Ndugu Yangu Kwa Mfano Wa Siku Hii Ya Qiyama Fanya Mema

Kitabu hiki kinazungumzia: Umuhimu wa kujiandaa kutokana na siku ya Qiyama, pia imeelezea kuhusu umauti, mambo ya kaburini na siku ya kufufuliwa.

اسم المادة: أخي لمثل هذا اليوم فاعمل


تأليف: أبو الحسن بن محمد الفقيه


الناشر: المكتب التعاوني للدعوة وتوعية الجاليات بالربوة


نبذة مختصرة: كتاب مترجم باللغة السواحيلية، فيه بيان أهمية الاستعداد لليوم الآخر، وفيه ذكر فيه أحوال الموت والحياة البرزخية ويوم النشور.


Ndugu Yangu
Kwa Mfano Wa Siku Hii Ya Qiyama Fanya Mema

[ Kiswahili - Swahili -السواحيلية ]

 


        
Mtunzi:
Abul-Hasani Muhammad Al-Faqiih


Mfasiri:
Abubakari Shabani Rukonkwa.

 

Kimerejewa na:
Yunus Kanuni Ngenda

 


أخي
لمثل هذا اليوم فاعمل

المؤلف:
فضيلة الشيخ: أبو الحسن محمد الفقيه

المترجم:
أبوبكر شعبان ركونكوا.

المراجع:
يونس كنون نغندا

 

 

 

 


YALIOMO:

1.    Utangulizi.
2.    Ndugu yangu kwa mfano wa siku Hii ya qiyama fanya Mema.
3.    Siku ya kutolewa roho.
4.    Siku ya kuingizwa kaburini.
5.    Siku ya kufufuliwa.

 

 

 

 

 

 

 

بسم الله الرحمن الرحيم

Ndugu Yangu
Kwa Mfano Wa Siku Hii Ya Qiyama Fanya Mema
    

        
Utangulizi:
Hakika sifa zote njema ni za Mwnyezi Mungu ambae tuna muhimidi, tunamuomba msaada na msamaha na tunajikinga kwake kutokana na shari za nafsi zetu na matendo yetu mabaya, mwnye kuongozwa na Mwenyezi Mungu hakuna wa kumpoteza na mwenye kupotezwa na Mwenyezi Mungu hakuna wa kumuongoa, na ninashahidilia kuwa hakuna Mola apasae kuabudiwa kwa haki isipokuwa ni Mwenyezi Mungu peke yake hana mshirika. Na ninashahidilia kuwa Muhammad (s.a.w) ni mja wake na Mtume wake.

