la kwanza."
Kisha akasema:
"Kutokana na kauli sahihi ni kwamba hairuhusiwi kwa mwanamke kuonesha uso, mikono na miguu mbele ya wanaume ajinabi. Hata hivyo kabla ya kufuta ilikuwa inaruhusiwa kwake kuvionesha. Hivi sasa hakuna anachoruhusiwa kuonesha isipokuwa nguo tu." 
Kwenye mjaladi huo huo amesema:
"Ama kuhusu uso, mikono na miguu, haruhusiwi tu kuvionesha wanaume ambao ni ajinabi. Hata hivyo anaruhusiwa kuwaonesha wanawake na ndugu wanaume wasioweza kumuoa."
Amesema pia:
"Msingi wa hili ni kwamba unajua kuwa Shari´ah iko na malengo mawili:
1- Kutofautisha kati ya wanaume na wanawake
2- Kumfunika mwanamke."
Haya ni maneno ya Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah. Kuhusiana na maneno ya Hanaabilah, nitataja maoni ya wanachuoni waliokuja nyuma. Mwandishi wa "al-Muntahaa" amesema:
"Ni haramu kwa mwanaume mhasi au mtowashi kumtazama mwanamke ajinabi."
Kwenye kitabu "al-Iqnaa´" kuna:
"Ni haramu kumtazama mwanamke huru na ni haramu kutazama nywele zake."
Mwandishi wa "ad-Daliyl" amesem:
"Kutazama kuna aina nane. Ya kwanza ni mwanaume ambaye kishabaleghe, hata kama ni mtowashi, kumtazama mwanamke ajinabi pasina haja. Haijuzu kwake kutazama chochote kwake, hata nywele zake za bandia."
Shaafi´iyyah wanasema namna hii:
"Ikiwa ni mtazamo wa matamanio au kunakhofiwa fitina, basi ni haramu kabisa. Hakuna tofauti yoyote juu ya hilo. Na ikwia mtazamo sio wa matamanio na hakukhofiwi fitina yoyote, kuna kauli mbili juu ya suala hili. Zimetajwa na mwandishi wa kitabu "Sharh-ul-Iqnaa´" ambaye amesema:
"Kauli sahihi ni kuwa ni haramu kama ilivyotajwa katika "al-Minhaaj" na asli yake. Maimamu kwa makubaliano ya waislamu wote wamesema kuwa haipaswi kwa wanawake kutoka uso wazi na kwamba kutazama kunapelekea katika fitina na kuamsha matamanio."
Allaah (Ta´ala) amesema:
وَقُل لِّلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ
"Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao... "
Katika mazuri ya Shari´ah imekuja kuzuia kila ambacho kinapelekea katika madhara na mbali na hali zilizofafanuliwa."
Katika kitabu "Nayl-ul-Awtwaar" mna:
"Waislamu wamekubaliana juu ya kwamba hairuhusiwi kwa wanawake kutoka nyuso wazi na khaswa pale ambapo madhambi ni mengi."

21. Dalili juu ya kwamba inajuzu kwa mwanamke kuonesha uso

Nijuavyo ni kuwa wale wenye kujuzusha mwanaume kumwangalia mwanamke ajinabi na mikono yake hawana dalili kutoka katika Qur-aan na Sunnah isipokuwa zifuatazo:
1- Kauli ya Allaah (Ta´ala):
وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا لِبُعُولَتِهِنَّ
"... na wala wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa yale yanayodhihirika [kwa kuwa hakuna njia ya kuyaficha]... "
Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:
"Bi maana uso, vitanga vya mikono na pete."
Imepokea al-A´mash kutoka kwa Sa´iyd bin Jubayr kutoka kwake. Tafsiri ya Swahabah ni hoja kama tulivyotangulia kusema.
2- Abu Daawuud amepokea katika "as-Sunan" yake kutoka kwa ´Aiashah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ya kwamba Asmaa´ bint Abiy Bakr (Radhiya Allaahu ´anhumaa) aliingia kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na alikuwa amevaa mavazi ya kubana ambapo Mtume akageuka na kusema:
"Ee Asmaa´! Wakati mwanamke anapobaleghe hatakiwi kuonesha chochote isipokuwa hiki na hiki" na akaashiria uso na vitanga vyake vya mikono."
3- al-Bukhaariy na wengine wamepokea kutoka kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) jinsi kaka yake al-Fadhwl alivokuwa amekaa kwenye mnyama nyuma ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati wa Hajj ya kuaga. Pindi mwanamke kutoka Khath´am alipokuja akaanza kumtazama na yeye [mwanamke huyo] anamtazama. Hivyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akageuza uso wake upande mwingine . Katika hili kuna dalili kuwa mwanamke alionesha uso wake.
4- al-Bukhaariy na wengine wamepokea kutoka kwa Jaabir bin ´Abdillaah (Radhiya Allaahu ´anhumaa) juu ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwaswalisha kwake watu swalah ya idi na akawapa mawaidha na kuwakumbusha kisha akaenda kwa wanawake akawapa mawaidha na kuwakumbusha. Akasema:
"Enyi wanawake! Toeni swadaqah! Hakika nyinyi ndio wengi Motoni." Ndipo akasimama mmoja katika wanawake bora na alikuwa na mashavu ya kupauka... "
Lau uso wake ungelikuwa hauko wazi basi mtu asingelijua ana mashavu ya kupauka.
Nijuavyo ni kwamba hizi ndio dalili kuwa inajuzu kwa mwanamke kuonesha uso wake wanaume ajinabi.