Ndugu Yangu
Kwa Mfano Wa Siku Hii Ya Qiyama Fanya Mema

Amesemaa Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Hakika kwa Mola wako Mlezi ndio marejeo}. (Al-Alaq: 8).
Katika kitabu cha Mwenyezi Mungu kuna aya inayopasua maini na nyoyo za waja wa Mwenyezi Mungu wakweli zinainyenyekea aya hiyo, muumini wa kweli mwenye itikadi sahihi na yakini anapoizingatia aya hiyo moyo wake unatekwa na akili itashughulishwa na aya hiyo, na aya hiyo itakuwa ndiyo hima yake: Hakika ni aya ya kukhofisha na ni ukulele wa kutahadharisha, inakhofisha siku ambayo siyo kama masiku mengine na inazungumzia tukio la kufufuliwa watu wote.
Ni aya ambayo kwa sababu yake Mwenyezi Mungu alituma Mitume na akateremsha Vitabu na ndani ya siku hiyo watu watatengana, kundi moja litaingia Peponi na kundi jingine litaingia Motoni, aya hiyo ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na iogopeni Siku ambayo mtarudishwa kwa Mwenyezi Mungu, kisha kila nafsi italipwa ilicho chuma. Nao hawatadhulumiwa}. (Al-Baqra: 281).
Hakika ni siku ambayo kila nafsi itarejea kwa Mola na Muumba wake! Hikika ni siku ambayo nafsi zitahesabiwa na kila nafsi itahesabiwa kulingana na matendo yake, amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Basi anaye tenda chembe ya wema, atauona!* Na anaye tenda chembe ya uovu atauona!}. (Al-Zilzaal 7-8).
Ndugu yangu: Hakika siku hiyo ni siku ya Qiyama, siku ambayo Mitume watafazaika na maneno yao siku hiyo yatakuwa (Allahuma sallim sallim), mawalii watatetemeka siku hiyo kwa khofu na uwoga ni siku ya shida na tabu, siri zitafichuliwa siku hiyo na vitabu vya matendo vitagawiwa na viumbe watakuwa ktika fitna siku hiyo, amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Siku hiyo mtahudhurishwa-haitafichika siri yoyote yenu}. (Al-Haaqah: 18).
Ni siku ambayo watasimamishwa mashahidi, kuna nyuso siku hiyo zitakuwa nyeusi na nyingingine zitakuwa nyeupe, amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Siku ambayo kila nafsi itakuja jitetea, na kila nafsi italipwa sawa sawa na a'mali ilizo zifanya, nao hawatadhulumiwa}. (Al-Nahli: 111).
Ni siku ambayo mtoto atamkimbia baba yake na atamkana mama yake na ndugu yake na mkewe na mwanae, amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Kila mtu miongoni mwao siku hiyo atakuwa na lake la kumtosha}. (Abasa: 37).
Ni siku ya malipo na ni siku ya majuto, ni siku ya kubadilisha na ni siku ya mkutano, ni siku inayosogea na ni siku ya marejeo, ni siku ya hukumu na ni siku ya kupimwa matendo, ni siku ya kukata tamaa na ni siku ngum, ni siku ya kushuhudiwa na ni siku ya upambanuzi, ni siku ya kukimbiana na ni siku ambayo haina shaka ndani yake, ni siku isiyozuilika kwa Mwenyezi Mungu na hakuna nafsi itakayo zungumza isipokua kwa idhini yake Mwenyezi Mungu, sauti zitakuwa kimya kwa Mwenyezi Mungu hautosikika isipokuwa mnong'ono, kila mmoja siku hiyo atatarajia amani ya nafsi yake wala hatomjali aliye pembezoni mwake, atakua akisema: Nafsi yangu! Nafsi yangu!.
Ndugu yangu uko wapi wewe na siku hii? Ziko wapi kumbukumbu zako kutokana na hali ya siku hiyo? Iko wapi hima yako kutokana na mfazaiko wa siku hiyo na vitisho vyake!?.
Kutoka kwa Abuu Huraira (r.a) alisema Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w): (Watu watatokwa na jasho siku ya Qiyama mpaka jasho zao zitafika ardhini kiasi cha dhiraa sabini, na jasho litawameza mpaka kufikia katika masikio yao). Ameipokea hadithi hii Imamu Bukhar.
Amesema Ibrahim Al-Tamimy: [Vitu viwili vilinikatia ladha ya dunia: Kukumbuka Umauti na kukumbuka kusimamishwa mbele ya Mwenyezi Mungu].
Anasema Mshairi:
Ipigie mfano nafsi yako ikighafilika na umauti,
Itakavyokuwa siku ya Qiyama wakati mbingu inaondoka
Na wakati jua litakapo kunjwa kunjwa na likasogezwa
Karibu na vichwa vya wanadamu.
Na pindi nyota zitakapo dondoka na zikazunguka badala
Ya kuwaka. Na bahari zitakapo ripuka kutokana na khofu
Utaziona kama moto mkubwa unavyowaka.
Na kumbuka milima itakapong'oka ikatoka sehemu yake,
Utaiona kama mawingu yanavyotembea.
Na pindi vitakapo gawiwa vitabu vya matendo,
Siri zote za wanadamu zitafichuka.
Na kumbuka mwanadamu Moto wa Jahannam utakapo washwa
Basi utakuwa ukiunguruma kwa ajili watu wenye madhambi.
Ndugu yangu: Kila kitu kina uhakika wake, na uhakika wa imani yako kwa siku hii ni kuibeba hima yako ndani ya moyo wako kutokana na siku hiyo na mawazo yako yaifanyie kazi siku hiyo, na uikumbuke mara kwa mara kwasababu ni siku ngum na kwa makafiri siyo nyepesi, amepata hasara mwenye kubeba dhulma siku hiyo na mwenye kughafilika na siku hiyo amepata hasara, amesema Mwenyezi Mungu Mtukfu: {(Aambiwe): Kwa hakika ulikuwa umeghafilika na haya; basi leo tumekuondolea pazia lako, na kwa hivyo kuona kwako leo ni kukali.}. (Qaaf: 22).
     Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukfu: {Basi nyinyi abuduni mpendacho badala yake Yeye. Sema: Hakika walio khasirika ni wale walio jikhasiri nafsi zao na ahali zao Siku ya Kiyama. Tambueni kuwa hiyo ndiyo khasara iliyo dhaahiri}. (Al-Zumar: 15).
Anasema Mshairi:
Ewe kijana mwenye kumuasi Mola wa A'rshi hivi unajua malipo ya mwenye maasi? Bisi ni Moto wa Jahannam wenye muungurumo na hasira siku atakapochukuliwa mwenye maasi na kutupwa ndani yake.
Ikiwa unaweza kuvumilia moto basi muasi Mwenyezi Mungu, na la sivyo usimuasi Mwenyezi Mungu, na yale uliyoyachuma katika maasi ilazimishe nafsi yako kuyaacha.
Siku Ya Kutolewa Roho
Ndugu yangu: Qiyama cha mtu kinasimama kwa kufa kwake, wakati huo ndio itaonekana nafasi yake na mafikio yake yatabainika, siku ya kufa kwake siri inafichuka na kubainika namna alivyo na matendo yake yanabainika hali yake, sifa yake na malipo yake yana nasibiana na matendo aliyoyafanya katika uhai wake.
      Wakati wa kutokwa roho: Ni wakati wa kuachana unaoshuhudiwa, ni wakati mwanadam anajionea ulimwengu wa ghaibu, basi anashuhudia na kuona Malaika wakimjia vile walivyo kutokana na matendo aliyonayo, na katika hadithi amesema Mtume (s.a.w): (Anapokaribia kufa muumini wanamjia Malaika wa rehma na Hariri nyeupe kisha wanasema kuiambia roho toka ukiwa umeridhia na umeridhiwa uende katika raha na manukato na Mola wako hajakukasirikia, baisi ile inatoka ikiwa na harufu nzuri ya miski wanapeana Malaika baadhi yao kwa wengine mpaka wanaifikisha katika mlango wa mbingu kisha Malaika wanasema uzuri ulioje wa harufu hii mliyokuja nayo kutoka ardhijni! Kisha wanaiweka katika roho za waumini, basi hao waumini wanamfurahia kuliko anavyomfurahia mmoja wenu mgeni anapo mtembelea, kisha wanamuuliza Fulani kafanya nini? na Fulani kafanya nini? Wengine watasema muacheni hakika alikuwa katika matatizo ya dunia, atakaposema kuwajibu atasema je! Hakuja huku? Watajibu alipelekwa katika mafikio yake ya Motoni. Na hakika makafiri wanapofikiwa na umauti wanajiwa na Malaika wa adhabu na kitambaa chepesi kisha wanasema kuiambia roho: toka haliyakuwa umechikia na umechukiwa uende kataka adhabu ya Menyezi Mungu, itatoka ikiwa na harufu mbaya kama ya mzoga, wataipeleka mpaka katika mlango wa ardhini watasema ubaya ulioje wa harufu hii? Kisha waiweke katika roho za makafiri).