 
22. Dalili za kujifunika ni zenye kutangulizwa juu ya dalili za kujifunua

Lakini hata hivyo dalili hizi hazigongani na dalili zenye kuwajibisha Hijaab kwa njia nyingi ikiwa ni pamoja na:
Mosi: Dalili za kujifunika ni zenye kutoka kwenye kianzio wakati dalili zenye kujuzisha kujifunua ziko katika kianzio. Zenye kutoka kwenye kianzio zinapewa kipaumbele juu ya ambazo ziko katika kianzio. Hilo ni kwa sababu kilichoko katika kianzio kinahusiana na kitu kubaki kama jinsi kilivyokuwa. Kunapokuja dalili juu ya kitu chenye kutanua zaidi kutoka kwenye kianzio, basi hiyo ina maana kuwa hukumu ya kianzio imebadilika. Ndio maana tunasema kile chenye kutanua zaidi kutoka kwenye kianzio ni elimu zaidi yenye kuthibitisha ya kuwa ile hukumu asili imebadilika - yenye kuthibitisha ni yenye kupewa kipaumbele juu yenye kupinga.
Mtazamo huu ni wa jumla na imara hata kama itahusiana na dalili zilizo na nguvu sawa kutokana na kuthibiti kwake na ushahidi.

 
23. Tafsiri ya maneno ya Ibn ´Abbaas

Pili: Tukizingatia dalili zenye kujuzisha kujifunua basi tutaona ambavyo hazina nguvu sawa na zile zenye kukataza. Yanabainika ifuatavyo:
1- Tafsiri ya Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) inaweza kufasiriwa kwa njia tatu:
Ya kwanza: Inawezekana alisema hivo kabla ya Aayah yenye kuamrisha kujifunika kuteremshwa, kama jinsi nilivyomnukuu karibuni Shaykh-ul-Islaam akisema.
Ya pili: Inawezekana anacholenga ni yale mapambo ambayo ni haramu kuonesha, kama jinsi alivyosema Ibn Kathiyr katika Tafsiyr yake. Kinachosapoti uwezekano huu ni tafsiri yake (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ya Aayah:
يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَاءِ الْمُؤْمِنِينَ يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِن جَلَابِيبِهِنَّ ۚ ذَٰلِكَ أَدْنَىٰ أَن يُعْرَفْنَ فَلَا يُؤْذَيْنَ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا
"Ee Nabii! Waambie wake zako na mabinti zako - na wanawake [wote] wa Waumini - ya kwamba [nje ya nyumbani] wajiteremshie mavazi yao ya juu; hivyo kunapeleka karibu zaidi watambulikane [kuwa ni wanawake wa heshima] na wasiudhiwe. Na Allaah ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu."
Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:
"Allaah amewaamrisha wanawake pindi wanapotoka majumbani wafunike nyuso zao kwa mavazi yao ya juu na waoneshe jicho moja tu."
Ya tatu: Lau tutasema kuwa hakumaanisha si cha kwanza wala cha pili, tafsiri yake si hoja ikiwa Swahabah mwingine anasema kitu kingine. Ikiwa Swahabah mwingine ana kauli nyingine, basi mtu anachukua ile kauli ambayo dalili yake ina nguvu. Katika hali hii Ibn Mas´uud ana kauli nyingine kuliko Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa).  Ibn Mas´uud amefasiri Kauli ya Allaah (Ta´ala):
إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا
"... isipokuwa yale yanayodhihirika..."
na kusema kuwa makusudio ni yale mavazi ya juu ambayo hakuna namna ya kuyaficha. Kwa hiyo ni wajibu kutafuta kauli yenye nguvu na kuitendea kazi.