Ndugu yangu: Mtu mwenye akili anazingatia mwisho wake na anaufanyia maandalizi mazuri, basi itakase nafsi yako kwa kufanya twaa, na itie manukato roho yako kwa kumridhisha Mola wako na kutekeleza amri zake na kujiepusha na makatazo yake, na kufanya haraka katika kutenda mambo ya kheri ikiwa inatarajia kuokoka siku itakapotolewa na kunyanyuliwa daraja wakati wa kufariki, hakika ya roho hazipati manukato isipokuwa kwa amali njema ambazo ndani yake ni kumpwekesha Mwenyezi Mungu na kujiepusha na ushirikina, anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Hakika shirki ni dhulma kubwa}. (Luqman: 13).
Matendo mazuri pia yanakusanya tabia nzuri na ibada zilizo sahihi ambazo zinafanywa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, mfano wa roho kama hizi Mwenyezi Mungu amezizungumzia katika Qur'an kwa kusema: {Wale ambao Malaika huwafisha katika hali njema, wanawaambia: Amani iwe juu yenu! Ingieni Peponi kwa sababu ya yale mliyo kuwa mkiyatenda}. (Al-Nnahli: 32).
Roho kama hizi ndiyo zitakazopokelewa na walinzi wa Pepo na huku wakisema: {Na walio mcha Mola wao Mlezi wataongozwa kuendea Peponi kwa makundi, mpaka watakapo fikilia, nayo milango yake imekwisha funguliwa. Walinzi wake watawaambia: Salaam Alaikum, Amani iwe juu yenu! Mmet'ahirika. Basi ingieni humu mkae milele}. (Al-Zzumar: 73).
Ndugu yangu: Katika kutokwa na roho ukweli wa matendo huwa unadhihirika na kubainika udhalili wa dunia, kwani hakuna kinachodhihiri kwa anayekufa chenye kumfaa isipokuwa isipokuwa matendo yake, na kwa kufa kwake ndiyo mwisho wa matendo yake, na kutokana na matendo atakayokufa nayo ndiyo atakayofufuliwa kwayo, kama ilivyokuja katika hadithi ya Mtume (s.a.w): (Mwenye kufa katika jambo, atafufuliwa katika jambo hilohilo). Ameipokea Haakim.
Ikiwa ni hivo ndugu yangu, wakati roho yako inatoka inaonyesha hali yako itakavyokuwa kaburini, siku ya kufufuliwa na siku ya kuhesabiwa, mtu mmoja aliambiwa wakati anakata roho: sema laa ilaha ila Llah! Akasema: sitonufaika na kauli hiyo, na mimi hakuna dhambi ambayo sijaifanya, kisha akakata roho na hakuweza kuitamka.
Na mtu mwingine aliambiwa: sema laa ilaha ila Llah! Akasema: haitanisaidia, sijawahi kuswali hata swala moja, kisha akakata roho na hakuweza kuitamka.
Na mtu mwingine aliambiwa: sema laa ilaha ila Llah! Akasema kila ninapotaka kutamka ulimi wangu unagoma kutamka.
Basi watu hao walizama katika maasi wakaitelekeza shahada na wakawa na mwisho mmbaya, tunamuomba Mwenyezi Mungu atupe salama.
Anasema Mshairi:
          Utaacha ibada kwa ajili ya kujishughulisha na dunia mpaka lini!
            Utakuwa mvivu wa kuacha ibada mpaka lini!
           Kila siku maovu yako yanaandikwa wewe huchoki?
           Ewe mwenye kuiadhibu nafsi yako,
           Na unachelewa kuwa mtu mwema.
           Basi jua kuwa kifo kinakujia haraka
           Na kaburi ndio sanduku la matendo.
Ndugu yangu fahamu ya kwamba hakika mwanadamu madamu anamatumaini ya maisha basi hawezi kuyakata matumaini yake ya kidunia, na huenda nafsi yake isimkubalie kuacha ladha za dunia na matamanio yake sawa ni ya halali au ya haramu na shetani anaipa matarajio ya kutubia mwisho wa umri wake, kifo kinapofika na akakata tamaa ya maisha ndipo anapozinduka na kujua kwamba alikuwa katika dimbwi la matamanio ya dunia, na wakati huo ndipo anapojuta majuto makubwa yanayokaribia kuiangamiza nafsi yake, na ndipo anapoomba kurejea duniani ili atubie na kufanya matendo mema, wakati huo ombi lake halitojibiwa, basi yatajikusanya kwake mambo mawili, uchungu wa kutokwa na roho na majuto ya kutokufanya mema.
Mwenyezi Mungu Mtukufu amewatahadharisha waja wake kutokana na hali hiyo ili wajiandae na umauti kabla haujawafikia kwa kufanya toba na matendo mema, amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na rejeeni kwa Mola wenu Mlezi, na silimuni kwake, kabla ya kukujieni adhabu. Kisha hapo hamtanusuriwa*Na fuateni yaliyo bora kabisa katika yale yaliyo teremshwa kwenu kutoka kwa Mola wenu Mlezi, kabla haijakujieni adhabu kwa ghafla, na hali hamtambui*Isije ikasema nafsi: Ee! majuto yangu kwa yale niliyo poteza upande wa Mwenyezi Mungu, na hakika nilikuwa miongoni mwa wanao fanya maskhara!}. (Al-Zzumar: 54-56).
Alisikika mmoja katika watu waliokuwa wakitokwa na roho akijipiga usoni mwake huku akisema: Ee majuto yangu kwa yale niliyo poteza upande wa Mwenyezi Mungu, na hakika nilikuwa miongoni mwa wanao fanya maskhara.
Na akasema mwingine wakati wa kufa kwake: dunia imenishughulisha mpaka umri wangu umeondoka.
Na akasema mwingine wakati wa kufa kwake: yasikudanganyeni maisha ya dunia kama yalivyo nidanganya mimi, amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Mpaka yanapo mfikia mmoja wao mauti, husema: Mola wangu Mlezi! Nirudishe* Ili nitende mema sasa badala ya yale niliyo yaacha. Wapi! Hii ni kauli aisemayo yeye tu. Na nyuma yao kipo kizuizi mpaka siku watapo fufuliwa}. (Al-Muuminun: 99-100).
Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: { Na toeni katika tulicho kupeni kabla hayajamfikia mmoja wenu mauti, tena hapo akasema: Mola wangu Mlezi! Huniakhirishi muda kidogo nipate kutoa sadaka, na niwe katika watu wema?* Wala Mwenyezi Mungu hataiakhirisha nafsi yoyote inapo fika ajali yake; na Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda}. (Al-Munafiquun: 10-11).
Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na watatiliwa kizuizi baina yao na hayo wanayo yatamani, kama walivyo fanyiwa wenzao zamani. Hakika hao walikuwa na shaka ya kutia wasiwasi}. (Sabaa: 54).
Jopo la wanachuoni wema waliotangulia akiwemo Omar bin Abdul-Aziz wameifasiri aya hii kwamba, hao watu waovu waliotajwa katika aya waliomba toba wakati milango ya toba imeshafungwa.
Amesema Al-Hasan: Muogope Mwenyezi Mungu ewe mwanadamu, yasikupate wewe mambo mawili, uchungu wa mauti na majuto ya kutokufanya mema.
Amesema Ibn Samak: Tahadhari na uchungu wa mauti na mshangao, kwa kifo kukujia ghafla hali ya kuwa upo katika upotofu, utakayoyapata na utakayoyaona miongoni mwa adhabu hayana mfano wake. (Latwaaif Al-maarif, cha Ibn Rajab, ukurasa wa 575).
Siki Ya Kuingizwa Kaburini
Siku hiyo ndugu yangu kuonekana kwa mtu duniani kutaisha, ndugu zake watambeba wakiwa wanalia, watamuweka kaburini na kumfukia na mchanga, na watakaa siku chache wakihuzunika na kisha watamsahau.