 
24. Tafsiri ya Hadiyth ya Asmaa´

2- Hadiyth ya ´Aaishah ni dhaifu kutokana na sababu mbili:
Ya kwanza: Kuna mkato baina ya ´Aaishah na Khaalid bin Jurayk ambaye amepokea kutoka kwake. Kasoro hiyo ameiashiria Abu Daawuud mwenyewe pale aliposema:
"Khaalid bin Jurayk hakusikia kitu kutoka kwa ´Aaishah."
Abu Haatim ar-Raaziy amesema pia kuwa Hadiyth ina kasoro.
Ya pili: Kwenye mnyororo kuna Sa´iyd bin Bashiyr an-Naswriy ambaye alikuwa anaishi Damascus. Ibn Mahdiy na ukiongezea juu yake Ahmad wameacha mapokezi yake, Ibn Ma´iyn, Ibn-ul-Madiyniy na an-Nasaa´iy wamesema alikuwa ni dhaifu. Hivyo basi Hadiyth ni dhaifu na haiwezi kusimama na zile Hadiyth Swahiyh zinazowajibisha kujifunika.
Isitoshe jengine ni kwamba Asmaa´ bint Abiy Bakr (Radhiya Allaahu ´anhumaa) alikuwa na miaka ishirini na saba wakati wa Hijrah ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Alikuwa ni mwanamke mkubwa. Ni jambo lisilowezekana akaingia kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amevaa mavazi ya kubana yenye kuonesha zaidi ya uso na mikono na Allaah ndiye anajua zaidi. Na kama itakuwa Swahiyh basi ni lazima tukio hili liwe limetokea kabla ya kufaradhishwa Hijaab. Kwa sababu dalili za kujifunika ni zenye kutanua zaidi kutoka kwenye kianzio, kama tulivyotangulia kusema.

 
25. Tafsiri ya Hadiyth ya al-Fadhwl

3- Hadiyth ya Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) haitolea dalili yoyote ya kujuzusha kumtazama mwanamke ajinabi. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakumuitikia al-Fadhwl kwa kitendo chake;  bali aligeuza uso wake upande mwingine. Ndio maana an-Nawawiy ametaja katika tafsiri yake "as-Swahiyh" ya Muslim kwamba Hadiyth inatolea dalili juu ya uharamu wa kumwangalia mwanamke ajinabi. Haafidhw Ibn Hajar amesema katika "Fath-ul-Baariy" ya kwamba Hadiyth inatolea dalili juu ya uharamu wa kumwangalia mwanamke ajinabi na kuwa ni wajibu kushusha macho. ´Iyaadhw amesema kuwa baadhi ya wanachuoni wanasema sio wajibu ikiwa hakukhofiwi fitina lakini kitendo chake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa al-Fadhwl kinasema mengi kuliko maneno.
Lau mtu atauliza ni kwa nini basi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakumuamrisha mwanamke kufunika uso, udhahiri ni kwamba alikuwa katika Ihraam. Katika hali hii ni jambo ambalo halikuwekwa kwenye Shari´ah kwake kufunika uso ikiwa kama hachelei kuna ajinabi yeyote anayemwona. Kuna uwezekano vilevile Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwambia baada ya hapo. Kwa sababu tu haikupokelewa haina maana kwamba haikutendeka. Kwa sababu kukosekana mapokezi hakuna maana yanakosekana mapokezi.  Muslim na Abu Daawuud wamepokea kupitia kwa Jaabir bin ´Abdillaah al-Bajaliy (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesema:
"Nilimuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya mtazamo wa ghafla ambapo akasema: "Tazama kando." Au akaniamrisha nitazame kando."

 
26. Tafsiri ya Hadiyth ya mwanamke mwenye mashavu ya kupauka

4- Hadiyth ya Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh) haikutaja ni wakati gani jambo hili lilitokea. Aidha mwanamke huyu alikuwa ni mzee sana asiyetaraji tena kuolewa (na hivyo anaruhusiwa kuonesha uso tofauti na wengine) au ilitokea kabla ya kuteremshwa Aayah yenye kuwajibisha kujifunika. Aayah hiyo iko katika Suurat-ul-Ahzaab ambayo imeteremshwa miaka tano au siba baada ya Hijrah na swalah ya Idi iliwekwa katika Shari´ah miaka miwili baada ya Hijrah.

 
27. Khitimisho ya kitabu "al-Hijaab"

Nimeiingilia mada hii kwa undani kwa sababu watu wana haja ya kuwa na ujuzi kuhusu suala hili kubwa na la kijamii. Wengi ambao wanataka wanawake waoneshe nyuso zao hawakulifanyia suala hili utafiti na uhakiki utakikanao. Ni wajibu kwa kila mtafiti  kuwa mwadilifu na mwenye inswafu, asizungumze kabla ya kujifunza na asimame katika maoni ya dalili tofauti msimamo wa hakimu aliye kati ya watu wawili; asiwe ni mwenye kupendelea na ahukumu kwa elimu. Asichague upande bila ya dalili yake. Aangalie dalili za pande zote na asisukumwe na mtazamo ambao tayari kishakuwa nao mpaka akapetuka na kuvuka mipaka dalili zake na akafikia mpaka kupuuza na kufanya si lolote si chochote dalili za upande mwingine. Ndio maana wanachuoni wanasema inatakikana kwa mtu kustadili kabla ya [kuanza] kuonelea. Hili ni kwa sababu maoneleo yanatakiwa kuwa chini ya dalili na si kinyume chake. Ambaye anaonelea kabla ya dalili anakuja kuathirika na maoneleo yake ambayo yanamfanya ima kupitilia mbali maandiko yasiyomsapoti au kuyapotosha ikiwa hakuweza kuyatupilia mbali.
Mimi na wengine sote tumeona jinsi kutafuta dalili juu ya maoneleo kunavodhuru. Hilo humfanya mtu ikiwa ni pamoja na Hadiyth dhaifu kuonelea kuwa ni Swahiyh na kufasiri maandiko kwa njia zote ziwezekanazo ili tu kuyathibitisha maoni yake. Nilisoma makala ya mwandishi mmoja ambaye alitumia hoja Hadiyth ya ´Aaishah jinsi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alivomwambia Asmaa´ bint Abi Bakr (Radhiya Allaahu ´anhum):
"Ee Asmaa´! Wakati mwanamke anapobaleghe hatakiwi kuonesha chochote isipokuwa hiki na hiki" na akaashiria uso na vitanga vyake vya mikono."
Hadiyth imepokelewa na Abu Daawuud. Mwandishi huyo amesema kuwa wanachuoni [wote] wamekubaliana juu ya kwamba Hadiyth ni Swahiyh. Si kweli. Ni vipi watakubaliana na wakati Abu Daawuud mwenyewe amesema kuwa kasoro ya Hadiyth kuna mkato katika mnyororo na Ahmad na maimamu wengine wamesema kuwa mpokezi mmoja ni dhaifu? Ushabiki na ujinga unamfanya mtu kutumbukia kwenye mtihani na maangamio. Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema:
Vua mavazi mawili
yanayomfanya yule mvaaji kudharauliwa na kudhalilishwa
Vazi lililokusanya ujinga
na juu yake kuna ushabiki - ubaya uliyoje wa vazi hili!
Jivishe uadilifu, nguo iliyo na fakhari zaidi
ambayo haijapatayo kuketi kwa mtu
Waandishi na watunzi wanapaswa kuhadhari kupuuza na kutelekeza dalili na kuwa na haraka ya kuzungumza pasina elimu na hivyo wakawa ni wenye kutumbukia katika wale ambao Allaah (Ta´ala) amesema:
فَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّنِ افْتَرَىٰ عَلَى اللَّـهِ كَذِبًا لِّيُضِلَّ النَّاسَ بِغَيْرِ عِلْمٍ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ
"Nani dhalimu zaidi kuliko yute anayemzulia Allaah uongo ili apoteze watu bila elimu? Hakika Allaah Hawaongozi watu madhalimu."
Vilevile asipuuzie dalili na kukadhibisha yenye kutolewa dalili ikawa ni shari chungumzima na akaja kutumbukia katika wale ambao Allaah (Ta´ala) amesema:
فَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّن كَذَبَ عَلَى اللَّـهِ وَكَذَّبَ بِالصِّدْقِ إِذْ جَاءَهُ ۚأَلَيْسَ فِي جَهَنَّمَ مَثْوًى لِّلْكَافِرِينَ
"Basi ni nani dhalimu zaidi kuliko yule aliyemsingizia uongo Allaah na akaukadhibisha ukweli ulipomjia? Je, kwani [Moto wa] Jahannam si makazi kwa makafiri?"
Ninamuomba Allaah (Ta´ala) atuoneshe haki na atuwafikishe kuweza kuifuata na atuoneshe batili na atuwafikishe kuweza kujiepusha nayo na atuongoze katika njia iliyonyooka. Hakika Yeye ni mwingi wa kutoa na Mkarimu. Allaah amsifu, ambariki na kumswalia Mtume wetu Muhammad, familia yake na Maswahabah zake wote.

Imeandikwa na Muhammad bin Swaalih al-´Uthaymiyn