Ama aliyezikwa, kwa hakika ameingia katika ulimwengu wa barzakh, na amekalishwa tangu kuingia kwake kaburini kwa ajili ya kuulizwa, amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Basi anaye tenda chembe ya wema, atauona*Na anaye tenda chembe ya uovu atauona!}. (Al-Zzilzaal: 7-8).
Sogea karibu ndugu yangu tuishi na mawaidha ya Mtume (s.a.w) yanayobainisha mafikio ya mwanadamu katika kaburi lake, na yanatupa habari juu ya yale yanayojiri katika kaburi kutokana na mambo tusiyoyajua, anasema Mtume (s.a.w): (Hakika maiti anapolazwa kaburini, anasikia nyayo za waliomsindikiza pindi wanaporudi, akiwa ni muumini swala yake inakuwa katika kichwa chake, na swaumu inakuwa upande wake wa kulia, na zaka inakuwa upande wake wa kushoto, na matendo yake ya kheri miongoni mwa sadaka, swala, wema na kuwafanyia watu mambo mazuri, yanakuwa miguuni mwake, swala itasema: upande wangu hakuna nafasi ya kuingia, na swaumu itasema: upande wangu hakuna nafasi ya kuingia, kisha zaka itasema: upande wangu hakuna nafasi ya kuingia, na matendo yake mema yaliyo upande wa miguuni yatasema: upande wangu hakuna nafasi ya kuingia, kisha antambiwa akae! Naye atakaa, utaletwa mfano wa jua na atatoa idhini lizame, kisha ataulizwa: unaonaje kuhusu huyo aliyekuwa kabla yenu unasemaje kuhusu yeye na unamshahidilia nini? Atasema: niacheni mpaka niswali. Kisha watamwambia: hakika utaswali tujibu tunayokuuliza. Unaonaje kuhusu huyo aliyekuwa kabla yenu unasemaje kuhusu yeye na unamshahidilia nini? Mtume (s.a.w) akasema: yule mtu atasema: Muhammad! Ninashahidilia kuwa ni Mtume wa Mungu, na hakika alikuja na haki kutoka kwa Mola wake, kisha ataambiwa: wewe uliishi katika imani hiyo, na ulikufa na imani hiyo, na utafufuliwa na imani hiyo Mwenyezi Mungu akipenda, kisha atafunguliwa mlango miongoni mwa milango ya Pepo, na kisha ataambiwa: haya ndiyo makazi yako na ndiyo aliyokuandalia Mwenyezi Mungu.
Basi atazidi kuwa na tamaa na furaha, kisha litapanuliwa kaburi lake dhiraa sabini na litatiwa nuru ndani yake na kiwiliwili kitarejeshwa kama kilivyokuwa mwanzo, na inawekwa roho yake katika roho za watu wema mfano wake, zinakuwa kama ndege waliowekwa katika miti ya Peponi, na hiyo ndio maana ya kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Mwenyezi Mungu huwatia imara wenye kuamini kwa kauli ya imara katika maisha ya dunia na katika Akhera}.(Ibrahim: 27).
Na hakika kafiri atakapojiwa na Malaika katika kaburi lake upande wake wa kichwani, kuliani mwake, kushotoni mwake na miguuni mwake hawatakuta kitu chochote katika matendo mema, kisha ataambiwa akae! Naye atakaa akiwa mwoga na huku akitetemeka kisha ataulizwa: Unaonaje kuhusu huyo aliyekuwa kabla yenu unasemaje kuhusu yeye na unamshahidilia nini? Atajibu: Mtu gani? Na wala hatajua jina lake, ataambiwa Muhammad! Atajibu: sijui! Nilikuwa nikisikia watu wakisema nami nikasema kama wanavyosema, kisha ataambiwa: wewe uliishi katika imani hiyo, na ulikufa na imani hiyo, na utafufuliwa na imani hiyo Mwenyezi Mungu akipenda, kisha atafunguliwa mlango miongoni mwa milango ya Moto, na kisha ataambiwa: haya ndiyo makazi yako ya Motoni na ndiyo aliyokuandalia Mwenyezi Mungu, basi atazidi kuwa na majuto na maangamio, kisha atafunguliwa mlango miongoni mwa milango ya Pepo na ataambiwa haya ndiyo makazi yako aliyokuandalia Mwenyezi Mungu laiti kama ungemtii, basi atazidi kuwa na majuto na maangamio, kisha atabanwa katika kaburi lake mpaka mbavu zake zitofautiane, hayo ndiyo maisha ya dhiki aliyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na atakaye jiepusha na mawaidha yangu, basi kwa yakini atapata maisha yenye dhiki}. (Twaha: 124).
Ndugu yangu: Jiandae kwa ajili ya kuulizwa na kukutana na vitisho hivyo, hakika kaburi ni nyumba ya kwanza ya akhera, na ndani yake utadhihiri ukweli wa matendo.
Othman bin Affaan (r.a) alikua akisimama katika makaburi analia mpaka ndevu zake zinalowa, akaulizwa: Mbona unapokumbuka Pepo na Moto hulii lakini unaposimama makaburini unalia? Akasema: Nilimsikia Mtume (s.a.w) akisema: (Hakika kaburi ni nyumba ya kwanza ya akhera, atakapookoka mtu kaburini basi yatakayokuja baada yake ni mepesi, na ikiwa hakuokoka kaburini basi yatakayokuja baada yake ni mazito).
Basi anajiandaa na ibada kutokana na siku kama hii mtu mwenye akili, ndani ya kaburi mwenye matendo mema atapata mafanikio na matendo maovu atapata hasara.
Siku Ya Kufufuliwa
Ndugu yangu fanya ibada kwa ajili ya siku hii ya kufufuliwa kwasababu ukombozi wa nafsi yako siku hiyo ni matendo yako mema, amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Wala hapana yeyote katika nyinyi ila ni mwenye kuifikia. Hiyo ni hukumu ya Mola wako Mlezi ambayo lazima itimizwe*Kisha tutawaokoa wale walio mchamngu; na tutawaacha madhaalimu humo wamepiga magoti}. (Mariyam: 71-72).
Mali zako siku hiyo hazita kufaa na dini yako hautoinunua kwa mali zako siku hiyo, na cheo chako siku hiyo hakitakunyanyua, amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Siku ambayo kwamba mali hayato faa kitu wala wana* Isipo kuwa mwenye kumjia Mwenyezi Mungu na moyo safi}. (Al-Sshuaraa: 88-89).
Na amesema Mtume (s.a.w): (Siku ya Qiyama ataambiwa mtu wa Motoni: Unaonaje laiti ungekuwa unamiliki vilivyoko ardhini ungevitoa fidia ili uokolewe na huu Moto? Atajibu: Ndiyo! Mwenyezi Mungu atamwambia: Umesema uongo! Nilitaka kwako wewe jepesi kuliko hilo, nilikukataza toka ukiwa katika mgongo wa Adam ya kwamba usinishirikishe na chochote, ukakataa na ukanishirikisha). (Swahihul-Jaamia: 8123).
Ndugu yangu kumbuka kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Kila nafsi itaonja mauti. Na bila ya shaka mtapewa ujira wenu kaamili Siku ya Kiyama. Na atakaye epushwa na Moto na akatiwa Peponi basi huyo amefuzu. Na maisha ya dunia si kitu ila ni starehe ya udanganyifu}. (Al-Imran: 185).
Na kumbuka kuwa utarejea kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, kama anavyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Hakika kwa Mola wako Mlezi ndio marejeo}. (Al-a'laq: 8).
Na utaulizwa kama anavyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na wasimamisheni. Hakika hao watasailiwa}. (Al-Swafaat: 24).
Basi kurejea kwako kufanyie hesabu, na maswali yako yaandalie majibu, na tahadhari usije ukafa katika hali ya kughafilika ukatamani wakati huo laiti ungezidishiwa umri kwa kusema: {Mpaka yanapo mfikia mmoja wao mauti, husema: Mola wangu Mlezi! Nirudishe* Ili nitende mema sasa badala ya yale niliyo yaacha. Wapi! Hii ni kauli aisemayo yeye tu. Na nyuma yao kipo kizuizi mpaka siku watapo fufuliwa}. (Al-Muuminuun: 99-100).
Na rehma na amani ziwe juu ya Mtume wetu Muhammad (s.a.w) na watu wake, na Maswahaba wake wote.